Timu nne za Bunge zaibuka kidedea katika michezo mitatu


Spika wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), Mheshimiwa Joseph Ntakirutimana akisalimiana na Mchezaji wa Timu ya Mpira wa Pete kutoka Bunge la Tanzania, Mheshimiwa Bupe Mwakang’ata wakati timu hiyo ikijiaanda kuingia uwanjani kuchuana na Timu ya EALA. Mchezo huo uliofanyika katika Uwanja wa Aghakani Jijini Mombasa, Kenya, ulimalizika kwa Timu ya Tanzania kuifunga Timu ya EALA mabao 50-2.

TIMU  nne za Bunge la Tanzania zimeshuka dimbani hii leo katika mashindano ya Michezo ya Mabunge ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuibuka kidedea katika michezo mitatu.

Timu zilizocheza leo katika mashindano haya yanayoendelea Jijini Mombasa nchini Kenya ni Timu ya Mpira wa Miguu, Timu ya Mpira wa Pete na Timu ya Mpira wa Kikapu wanawake na wanaume.

Mchezo wa mpira wa pete timu ya Bunge la Tanzania iliichakaza timu ya Bunge la Afrika Mashariki (EALA) kwa magoli 50-2.

Katika mchezo huo vinara wafungaji walikuwa Mheshimiwa Dkt. Christina Mzava, Mheshimiwa Esther Matiko na Mheshimiwa Ngwasi Kamani

Katika mpira wa kikapu Wanaume Timu ya Tanzania imejichukulia pointi za mezani baada ya wapinzani wao timu ya Bunge la Sudani ya Kusini kushindwa kufika uwanjani.

Kwa upande wa Mpira wa Miguu Timu ya Bunge la Tanzania ilitoka sare ya bao 1-1 na timu ya mpira wa Miguu ya Bunge la Burundi.

Goli la Timu ya Tanzania lilifungwa na Mheshimiwa Simai Hassan Sadiki katika kipindi cha kwanza cha machezo huo.

Kesho Timu za Tanzania zitakazoingia ulingoni ni Timu za Gofu, Timu ya Mpira wa Pete na Timu ya Kamba Wanaume na Wanawake

Related Posts