Simba yakomaa na Kibu | Mwanaspoti

KWA hali ilivyo kuna uwezekano Kibu Denis akasalia Simba msimu ujao baada ya viongozi kufanikiwa kumshawishi yeye na wakala wake kwa asilimia kubwa.

Mwanaspoti ndilo lilikuwa la kwanza kukupa taarifa zote kuhusu Kibu kuanzia mazungumzo ya mkataba mpya ndani ya Simba baada ya ule wa awali kuwa mbioni kumalizika mwishoni mwa msimu huu.

Dili la kutakiwa na Yanga na Ihefu sambamba na mkwanja uliokuwa mezani kwa ‘Mkandaji’ kutoka kwa timu hizo tatu akiumiza kichwa achukue pesa ya nani na kuchagua msimu ujao acheze wapi.

Simba imefikia pazuri kumuongeza Kibu mkataba wa miaka miwili. Moja ya watu wa karibu na Kibu amelithibitishia Mwanaspoti kwamba staa huyo muda wowote kuanzia sasa huenda akakubali yaishe kwa kusaini mkataba wa Simba na kuzitupilia mbali ofa za Yanga na Ihefu ambazo zilikuwa zimesheheni mamilioni ya pesa na bonasi kedekede.

Katika ufuatiliaji wa karibu wa Mwanaspoti, wino atakaoumwaga Kibu ndani ya Simba huenda ukawa na thamani ya shilingi 300 milioni ambayo italipwa kwa awamu lakini pia mshahara wake utapanda hadi shilingi 12 milioni ambapo ukiweka na bonasi za mechi basi kwa mwezi atakuwa anakunja zaidi ya shilingi 15 milioni.

Mkataba huo kama ukifanikiwa utamfanya Kibu kuwa miongoni mwa mastaa wazawa wanaolipwa pesa nyingi ndani ya Simba akiingia anga za Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Aishi Manula, na John Bocco ambaye atastaafu rasmi mwishoni mwa msimu huu.

Alipotafutwa Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally alisema Simba kwa sasa inahakikisha inawabakisha wachezaji inaowahitaji na kumaliza ligi na baada ya hapo wataweka wazi mipango yote ya usajili.

“Kila mchezaji tunayemtaka Simba lazima abaki. Hakuna timu Tanzania inayoweza kuchukua mchezaji Simba kama tunamuhitaji. Niwahakikishie mashabiki wetu hakuna mchezaji tunamtaka Simba na tutashindwa kumuongezea mkataba, hilo wasiliwaze kabisa,” alisema Ahmed na kuongeza;

“Ligi ikimalizika tunaenda mapumziko kidogo kisha tunaanza kushusha mashine mpya kwaajili ya msimu ujao. Tutasajili wachezaji bora na imara. Simba itabadilika na kila mtu atamani kuwa Mwanasimba,” alisema.

Kibu aliyewahi kutamba na timu za Kumuyange FC ya Ngara, Kagera na Geita Gold, alitua Simba mwanzoni mwa msimu wa 2021/2022 akitokea Mbeya City ambapo katika msimu wake wa kwanza Msimbazi alifunga mabao manane na kutoa pasi za mwisho nne kwenye ligi, akiibuka mfungaji bora wa timu hiyo na msimu uliofuata 2022/2023 kwa maana ya msimu uliopita alicheka na nyavu mara mbili kwenye ligi na msimu huu amefunga bao moja hadi sasa katika ligi inayoelekea ukingoni.

Pamoja na kutokuwa na namba nzuri lakini Kibu amekuwa mchezaji tegemeo kwenye timu anazocheza tangu akiwa Kumuyange, Geita, Mbeya City, Simba na hata timu ya taifa ya Tanzania kwani amekuwa akitumiwa na makocha wote wanaofundisha katika timu hizo.

Kocha wa zamani wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ alisema Kibu ni mchezaji ambaye kila timu inahitaji kuwa naye kutokana na nguvu, nidhamu na uwezo wake wa kupambana.

“Kibu ni mchezaji atakayependwa na kila kocha. Anafanya kile unachomuelekeza lakini pia anauwezo wa kucheza kwenye zaidi ya maeneo matatu uwanjani na akakupa kitu kizuri kutokana na kasi, nguvu na ari yake ya kupambana zaidi,” alisema Robertinho.

Kiungo wa zamani wa Simba na Yanga, Haruna Moshi ‘Boban’ alisema Simba ingefanya makosa kumuacha Kibu kwani ni mchezaji mwenye ari ya kupambana lakini pia amekuwa akijitoa zaidi kwaajili ya timu.

“Kibu anauwezo mkubwa uwanjani. Anaweza kukaba na kushambulia pia ana nguvu na aina yake ya uchezaji ni wa kisasa ambao unatakiwa kwa sasa kwani ananyumbulika na kufanya majukumu mengi uwanjani hivyo Simba ihakikishe haondoki,” alisema Boban.

Awali baada ya kuona timu nyingi zinamtaka na mkataba wake unaelekea ukingoni, Kibu na uongozi wake chini ya meneja Carlos Sylvester waliweka dau la sh 400 kuwa pesa ya usajili mpya ya Kibu huku wakitaka timu itakayofika bei ilipe zote kwa mkupuo na mkataba uwe wa miaka miwili tu.

Simba, Yanga na Ihefu ziliingia katika meza ya majadiliano  ambapo Ihefu pekee ndiyo ilifika bei na kuzidisha sh 100 milioni ili iwe sh 500 milioni lakini impe mkataba wa miaka mitatu jambo ambalo upande wa Kibu haukuwa tayari.

Yanga na Simba zote ziliishia kwenye kutoa sh 300 milioni ambapo ilibaki kidogo Kibu aachane na Simba na kusaini Yanga baada ya Wananchi kuwa tayari kulipa hiyo pesa kwa mpigo lakini pia kumpatia gari kali la kutembelea na nyumba atakayoishi kwa miaka miwili atakapokuwa ndani ya timu hiyo tofauti na kwa Simba iliyopanga kumpa sh 300 milioni lakini nusu nusu (150 kwa mwaka).

Hata hivyo Simba baada ya kuona ‘maji yamezidi unga’ imemrudia Kibu na kumshawishi zaidi na kumuahidi maisha mazuri ndani ya Simba jambo lililompa utulivu na anafikiria kubadili maamuzi.

Simba pia imenasa saini ya beki wa Coastal Union Lameck Lawi anayemudu kucheza eneo la beki wa kati, pembeni na hata kiungo wa chini akiwa tegemeo kwenye kikosi cha Wagosi wa Kaya.

Related Posts