MABAO mawili yaliyofungwa ndani ya dakika tano za kipindi cha pili, yaliitibulia Simba kutoka na ushindi ugenini baada ya kufungwa 2-1 na CS Constantine katika mechi ya raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mohamed Hamlaoui uliopo mji wa Constantine, Algeria.
Kipigo hicho kimekuwa ni muendelezo mbaya kwa timu za Tanzania baada ya juzi usiku, Yanga nao kufumuliwa mabao 2-1 ikiwa nchini humo na MC Alger ya Algeria, mechi iliyopigwa juzi ikiwa ni kipigo cha pili kwa timu hiyo baada ya awali kufumuliwa nyumbani kwa idadi kama hiyo na Al Hilal ya Sudan ilikuwa uwanjani usiku wa jana kuumana na TP Mazembe ya DR Congo.
Katika mchezo wa jana kocha Fadlu Davids aliwaanzisha mabeki wa kati watatu, Abdulrazak Hamza, Chamou Karaboue na Fondoh Che Malone waliosaidia na mabeki wa pembeni Shomary Kapombe na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.
Eneo la kiungo alianza na Fabrice Ngoma na Augustine Okejepha, huku eneo la mbele likiwa linaongozwa na Leonel Ateba akisaidiana na Jean Charles Ahoua na Kibu Denis ambao waliivuruga ngoma ya wenyeji hasa kipindi cha kwanza ambacho Simba ilitawala kwa sehemu kubwa sawa na ilivyokuwa kipindi cha pili.
Tofauti na kikosi ambacho kilianza kwenye mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi dhidi Onze Bravos Do Maquis ya Angola, kocha wa Simba, Fadlu Davids aliamua kufanya mabadiliko ya wachezaji wawili ambao ni Steven Mukwala na Ladaki Chasambi huku wakianza Leonel Ateba na Chamou Karaboue.
Msauzi huyo, aliamua kuanzisha kikosi cha kimkakati ambacho kilionekana kuwa na idadi kubwa ya wachezaji (8) wenye uwezo wa kulinda ambao ni Shomary Kapombe, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Che Malone, Chamou Karaboue, Abdulrazack Hamza, Fabrice Ngoma, Kibu Denis na Augustine Okejepha.
Imewezekanaje? ukuta wa Simba ulikuwa na mabeki wa tano, watatu wa kati, Che Malone, Hamza na Karabou mmoja alikuwa akiibia kwa kusogea eneo la kiungo ambalo lilikuwa na Ngoma pamoja na Okejepha.
Idadi ya wachezaji Simba wakati wakishambuliwa ilikuwa kubwa zaidi ya wachezaji sita walikuwa nyuma lakini wakati wakiwa na mpira mambo yalikuwa yakibadilika, Ahoua, Kibu na Ateba ndio wachezaji wa kwanza ambao walikuwa wakivuka nusu ya wapinzani wao, Kapombe na Tshabalala wakiongeza idadi ya wachezaji kushambulia, nyuma wakibaki, Malone, Karaboue na Hamza kabla ya mpango kubadilika kipindi cha pili.
Pambano hilo lilianza huku ikinyesha mvua kubwa, ambayo haikuzizuia timu hiyo kutandaza soka tamu kila moja ikitengeneza mashambulizi ya kushtukiza kwa dakika 10 za awali kabla ya Simba kutawala mchezo kwa kulisakama zaidi lango la wenyeji.
Juhudi za Simba zilizaa matunda dakika ya 24 wakati nahodha Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ alipoitanguliza kwa bao tamu lililotokana na krosi dongo iliyoenda kusindikizwa na kipa Kheireddine Boussouf aliyeamini anaupangua mpira huo na kuuzamisha wavuni.
Tshabalala alipiga mpira huo akiwa pembeni baada ya kugongeana vyema na Ahoua na kutesti zali baada ya kumchungulia kocha wa Constantine ambaye hakuamini kama ametunguliwa bao la mapema.
Bao hilo liliongeza kasi ya mchezo huo, kila timu ikisaka bao, lakini hadi dakika 45 za kwanza zinaisha Simba ilikuwa mbele kwa bao hilo 1-0.
Kipindi cha pili kilianza kwa wenyeji kushambulia kwa kasi na kufanikiwa kutumia dakika tano tu, kusawazisha bao na kuongeza jingine la pili.
Bao la kusawazisha la Constantine liliwekwa kimiani na beki Hamza aliyejifunga katika harakati za kuokoa mpira dakika ya 48 na wakati Simba ikijiuliza imefungwaje, Brahim Dib aliiandika timu hiyo bao la pili dakika ya 50 na dakika saba baadae Wekundu hao walipata pigo kwa Hamza kuumia na kutolewa uwanjani.
Nafasi ya beki huyo wa kati ilichukuliwa na Debora Mavambo kabla ya kocha Fadlu kuwatoa kwa mpigo wachezaji wawili, Leonel Ateba na Tshabalala na nafasi zao kuchuliwa na Valentin Nouma na Steven Mukwara kabla ya kumtoa tena na kumuingiza Edwin Balua aliyechukua nafasi ya Okejepha.
Matokeo hayo yameifanya Simba kubaki na pointi tatu na kushika nafasi ya tatu baada ya Bravos do Maquis ya Angola kushinda nyumbani kwa mabao 3-2 dhidi ya CS Sfaxien, huku CS Constantine ikiongoza msimamo wa kundi A ikiwa na pointi sita kwani ilishinda pia mchezo wa kwanza dhidi ya Watunisia.
Simba inarudi nyumbani kwa ajili ya mechi ya raundi ya tatu dhidi ya CS Sfaxien mchezo utaopigwa Jumapili ijayo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
CS CONSTANTINE: Boussouf, Meddahi, Baouche, Bellaouel, Boudrama, Merba, Benchaira, Dib, Benchaa, Tahar na Kaibou
SIMBA: Camara, Kapombe, Tshabalala, Chamou, Che Malone, Hamza, Ngoma, Okejepha, Ateba, Ahoua na Kibu.
Katika mechi nyingine za michuano hiyo, RS Berkane ya Morocco ilishinda ugenini kwa mabao 3-1 dhidi ya Stellanbosch ya Afrika Kusini, huku ASEC Mimosas ya Ivory Coast ilitoshana nguvu na Orapa United ya Botswana kwa kutofungana, huku CD Luanda ya Angola na Stade Malien ya Mali zilitoka sare ya 1-1.