Simbu akwama Kawata Mlugu akishinda, Nyambui kesho

Wakati mwanariadha Alphonce Simbu akikwaa kisiki  kwenye uchaguzi wa Kamisheni ya Wachezaji (Kawat), Judoka Andrew Thomas Mlugu ametawazwa kuwa mwenyekiti mpya wa Kamisheni hiyo.

Mlugu amepata kura 38 za ndiyo, sita za hapana na kura tatu ziliharibika. Nafasi hiyo ilikuwa ikiwania pia na Simbu ambaye alienguliwa kwenye usaili saa chache kabla ya uchaguzi na muogeleaji Collins Saliboko aliyejitoa katikati ya mchakato.

Katika uchaguzi huo uliofanyika leo mjini Dodoma, mwanariadha, Andrew Rhobi aliibuka kinara kwa kupata kura 42 za ndiyo, 3 za hapana na kura mbili ziliharibika.

Mwanariadha mwingine, Failuna Abdi Matanga alipata kura 30 za ndiyo na kura 14 za hapana huku kura tatu zikiharibika. Failuna alikuwa akichuana kuwania ujumbe kwenye Kamisheni hiyo.

Wengine walioshinda ujumbe ni mwanariadha Josephat Gisemo aliyepata kura 29 na ndiyo na 15  za hapana huku tatu zikiharibika.

Walioshinda ujumbe kwa nafasi ya mwanamke na mwanaume kutokea Zanzibari ni Rauhiya Hassan Suluhu aliyepata kura 45 za ndiyo na mbili za hapana na Omary Bakar Omar aliyepata kura 35 za ndiyo na 12 za hapana.

Katika hatua nyingine, wagombea 11 kesho Jumanne watechuana kuwania uongozi wa Olimpians.

Wagombea hao ni Tasir Kitisa anayewania uenyekiti akiwa mgombea pekee kwenye nafasi hiyo inayoshikiliwa na Gidamis Shahanga anayemaliza muda wake.

Nguli wa riadha, Suleiman Nyambui ni mgombea pekee kwenye nafasi ya makamu mwenyekiti akitetea kiti chake. Kwenye ukatibu, bingwa wa zamani wa Afrika wa mbio za mita 800, Samwel Mwera anachuana na muogeleaji nguli,  Khalid Rushaka.

Katibu anayemaliza muda wake, Mwinga Mwanjala amesema wagombea wengine saba wanachuana kuwania nafasi tatu za ujumbe.

Wagombea hao ni Restituta Joseph, Mosi Ally, Failuna Matanga, Andrew Thomas Mlugu, Zakaria Barie, Samwel Kwang na Zakia Mrisho.

Wapiga kura kwenye uchaguzi huo ni wale wanamichezo wote waliowahi kushiriki michezo ya Olimpiki kuanzia 1964 Tanzania iliposhiriki kwa mara ya kwanza ikijulikana kama Tanganyika.

Related Posts