HAKUNA habari za ushiriki wa Simba wala Yanga kwenye michuano ya Mapinduzi Cup msimu huu na waandaaji wametoa sababu zao za msingi kuwa ni kutoa fursa ya kuziandaa timu za Taifa zitakazoshiriki CHAN mwakani pamoja na Afcon.
Makamu Mwenyekiti Kamati ya mashindano ya Kombe la Mapinduzi, Suleiman Jabir alisema mashindano hayo msimu huu 2025 yatajumuisha timu za taifa badala ya vilabu hii ni kufuatia Tanzania, Kenya na Uganda kuwa wenyeji wa mashindano ya Afcon na CHAN. ili kutoa fursa ya kupata mazoezi kwa timu za Taifa.
“Mashindano yanaanza Januari 3 na fainali kuchezwa 13 Januari kabla ya hapo kutakua na droo maalum yakupanga makundi ya mashindano ambayo yatafanyika katika uwanja wa Gombani Pemba baada ya uwanja wa Amaan kuwa katika maboresho,” alisema na kuongeza;
“Timu za taifa ambazo zitashiriki ni pamoja na Zanzibar Heroes, Kenya, Uganda, Kilimanjaro Stars, Burundi na Burkinafaso.”
Alisema timu zitakuwa kwenye makundi mawili kila kundi litakuwa na timu mbili kwenye hatua ya nusu fainali na baadae fainali.
Jabir alisema bingwa kwenye mashindano hayo ataondoka na kitita cha Sh. milion 100, maandalizi ya mashindano hayo yamekamilika.
“Pamoja na mashindano haya ya mpira wa miguu kwa timu za Taifa, kamati pia itaandaa sapraizi tofauti tofauti zitakazoongeza vionjo, ladha na furaha kwa watu wote. kutakua na zawadi mbalimbali na pia wachezaji mmoja mmoja katika vipengele tofauti tutakavyotangaziana baadae.”