Sh3 bilioni kukarabati miundombinu ya maji Rombo

Rombo. Wakati Wilaya ya Rombo ikikabiliwa na upungufu wa maji lita milioni 12 kati ya milioni 22 zinazozalishwa kwa siku, Serikali imeanza ukarabati wa miundombinu ya zamani ya maji, ili kukabiliana na changamoto hiyo.

Akizungumza leo Jumapili, Desemba 8, 2024 wakati wa kukabidhi rola za maji katika eneo la Nalemuru, Rongai wilayani humo, Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Rombo (Rombowssa), Tumaini Marandu amesema Serikali imetoa zaidi ya Sh3 bilioni kwa ajili ya ukarabati huo.

“Tumeanza ukarabati wa miundombinu ya maji kwenye wilaya hii ya Rombo, ili tuboreshe huduma ya maji, ukarabati huu kwa wilaya nzima utagharimu zaidi ya Sh3 bilioni. Hatua hii itapunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya maji iliyopo,” amesema Marandu.

Amesema kwa eneo la Nalemuru na Tarakea ambalo ndilo lenye changamoto kubwa ya uchakavu wa miundombinu ya maji, Serikali imetenga Sh900 milioni kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ili wananchi waondokane na changamoto kubwa ya maji iliyopo sasa.

Aidha, amewataka wananchi wa wilaya hiyo, kuendelea kutunza na kuvilinda vyanzo vya maji ili huduma ya maji iwe endelevu.

Kwa upande wake, Mbunge wa Rombo ambaye pia ni Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema changamoto ya maji wilayani humo ni kubwa na kwamba suala la maji halipaswi kufanyiwa mchezo.

“Suala la maji tutasimama na kunyooka nalo mpaka tumalize changamoto hii Rombo, mahitaji ya maji Rombo ni makubwa na ndio changamoto namba moja,”amesema Profesa Mkenda.

Aidha, ameishukuru Serikali kuhakikisha inatenga fedha kwa ajili ya kushughulikia matatizo ya maji wilaya humo.

Akizungumzia mipango ya Serikali kupunguza changamoto ya maji wilayani humo, Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Raymond Mwangwala amesema kwa kipindi cha miaka mitatu, Serikali imetoa zaidi ya Sh 22 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji wilayani humo.

“Tunaingia mwaka 2025  tukiwa tumepunguza kwa  kiasi kikubwa upungufu wa maji kwenye wilaya yetu, tulikuwa tunauhitaji wa maji lita milioni 33 kwa siku, lakini sasa tunapokea maji lita milioni 21 hadi milioni 22 kwa siku, hivyo tuna upungufu wa maji lita milioni 11 hadi 12 kwa siku,” amesema Mwangwala.

Wakizungumzia changamoto ya maji, wananchi wa wilayani hiyo, wamesema wakati wa kiangazi wanalazimika kunywa maji machafu kutoka Mto Nalemuru, hali ambayo ni tishio kwa usalama wa afya zao.

John Joseph na Rosemary Kessi, wamesema kwa miaka mingi, hasa wakati wa kiangazi wamekuwa wakitumia maji machafu na wakati mwingine kulazima kutembea zaidi ya kilomita 15 kusaka maji safi na salama.

“Changamoto ya maji hapa kwetu ni kubwa, kwa sasa tunachota maji Mto Nalemuru, lakini wakati mwingine tunalazimika kutembea zaidi ya kilomita 15 kwenda misituni kutafuta maji,” amesema Rosemary.

Related Posts