Miaka 13 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe Syria imefika mwisho?

Dar es Salaam. Swali ambalo wengi wanajiuliza ni kwamba kupinduliwa kwa Rais Bashar al-Assad nchini Syria itakuwa mwanzo wa maisha mapya ya amani kwa Wasyria baada ya mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yaliyodumu kwa miaka 13?

Mapigano nchini humo yalianza 2011 baada ya vuguvugu la kumng’oa Assad kushindikana hadi kufikia jana, Desemba 8, 2024, huku kwa kipindi chote hicho ikisababisha vifo vya watu zaidi ya nusu milioni, miji kuharibiwa na watu kukimbilia nchi za Jirani.

Sababu mojawapo iliyochangia mzozo huo kuanza ni idadi kubwa ya Wasyria waliokuwa wakilalamikia ukosefu wa ajira, rushwa na ukosefu wa uhuru wa kisiasa chini ya Rais Assad, ambaye alimrithi baba yake, Hafez baada ya kufariki dunia Juni 10, 2000.

Baada ya piga nikupige ya muda mrefu, jana Desemba 8, 2024 taarifa za utawala wa Rais Assad kuangushwa ziligonga vichwa vya habari duniani, baada ya waasi kuingia katika mji wa Damascus.

Taarifa zinasema Rais Assad na familia yake ambao wameitawala nchi hiyo kwa zaidi ya miaka 53 wamekimbilia Russia.

Picha za video zinazosambaa katika mitandao ya kijamii zinaonyesha mamia ya watu wakivunja sanamu na kuchoma moto picha za familia ya Assad ziliopo mjini Damascus. Assad amekuwa Rais wa Syria tangu mwaka 2000, akipokea kijiti hicho kutoka kwa baba yake.

Machi 2011, maandamano ya kuunga mkono demokrasia yalizuka katika mji wa kusini wa Deraa, yakichochewa na maasi katika nchi jirani dhidi ya watawala wakandamizaji.

Wakati Serikali ya Syria ilipotumia nguvu kubwa kudhibiti wapinzani, maandamano ya kumtaka Rais huyo ajiuzulu yalipamba moto nchi nzima.

Machafuko yakaenea na ukandamizaji ukazidi. Wafuasi wa upinzani walichukua silaha, kwanza kujilinda na baadaye kuondoa vikosi vya usalama katika maeneo yao, huku Assad akiapa kukabiliana vikali.

Ghasia ziliongezeka na nchi ikaingia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe. Mamia ya makundi ya waasi yaliibuka na haikuchukua muda mrefu kwa mzozo huo kuwa zaidi ya vita kati ya Wasyria kumtetea au kumpinga Assad.

Kwa mujibu wa makala ya BBC, ofisi ya haki za kibinadamu ya Umoja wa Mataifa mwaka jana ilikadiria kwamba raia 306,887 ambao ni sawa na asilimia 1.5 ya watu wote kabla ya vita waliuawa kati ya Machi 2011 na Machi 2021.

Kamishna wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu wakati huo, Michelle Bachelet, amesema vifo hivyo ni matokeo ya moja kwa moja ya operesheni za kivita na kueleza kuwa  haijumuishi raia wengi zaidi waliokufa kutokana na ukosefu wa huduma za afya, chakula, maji safi na haki nyingine muhimu za binadamu.

Shirika la Uangalizi wa Haki za Kibinadamu la Syria (SOHR), lenye makao yake makuu nchini Uingereza, ambalo lina mtandao wa vyanzo vya habari, lilinakili vifo vya watu 503,064 kufikia Machi 2023.

Shirika hilo lilikadiria kuwa idadi halisi ya waliofariki kutokana na vita hivyo ilikuwa zaidi ya 613,400, huku raia wengine 55,000 wakiaminika kufa kwa mateso katika magereza yanayosimamiwa na Serikali.

Hata hivyo, baada ya kumpindua Assad muungano wa waasi wa Syria umesema unaendelea na kazi ya kukabidhi madaraka kwa utawala wa mpito na kuupa mamlaka kamili.

Familia ya Assad ni kina nani

Familia ya Assad ambayo utawala wake wa miaka 53 umeangushwa, imeiongoza Syria baada ya baba yake Bashar aitwaye Hafez al-Assad kuchukua mamlaka mwaka 1970.

Alitawala hadi kifo chake mwaka 2000 na alirithiwa na mwanaye Bashar al-Assad. Al-Assads asili yao ni Qardaha, Latakia.  Jina la familia Assad lilianza mwaka wa 1927, wakati ilipobadilishwa jina lake la mwisho kuwa al-Assad, kwa kiarabu “Simba”.

Akizungumzia kudondoshwa kwa Assad, mchambuzi wa siasa za kimataifa, Ibrahim Rahbi amesema si kweli kuanguka kwa utawala wa Assad kutamaliza mizozo ndani ya nchi hiyo, bali itarajiwe migawanyiko zaidi.

“Kuanguka kwa utawala wa Assad ni hatua moja na mustakabali wa maisha ya Wasyria ni hatua nyingine, kinachofuata tutarajie mgawanyiko ndani ambao kwa sehemu kubwa unatokana na udini wa washiha kutawala zaidi ya miaka 50 na wasuni wanaona kama shida,” amesema.

Amesema si mwisho wa mapigano na machafuko nchini humo, ila kitakachotokea kwa sasa watatengeneza mazingira kuonekana kama Syria ya wote kabla ya mgawanyo kuanza.

“Serikali wameamua kuiacha kwa Waziri Mkuu kwa kuwa hawakuharibu vitu, ikiwemo ofisi za taasisi za serikali wameonyesha kwamba hawana kisasi kwa kumuacha Waziri Mkuu ila takwa lao ilikuwa kumng’oa Assad,” amesema Rahbi.

Amesema haijafahamika utawala ujao utakuwa wa aina gani, ingawa makundi mbalimbali yaliungana kufanya mapinduzi hayo.

“Kinachotokea kwa sasa ni matokeo ya Assad ndani ya Syria. Alikuwa akiungwa mkono nje, lakini ndani asilimia kubwa walikuwa wamemchoka na kwa sasa kwao ni kama ukombozi,” ameeleza Rahbi.

Kwa upande wake, Profesa wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Mohamed Bakari amesema kinachohitajika kwa sasa nchini Syria ni busara za viongozi wa makundi yaliyoungana kumng’oa Assad.

Kama si hivyo, amesema kunaweza kutokea mgawanyiko zaidi kwa kuwa Syria ya sasa imepasuka vipande vipande kwanza udini.

Amesema makundi ya ndani yanaungwa mkono na mataifa ya kiarabu na magharibi, huku Assad mwenyewe alikuwa akiungwa mkono na mataifa ya Iran na Russia hali iliyopelekea mgawanyiko.

“Atakayeingia anatakiwa ajue hatari iliyopo kwamba changamoto kubwa iliyopo mbeleni endapo kusipokuwa na mtengamano, kwani inahitajika hekima kubwa inayotokana na ushirikiano,” amesema.

Amesema na ushirikiano huo pia unagusa hata watu walikuwa wakihudumu katika Serikali ya Assad Ili waweze kuwa na utengamano ambao kwa kiasi kikubwa waliweka silaha chini wakiwemo majenerali.

Profesa Bakari amesema kutakuwa na mapigano yasiyokwisha kama wasipoleta utengamano wao kwa wao.

Related Posts