Msuva na matarajio Afcon 2025

Mshambuliaji mahiri wa Taifa Stars, Simon Msuva ameendelea kudhihirisha umuhimu wake kwa soka la Tanzania kwa mabao yake muhimu katika safari ya kufuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).

Mabao aliyofunga dhidi ya Ethiopia na Guinea yamechochea mafanikio ya Stars na kumkaribisha kwenye rekodi ya kihistoria ya Mrisho Ngassa, mfungaji bora wa muda wote wa Taifa Stars.

Huku akisalia na bao moja pekee kuifikia rekodi ya Ngassa, safari ya Msuva katika kikosi cha Stars ime-jaa mafanikio na changamoto nyingi, lakini kila mara ameibuka shujaa wa taifa.

Mashindano ya AFCON 2025 huko Morocco ni fursa nyingine kwake kuimarisha urithi wake kwa taifa na kuweka alama katika historia ya soka nchini.

 Rekodi ya Ngassa kwa mujibu wa TFF

Simon Msuva, ambaye kwa sasa anachezea Al-Talaba SC ya Iraq, amekuwa nguzo muhimu kwa Taifa Stars tangu alipoanza kulitumikia taifa mwaka 2012.

Katika mechi 94 alizocheza hadi sasa, ameifungia Tanzania mabao 24, akihitaji bao moja tu kufikia rekodi ya Mrisho Ngassa aliyefunga mabao 25 katika mechi 100 alizocheza kati ya mwaka 2006 na 2015.

Kufuzu kwa mara ya nne kwa Tanzania katika AFCON, huku Msuva akiwa shujaa wa mchezo dhidi ya Guinea, ni hatua nyingine inayodhihirisha mchango wa mshambuliaji huyu kwa Taifa Stars.

Rekodi yake ya kufunga mabao muhimu katika mechi kubwa si jambo la bahati, bali ni matokeo ya bidii, nidhamu, na uwezo wa kiufundi.

Akizungumzia hilo, Msuva anasema; “Mara zote nimekuwa nikipambana ili kuwa msaada kwa nchi yangu iwe kwa kufunga au kutoa asisti, nimejisikia fahari kuona jina langu ni miongoni mwa wachezaji ambao wapo kwenye orodha ya wafungaji wa muda wote.”

Mbwana Samatta, nahodha wa Taifa Stars, anashika nafasi ya tatu kwenye orodha ya wafungaji bora wa muda wote wa Stars akiwa na mabao 22 katika mechi 83.

Samatta, pamoja na wachezaji wengine kama John Bocco mwenye mabao 16 katika mechi 84, wamekuwa na mchango mkubwa kwa timu ya taifa, lakini sasa macho yote yako kwa Msuva, ambaye anaonekana kuwa tayari kuchukua nafasi ya kuwa mfungaji bora wa muda wote wa Taifa Stars.

Tanzania ilijihakikishia nafasi katika fainali za AFCON baada ya ushindi wa kihistoria dhidi ya Guinea, mchezo uliomalizika kwa ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Simon Msuva.

Bao hilo lilikuwa la kipekee, si tu kwa sababu lilihitimisha safari ya kufuzu, bali pia kwa jinsi lilivyoweka matumaini makubwa kwa mashabiki wa soka nchini.

Safari ya kufuzu haikuwa rahisi. Stars walipambana na timu ngumu kama Guinea na Ethiopia, lakini ushindi dhidi ya timu hizo ulitokana na umoja wa kikosi, mbinu za makocha, na ubora wa wachezaji wa-kongwe kama Msuva na Samatta.

Na hapa Msuva anaeleza kibarua kilivyokuwa kigumu; “Baada ya kupoteza mechi mbili dhidi ya DR Con-go hali ilikuwa tofauti, hatukuwa na namna zaidi ya kufanya vizuri katika michezo yetu miwili ambayo ilikuwa mbele yetu.

“Nakumbuka sikuwa sehemu ya timu wakati tukipoteza lakini nilikosa amani na niliwapa moyo wachezaji wenzangu na kuwaambia bado tunayo nafasi ya kufanya vizuri na kweli tulifanikisha mpango wetu kwa kuifunga Ethiopa kwa mabao 2-0 tukiwa Congo na tukawafunga Guinea tukiwa nyumbani.”

Ushindi katika michezo hiyo miwili uliifanya Stars kufikisha pointi 10 na kumaliza katika nafasi ya pili ya Kundi H nyuma ya DR Congo ambao walimaliza vinara wakiwa na pointi 12.

Akiwa mchezaji mwenye uzoefu mkubwa katika mashindano ya kimataifa, Msuva anaamini safari hii itakuwa tofauti huko Morocco akiwa na malengo makubwa. Msuva ameelezea kuwa anataka kutumia mashindano hayo si tu kwa kuonyesha uwezo wake binafsi, bali pia kusaidia timu kuandika historia mpya.

“Mimi kama mchezaji, nataka kuona Tanzania ikivuka hatua ya makundi. Tunapaswa kuonyesha kuwa tuna uwezo wa kushindana na timu bora Afrika. Kila mmoja wetu ana jukumu la kuhakikisha tunatimiza ndoto hii,” anasema Msuva. 

Mbali na jukumu lake la kufunga mabao, Msuva pia atakuwa kiongozi muhimu kwa wachezaji chipukizi ndani ya kikosi. Uzoefu wake wa kucheza soka la kimataifa, hasa akiwa Al-Talaba SC ya Iraq, unamweka kwenye nafasi nzuri ya kuwasaidia vijana kujifunza na kukua kimchezo.

Katika historia ya Taifa Stars, Erasto Nyoni ndiye anayeongoza kwa kucheza mechi nyingi zaidi akiwa na mechi 107 na mabao saba, akifuatiwa na Mrisho Ngassa mwenye mechi 100. Kelvin Yondani anashika nafasi ya tatu akiwa amecheza mechi 97, huku Simon Msuva akifuatia kwa mechi 94.

Wachezaji wengine waliotoa mchango mkubwa ni pamoja na John Bocco, aliyefunga mabao 16 katika mechi 84, na Mbwana Samatta, ambaye ameifungia Stars mabao 22 katika mechi 83.

Related Posts