KIKOSI cha Yanga ambacho juzi usiku kilipoteza tena mechi ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kufumuliwa 2-0 na MC Alger ya Algeria, imezipiga bao Simba na Azam zinazochuana nao katika kuwania ubingwa wa Ligi Kuu.
Kipigo cha juzi usiku kilikuwa cha pili mfululizo kwa Yanga iliyopo Kundi A, baada ya awali kulazwa 2-0 pia ikiwa nyumbani, lakini ikiwa na rekodi nzuri katika Ligi Kuu ikicheza ugenini ukilinganisha na Simba na vinara Azam hadi sasa.
Katika Ligi Kuu Bara msimu huu Yanga imecheza michezo 11 na sita kati ya hiyo ni ya ugenini, ambapo imeshinda yote kwa maana imekusanya pointi zake 18, huku ikiwa imefunga jumla ya mabao manane tena bila ya kuruhusu nyavu zake kutikiswa.
Michezo ya nyumbani Yanga inaonyesha imecheza michezo mitano na kati ya hiyo imeshinda mitatu na kupoteza miwili, ambapo safu ya ushambuliaji imefunga mabao manane na kuruhusu manne, ikishika nafasi ya tatu kwenye msimamo na pointi zake 27.
Timu inayofuata kwa kukusanya pointi nyingi ugenini ni Azam FC ambayo imekusanya 17, katika michezo saba iliyocheza kati ya 13, ambapo timu hiyo inayoongoza Ligi imeshinda mitano na kutoka sare miwili, ikifunga mabao 11 na kuruhusu moja tu.
Katika michezo ya nyumbani Azam FC imecheza sita na kati ya hiyo imeshinda minne, sare mmoja na kupoteza mmoja pia huku ikikusanya pointi 13, ambapo imefunga jumla ya mabao manane na kuruhusu manne ikiongoza Ligi Kuu Bara na pointi zake 30.
Kwa upande wa Simba katika michezo ya ugenini imecheza mitano kati ya 11 msimu huu na kati ya hiyo imeshinda yote na kukusanya pointi 15, ambapo safu ya ushambuliaji ya kikosi hicho imefunga mabao sita bila kuruhusu nyavu zake kutikiswa.
Michezo sita iliyobaki ni ya nyumbani ambapo Simba imevuna pointi 13, ikishinda minne, sare mmoja na kupoteza pia mmoja huku safu ya ushambuliaji ya timu hiyo ikiwa imefunga mabao 16 na kuruhusu matatu, ikishika nafasi ya pili na pointi 28.
Kocha wa Azam FC, Rachid Taoussi alisema licha ya kiwango bora cha timu hiyo ugenini ila bado wana kazi kubwa ya kufanya kutokana na kutokuwa na mwenendo mzuri nyumbani, ingawa walipofikia anashukuru jitihada za kila mmoja wao.
“Ukiangalia michezo yetu miwili ya mwisho nyumbani utaona ufanisi wa mwisho ni mdogo kutokana na nafasi tunazotengeneza, tunaendelea kupambana ili kurekebisha changamoto hizo siku baada ya siku,” alisema Taoussi ambaye kitaaluma ni daktari.
Kwa upande wa kocha wa Simba, Fadlu Davids alisema muunganiko mzuri wa safu ya kiungo na mabeki ndio imekuwa chachu ya mwenendo mzuri wa matokeo hayo ugenini, jambo ambalo anahitaji kuliona likiendelea pia katika michezo yao ya nyumbani.