Akizungumza mjini Kyiv na Rais Volodymyr Zelensky, Merz anayeunga mkono kuipa Ukraine makombora ya masafa marefu ya Taurus , amesema anataka jeshi la Ukraine liwe na uwezo wa kushambulia kambi za jeshi zilizoko ndani ya Urusi. Amesema hawalengi kuwashambulia wananchi, wala miundo mbinu ya kiraia bali kambi zinazotumiwa na Urusi kuishambulia Ukraine.
Kansela Scholz tofauti na Merz amekuwa akikataa ombi la Zelensky la kuipa nchi yake makombora ya Taurus, akisema yatachochea zaidi mzozo wa Ukraine na kuitumbukiza Ujerumani moja kwa moja kwenye mzozo huo.
Soma zaidi: Merz awasili Ukraine kwa mazungumzo
Kwa upande wake Zelensky amesisitiza umuhimu wa Ulaya kuwa na dhamira ya dhati ya kuihakikishia usalama nchi yake katika mazungumzo yoyote ya usuluhishi yanayolenga kusitisha uvamizi wa Urusi.
Katika hatua nyingine, Baraza la Umoja wa Ulaya limesema kuwa litaipa Ukraine dola za kimarekani bilioni 4.4. Uamuzi huo umefikiwa baada ya mataifa wanachama kuidhinisha mpango wa kuipa fedha hizo.
Msaada wa Umoja wa Ulaya umetangazwa wakati waziri wa ulinzi wa Ukraine Rustem Umerov akisema leo kuwa amefanya mazungumzo na mwenzake wa Marekani Lloyd Austin kuhusu mkutano ujao wa Ramstein kuhusu Ukraine unaohusisha mataifa wanachama wa NATO, Umoja wa Ulaya na nchi nyingine zinazoiunga mkono Ukraine dhidi ya uvamizi wa Urusi.
Shambulio la bomu lililotegwa kwenye gari laua mtu mmoja Donesk
Tukisalia katika mzozo huo, bomu lililokuwa limetegwa ndani ya gari katika mji wa Donesk unaodhibitiwa na Urusi limemuuwa mtu mmoja, na mwingine amejeruhiwa.
Taarifa ambazo hazijathibitishwa kutoka Urusi zinadai kuwa mtu aliyeuwawa kwenye shambulio hilo ni mkurugenzi wa zamani wa gereza la Olenivka Sergei Yevsyukov, na aliyejeruhiwa anatajwa kuwa ni mke wake.
Mnamo Julai 2022, zaidi ya wafungwa 50 wa Ukraine waliuwawa katika gereza hilo na Ukraine iliituhumu Urusi kwa kuwauwa wafungwa kwa makusudi wakati Moscow ilidai kwamba Ukraine ndiyo iliyofanya mauaji hayo kwa shambulio la roketi.