SMZ yajipanga uzalishaji mpunga, mbogamboga

Unguja. Wakati Serikali ikiongeza eneo la kilimo cha umwagiliaji kutoka hekta 875 mwaka 2019 hadi kufikia hekta 2,300 mwaka 2024, imewataka wananchi kuachana na kilimo cha mazoea ili kufikia malengo ya kujitosheleza kwa ajili ya chakula na biashara.

Akizungumza wakati kuzindua maboresho ya miundombinu ya umwagiliaji, Desemba 8, 2024 kwenye mabonde manne yaliyofanyiwa uboreshaji, Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Zanzibar Shamata Shaame Khamis amesema nia ya Serikali ni kuinua wakulima wake, kuongeza chakula na kukuza pato la taifa. 

 “Haya mabonde kuna mashirika yamekuja yakitaka kuyachukua, lakini Serikali imesema inawapa wananchi wake, kwa hiyo imeboresha miundombinu ili kuwe na uzalishaji wa kutosha kwa misimu miwili,” amesema.

Miundombinu hiyo ya umwagiliaji imefanikiwa kupitia mradi wa Feed The Future kupitia Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (Usaid), na Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Korea Kusini (Koica).

Mabonde manne yanatumiwa na wakulima 5,710 ambapo yanatakiwa kutumika kwa misimu miwili na kuzalisha tani 11 za mpunga kwa ekari moja.

Mabonde hayo na wakulima wake kwenye mabano ni Cheju (2,500), Kibokwa (1,235), Kinyasini 1,600 na Mlemele 375 ambao wamepatiwa konde kwa kuendeleza kilimo cha mpunga.

Pamoja na miundombinu duni na teknolojia ya kisasa, mabadiliko ya hali ya hewa yameathiri uzalishaji wa mazao hayo lakini kupitia ushirikiano wa mataifa hayo wameshudia mabadiliko makubwa ya uzalishaji.

 “Yule ambaye ataona uwezo wake ni mdogo hataweza kulima kwa misimu miwili, atupishe kwahiyo tusingependa kabisa fursa hizi na jitihada hizi zinakwenda kuchezewa, fedha nyingi zimetumika na tuna nia njema tuungane kuzalisha ili tuwape moyo viongozi wetu kwa maendeleo yetu,” amesema.

Kwa mujibu wa Shamata, wanataka mabonde hayo yatumike kwa misimu miwili katika mazao mawili tofauti; “wakimaliza kulima mpunga waingie kwenye kilimo cha mbogamboga ambacho nacho kina mwmko mkubwa Zanzibar.

Katibu Mkuu wizara hiyo, Khamis ali amesema kwa wakulima ambao wameanza kutumia miundombinu hiyo, uzalishai wake umeongezeka kutoka tani 1.5 hadi tani 5.5 kwa msimu mmoja.

“Hivyo misimu miwili mkulima anazalisha tani 11, na huu ni mpango wa Serikali kuondokana na kilimo cha mazoea,” amesema.

Balozi wa Korea ya Kusini nchini Tanzania Eunju Ahn amesema mradi huo umeanzishwa mwaka 2019 na kwamba wataendelea kushirikiana na Zanzibar kuhakikisha mradi huo unakuwa endelevu na kuleta tija kwa taifa na wananchi.

Naye Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Michael Battle, amesema kwa pamoja wamepanua mpango huo ili kuleta manufaa ya mwaka mzima kwa wanajamii wa eneo hilo.

“Skimu hii ya umwagiliaji iliyoimarishwa sasa inashughulikia kikamilifu Unguja na Pemba, ushirikiano huu wa kimataifa umewawezesha maelfu ya Watanzania kuongeza tija katika kilimo na kuongeza pato la ndani kwa kiasi kikubwa,” amesema.

Amesema wanajivunia kuongeza athari za mpango huo wa umwagiliaji na kuugeuza kuwa operesheni ya mwaka mzima, wakiongeza ubora wa mavuno ya mpunga katika msimu mkuu wa kilimo na kupanua fursa za kilimo cha bustani wakati wa msimu usio na msimu na kuongeza matumizi ya mfumo wa umwagiliaji kwa mwaka mzima.

 Pili Kashinje, mkulima wa mboga mboga na matunda amesema wakati anaanza kuhamsiaka na kilimo,  aliona kama kazi kubwa lakini baada ya kuzoea anajivunia kuanza kupata masoko ndani na nje ya nchi.

“Mwanzoni ilikuwa changamoto kwani ilionekana siwezi lakini nimejiamini katika kilimo na sasa ninasambaza mbogamboga na matunda katika hoteli,” amesema.

Mkulima mwingine Ussi Makame, amesema: “Kwasasa najishughulisha na kilimo hiki hivyo watu wahamasike kulima kwa sababu ni kazi nzuri na kinalipa iwapo mtu atafuata maelekezo na miongozo yote.

Related Posts