Mafuta yashuka Zanzibar ikikaribisha uwekezaji zaidi

Unguja. Wakati mafuta ya petroli na dizelI yakishuka bei, Serikali imesema itaendelea kuweka mazingira wezeshi kuhakikisha upatikanaji wa huduma hiyo unazidi kuimarika.

Lakini pia imesema inawakaribisha wawekezaji zaidi kuwekeza katika nishati hiyo hususani kisiwani Pemba.

Bei ya petroli imeshuka kutoka Sh2,882 hadi Sh2,775 ikiwa ni tofauti ya Sh107 sawa na asilimia 3.72, huku dizeli ikishuka kutoka Sh3,033 hadi Sh2,892 tofauti ya Sh141 sawa na asilimia 4.65.

Kwa mujibu wa  taarifa ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (Zura), mafuta ya ndege yameshuka bei kutoka Sh2,538 hadi Sh2,414 ikiwa ni tofauti ya Sh124 sawa na asilimia 4.88.

Meneja wa kitengo cha Uhusiano Zura, Mbaraka Haji akizungumza leo Jumatatu Desemba 9, 2024, amesema kupungua kwa nishati hiyo kumetokana kupungua kwa wastani wa bei za mafuta kwenye soko la dunia.

“Pia Serikali imekuwa ikichukua jitihada mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupunguza tozo, na kuweka fidia ili kuwapuguzia makali wananchi,” amesema Haji.

Naye Waziri wa Maji, Nishati na Madini, Shaib Hassan Kaduara akizungumza wakati akifungua kituo cha Mafuta cha Puma Unguja mapema leo, amesema katika kuhakikisha upatikanaji wa nishati nafuu na zenye ubora kisiwani humo, kunahitajika kujengwa vituo vya mafuta ambavyo vitasaidia kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali za kupata nishati safi kwa wote.

“Katika kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa ya nishati nafuu na zenye ubora kisiwani hapa, ni lazima kujengwe vituo vya mafuta kwa lengo la kuwasogezea wananchi hiduma hizi na kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali kupata nishati safi kwa wote,” amesema Kaduara.

Pia, amefurahishwa kuona lengo la kampuni hiyo ni kuimarisha huduma zake katika maeneo ambayo bado hayajafikiwa ya huduma za nishati ikiwemo kisiwani Pemba.

“Nimetaarifiwa kuwa mnafanya tathmini maeneo ambayo hayajafikiwa ikiwemo Kisiwa cha Pemba, ninaomba huduma hizo zianzie Wilaya ya Chake Chake, Mkoa wa Kusini Pemba, na wengine waige waje kuwekeza upande wa nishati katika ksiwa hicho,” amesema Kaduara.

Amesema Serikali ipo tayari kushirikiana kupeleka huduma hizo kisiwani Pemba, ili wananchi wanufaike kupata huduma za uhakika za nishati.

Vilevile, amesema kampuni hiyo imeonesha uwajibikaji wa huduma za nishati na kuimarisha huduma za kijamii ikiwemo kuajiri wafanyakazi wazawa.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Puma Energy Tanzania, Fatma Abdalla amesema kituo hicho kimegharimu Sh2.5 bilioni hadi kukamilika kwake na kituo hicho ni ishara ya kujizatiti na kutoa huduma bora kwa wananchi.

Pia, amesema kituo hicho kipya cha huduma ni mwendelezo wa kuisaidia Zanzibar kukidhi mahitaji ya nishati kwa wakazi na wafanyabiashara wake.

“Zanzibar inaendesha shughuli za utalii, uchumi wa buluu, kilimo na usafirishaji wakati sekta hizo zikishamiri mahitaji ya ufumbuzi wa nishati ya kuaminika  yanahitajika,” amesema Fatma.

Amesema ajenda ya kampuni ni kuifanya Zanzibar kuwa suluhisho la nishati kwa kiwango cha kimataifa na kuchangia katika ajira za ndani, na kujiimarisha kuwa mshirika wa kutegemewa katika maendeleo.

Katika kuendeleza utoaji wa huduma, kampuni hiyo imeiomba Serikali iwapatie maeneo ya uwekezaji ya nishati mbalimbali ikiwemo mafuta ya gari na anga.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa bodi  Kampuni hiyo, Dk Majige Selemeni amesema wanatambua kwamba upatikanaji wa huduma za nishati ndio  msingi imara wa maendeleo.

Kituo hicho ni sehemu ya mkakati wa kupanua wigo katika kanda zote kuhakikisha huduma zao zinafikiwa ili kutoa mafuta yenye ubora na salama.

Naye, Bodaboda wa kituo cha Fuoni Melitano, Asaa Shaaban amesema awali ilikuwa wanaenda masafa marefu kupata huduma hiyo ila kwa sasa itakuwa ahueni kwa upande wao.

Related Posts