Saa 6 za kesi ya kina Shilton, yapangwa kusikilizwa Feb 10

HUWEZI kuamini, lakini ukweli ni kwamba serikali imetumia karibu saa sita kusoma maelezo ya mashahidi na vielelezo (commital proceedings) katika kesi ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroin zenye uzito kilo 34.89 inayomkabili mmiliki wa kituo cha Cambiasso Sport Academy, Kambi Seif na wenzake watano.

Saa hizo zimetumika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakati kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 43 ya mwaka 2023 ilipoitwa kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo  kabla ya kuhamishiwa Mahakama Kuu kwa hatua ya usikilizwaji.

Sababu ya kuchukua muda huo kuwasomea maelezo hayo ni kutokana na upande wa mashtaka kuwa na idadi kubwa ya mashahidi na vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani hapo.

Katika kesi hiyo, Serikali iliwasilisha jumla ya mashahidi 30 na vielelezo 89 ambavyo vinatarajia kutumika wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo huko Mahakama Kuu.

Mbali na Seif, washtakiwa wengine ni aliyekuwa kocha wa makipa wa Simba, Muharami Sultani ‘Shilton’ (40), Maulid Mzungu ‘Mbonde’ (54) mkazi wa Kisemvule na dalali wa viwanja na muuza nazi, ambaye ni kaka wa Shulton na Said Matwiko mkazi Magole.

Wengine ni John Andrew ‘Chipanda’ (40) mkazi wa Kitunda ambaye kazi yake ilikuwa ni kutafuta vijana wenye vipaji na kuwapeleka Cambiasso Sport Academy pamoja na Sarah Joseph, ambaye ni mke wa Matwiko.

Jopo la mawakili watatu wakiongozwa na wakili wa Serikali Mwandamizi, Grace Mwanga akisaidiana na mawakili wa Serikali, Roida Mwakamele na Judith Kyamba, waliwasomea maelezo hayo kwa kupokezana Desemba 5, 2024, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya.

Kesi hiyo ilianza kusikilizwa saa 6:20 mchana hadi saa 11:45 jioni ambapo upande mashtaka walianza kwa kuwasomea mashtaka yanayowakabili na kisha kuanza kusoma shahidi mmoja baada mwingine.

Baada ya hapo walisomea vielelezo 89, ambapo 36 kati ya hivyo ni vielelezo halisi na 53 ni nyaraka.

Katika mashahidi wanaotarajia kutoa ushahidi kwa upande wa mashtaka wapo maofisa kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), kocha msaidizi wa timu ya Simba, Seleman Matola, mahakimu wawili wa Mahakama ya Mwanzo Kigamboni na Ukonga, maofisa kutoka Brela, TRA, askari polisi, mtaalamu wa maandishi, ripoti mbalimbali ikiwamo, mtaalamu kutoka Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, wajumbe wa Serikali za Mitaa kutoka maeneo ambayo washtakiwa walikamatwa na fundi magari.

Mashahidi hao wa serikali, wanatarajia kutoa ushahidi wao katika Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, maarufu kama Mahakama ya Mafisadi.

Baada ya hapo, washtakiwa walipewa nafasi na wao wakaieleza mahakama kuwa watakuwa na mashahidi na vielelezo katika kujitetea huko Mahakama Kuu.

Hata hivyo, washtakiwa wote hawana wakili wa kuwatetea isipokuwa Seif pekee ambaye anatetewa na wakili Dominicus Nkwera.

Baada ya kusomewa maelezo hayo, Hakimu Lyamuya aliwaambia washtakiwa hao kuwa kesi yao tayari imeshapangiwa tarehe ya kusikilizwa Mahakama Kuu.

Hata hivyo, tofauti na kesi nyingine, kesi hii imepangwa kuanza kusikilizwa Februari 10, 2025 kwenye Mahakama Kuu na kwa muda wote huo hadi Februari mwakani, washtakiwa hao wataendelea kubaki rumande kwa sababu mashtaka yao hayana dhamana.

Washtakiwa baada ya kusomewa mashtaka yao, idadi ya mashahidi pamoja na vielelezo, Hakimu Lyamuya alisema kesi hiyo anaihamishia Mahakama Kuu Kitengo cha Uhujumu Uchumi na Makosa ya Rushwa, kwa ajili ya usikilizwaji.

Katika kesi ya msingi washtakiwa wanadaiwa kutenda makosa yao kati ya mwaka 2016, Aprili 15, 2021, Aprili 24, 2021, Oktoba 27, 2022 na Novemba 4, 2023 katika maeneo ya Kamegele wilaya ya Mkuranga na Dar es Salaam.

Related Posts