TAASISI ya Wanawake na Samia Mkoa wa Dar es Salaam, imesema Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ni miongoni mwa mafanikio makubwa ambayo Tanzania inajivunia inapoadhimisha miaka 63 ya Uhuru wa Tanganyika.
Hayo yalielezwa na Makamu Mwenyekiti wa Taasisi hiyo, Hanifa Mrisho, alipoongoza wanachama wa taasisi hiyo kufanya usafi na kufariji wagonjwa katika hospitali mbalimbali mkoani Dar es salaam, ikiwa ni kuadhimisha miaka 63 ya Uhuru wa Tanganyika.
Hanifa, amesema Rais Dk. Samia, kushika uongozi wa ngazi ya juu ya Urais wa Tanzania ni mafanikio makubwa katika miaka 63 ya Uhuru ambayo wanawake hasa wanatakiwa kujivunia.
“Ni jambo ambalo wengi hawakutegemea katika kipindi hiki. Lakini tumempata Rais Dk. Samia na utendaji wake umejipambanua uwezo mkubwa wa wanawake katika uongozi,”amesema Hanifa.
Ameeleza, Taasisi ya Wanawake na Samia, itaendelea kumuunga mkono Rais Dk. Samia, katika kila hatua.
“Rais Dk. Samia, aliagiza sherehe hizi za uhuru tufanye kwa kupanda miti na usafi. Taasisi ya Wanawake na Samia, tuliona ni vyema tukafanya usafi katika Hospitali zetu za Mkoa wa Dar es salaam, kuona wagonjwa na kugawa zawadi mbalimbali kwa wagonjwa,”amesema.
Kuhusu uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwakani, Hanifa alihimiza wanawake kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kwani Rais Dk. Samia ameonesha njia.
Akizungumzia kuhusu mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri kupitia mapato yake ya ndani kwa vikundi vya wajasiriamali wanawake, vijana na wenye ulemavu, Hanifa aliwataka watanzania kujitokeza.
“Wasikae majumbani. Wajitokeze kwani zitawasaidia kujenga uchumi na kuchangia mapato ya serikali. Lakini wakikopa warejeshe,”amesema.
Mkurugenzi wa Idara ya Afya Wanawake na Samia Mkoa wa Dar es Salaam,Johari Kafuku, amesema taasisi hiyo inamshukuru Rais Dk. Samia, kwa uboreshaji mkubwa wa huduma za afya.
“Hata vifo vya mama na mtoto vimepungua Tanzania kwa sababu ya Rais Dk. Samia kuboresha huduma, hususan ujenzi wa hospitali, vituo vya afya na magari ya wagonjwa,”ameeleza Johari.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mnazi Mmoja, Linda Mukasa, amepongeza Taasisi ya Wanawake na Samia kwa kufanya usafi katika hospitali hiyo kwani usafi ni jambo mtambuka.