Dar es Salaam. Familia ya aliyekuwa mtumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Aman Simbayao imesema inamuachia Mungu kwa kile kilichotokea kwa ndugu yao, huku Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba akitaka inunuliwe bondi ya Sh200 milioni kusomesha watoto.
Simbayao alifariki Desemba 5, 2024 katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam (MNH) alipokuwa akipatiwa matibabu, baada ya kushambuliwa Desemba 5, 2024 na wananchi wenye hasira kali eneo la Tegeta kwa Ndevu.
Akizungumza kwa niaba ya familia, mjomba wa marehemu Aman Kamguna amesema: “Kama wanafamilia hatuna cha kusema, tunamwachia Mungu.”
“Kijana wetu hatunaye, ameacha familia na watoto wadogo ambao sasa ni yatima, ikiwezekana hawa wawili wadogo wasomeshwe hawana msaada tena,” amesema kwa huzuni.
Amesema, binti wa kike wa marehemu aliyemtaja kwa jina la Najma alimuuliza swali kuhusu baba yake.
“Aliniambia babu, sijui nifanyeje? Kama baba (Simbayao) angekuwa ni mgonjwa ningekuwa nakwenda kumjulia hali, lakini hayupo tena, nikamwambia jikaze twende kumhifadhi kwenye nyumba yake ya milele,” amesema kwa huzuni akiomba watoto hao wasaidiwe kwenye elimu na afya.
Akitoa salamu za mwajiri, Kamishina Mkuu wa TRA, Yusuph Juma Mwenda amesema Mamlaka hiyo imeambiwa mke wa marehemu ni mjasiriamali.
“Aman ameacha mjane na watoto wadogo, licha ya taratibu nyingine za kisheri za kuwasaidia, TRA inafanya utaratibu kumuwezesha mjane aendelee kuishi.
“Ni mjasiriamali na sisi tuna huduma nyingi tutaona namna ya kumuajiri TRA ili aendelee kuwalea watoto wake,” amesema Mwenda.
Ameongeza kuwa kuhusu bima ya afya, wataona namna ya kuishughulikia ili watoto hao waendelee kupata matibabu na suala la elimu analiacha kwa Waziri Mwigulu Nchemba.
Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba ametaka zichangwe Sh200 milioni kwa ajili ya kununua bondi itakayowasaidia watoto Simbayao akisema wakati kukiwa na mchakato huo, atawachukua watoto wa marehemu na kuwasaidia binafsi.
Mwigulu amesema ofisi yake itawasilisha rambirambi, pia itawasilisha mchango wa kuanzisha mfuko wa kununua bondi ili kuwasaidia watoto.
“Wizara tutachangia, inatakiwa ipatikane milioni 200 ili kuweka bondi kwa ajili ya watoto wa marehemu,” amesema Mwigulu akiahidi kuendekea kuwasaidia.
Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema eneo ambalo mtumishi huyo alipigwa na kusababisha kifo chake litasafishwa na damu ya Simbayao iliyomwagika kwenye eneo hilo itazungumza.
“Lile eneo litasafishwa, msiniulize litasafishwa kwa namna gani ila litasafishwa, lazima damu iliyomwagika inene, mwili wa Amani utanena,” amesema.
Amesema hajawahi kuwa kiongozi legelege, hivyo eneo hilo la Tegeta kwa Ndevu na damu iliyomwagika ya Simbayao vitasafishwa.
“Kuna watu wamezoea kutii sheria kwa shuruti, mambo hayo yatapatiwa majibu muda si mrefu,” amesema Chalamila kwa msisitizo akisisitiza watumishi hao wa TRA walijitambulisha.
“Yule bwana (waliyekwenda kumkamata) aligoma akawapigia simu wanzake mwisho wa siku kikatokea hicho kikichotokea,” amesema Chalamila huku akishauri watumishi wa TRA kote nchini kuichangia familia ya marehemu Sh10,000 na kununja bondi ambayo itawasaidia watoto kusoma.
Desemba 7 akitoa taarifa wa umma, Kamanda wa Jeshi la Polisi, Kanda Maalumu Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema jeshi hilo, litawashughulikia wale wote wanaofanya makosa kinyume cha utaratibu, lakini wakitaka kukamatwa wanasingizia wanataka kutekwa.
Alisema Jeshi hilo halitawavumilia watu wanaotaka kujenga tabia ya kuwashambulia watumishi wa Serikali wakati wanapotekeleza majukumu yao kisheria.
Muliro alisema licha ya watumishi wa Serikali kufuata taratibu za kiutendaji, bado kuna tabia inataka kujengeka ‘ya watu kutaka kuwashambulia kwa sababu mbalimbali zisizokubalika.’
Desemba 5 lilitokea shambulio hilo wakati watumishi hao wakiwa kwenye majukumu ya kawaida ya kudhibiti ukwepaji kodi, eneo la Tegeta kwa Nyuki.
Tukio hilo lilitokana na maofisa hao kulizuia gari alilokuwa anaendesha dereva anayeshikiliwa mpaka sasa, kwa ajili ya ukaguzi wa magari yaliyoingia nchini bila kulipiwa kodi.”
Kwa mujibu wa TRA, gari hilo aina ya BMW x6 lenye namba T239 DHZ lilibainika kutokuwa ndani ya mfumo wa TRA na watumishi hao walipojaribu kulizuia, kuliibuka mzozo hadi dereva akipiga kelele kuomba msaada, akidai anatekwa.
Awali, Mkurugenzi wa huduma kwa mlipakodi TRA, Richard Kayombo aliliambia Mwananchi kuwa watumishi waliojeruhiwa walikuwa maofisa wa forodha na walikuwa wakitekeleza majukumu yao kwa mujibu wa Sheria ya Utawala wa Forodha wa Afrika Mashariki kuanzia kifungu 149 hadi 153.
Alisema maofisa hao wanapotekeleza majukumu yao, hawahitaji kibali chochote cha mahakama.