WAKATI dirisha la usajili likikaribia kufunguliwa, Singida Black Stars itaingia sokoni kusaka beki wa kati na mshambuliaji katika kukiongezea nguvu kikosi chake.
Singida ilianza msimu vizuri ikiongoza ligi kwa wiki kadhaa ikiwa chini ya kocha Patrick Aussems ‘Uchebe’, aliyewahi kuinoa Simba lakini baadaye nguvu yake ikaonekana kupungua na kushuka hadi nafasi ya nne.
Timu hiyo yenye jeuri ya fedha kwenye michezo 12 ya ligi iliyocheza,imeshinda saba, sare tatu na kupoteza miwili ikifikisha jumla ya alama 24.
Taarifa kutoka ndani ya idara ya ufundi ni kwamba Singida Black Stars itasajili kwa lazima beki wa kati baada ya kuona changamoto ya ubora kwa mabeki wake waliopo sasa.
Usajili huo ulishatajwa mapema hata kabla ya kumfuta kazi kocha Aussems ambaye naye alishataka kuona analetewa beki wa kati mwenye viwango.
“Tutasajili beki wa kati huu ni usajili wa lazima unnaona ambavyo pale kwa mabeki wa kati tunavyopata shida, kuna makosa mengi sana ukiondoa Tra BI (Antony) hawa mabeki wengine wamshindwakuwa na muendelezo mzuri wa viwango vyao,” alisema bosi huyo wa juu wa ufundi.
Endapo usajili huo utakamilika ina maana utawaweka kwenye wakati mgumu mabeki Edward Charles na Kennedy Juma, ambao ndio wamekuwa wakipishana kukaa benchi na kucheza.
Mbali na beki wa kati Singida pia itafanya msako wa kutafuta mshambuliaji wa kati mwenye makali ambaye atakuja kusaidiana na kinara wao wa mabao Mkenya Elvis Rupia.
Rupia ameshafunga mabao matano akizidiwa bao moja tu na kinara wa ufungaji kwenye ligi mshambuliaji wa Fountain Gate Seleman Mwalimu mwenye mabao sita, Mkenya huyo ndio uhai wa Singida katika kufunga mabao.
Nyuma ya Rupia wapo viungo Marouf Tchakei mwenye mabao matatu, Arthur Bada,Tra bi,Emmanuel Keyekeh wote wakifunga mabao mawili kila mmoja huku Damaro Camara na Ayoub Lyanga wakifunga bao moja kila mmoja.