Rais Assad wa Syria, familia wapewa hifadhi Russia

Moscow. Rais wa Syria, Bashar Al-Assad, aliyepinduliwa jana Jumapili Desemba 8, 2024 pamoja na familia yake wamewasili nchini Russia walipopewa hifadhi.

Mashirika ya habari ya Russia yameripoti yakinukuu chanzo cha Ikulu ya Kremlin: “Rais Assad wa Syria amewasili Moscow. Russia imewapa (yeye na familia yake) hifadhi kwa misingi ya kibinadamu.”

Assad amepinduliwa baada ya waasi kuingia mji wa Damascus jana, huku wakidai ushindi dhidi ya utawala wake uliodumu kwa miaka takribani 24.

Kwa mujibu wa The Washington Post, baada ya utawala wake kusambaratika chini ya kundi la Kiislamu lenye silaha la Hayat Tahrir al-Sham, Assad alishangazwa na hali ya jeshi lake mwenyewe.

Rais wa Syria aliyepinduliwa, Bashar Al-Assad akiwa na familia yake

Katika hatua nyjngine, SkyNews imesema Moscow ilikua imefikia makubaliano na viongozi wa upinzani wa Syria.  Chanzo kimoja kimesema waasi hao wamehakikisha usalama wa vituo vya kijeshi vya Russia na taasisi za kidiplomasia nchini Syria.

Russia imesema Assad aliondoka Syria baada ya mazungumzo na makundi ya waasi yaliyoungana kumng’oa Rais huyo ambaye pamoja na familia yake wameitawala Syria kwa miaka zaidi ya 53.

Awali, kulikuwa na sintofayamu juu ya alipokimbilia Assad baada ya waasi kuutwaa mji wa Damascus hadi pale mamlaka za Russia ziliponukuliwa na mashirika ya habari kama TASS.

Makundi ya waasi ya Syria yalianza harakati za kumpindua Assad tangu mwaka 2011 na yaligonga mwamba, huku katika mapigano ya kipindi chote zaidi ya watu nusu milioni wameripotiwa kupoteza maisha.

Baada ya mapinduzi hapo jana kufanikiwa taarifa ambazo bado hazijathibitishwa zinamtaja Abu Mohammad al-Jolani kuwa kiongozi mpya wa Syria.

Related Posts