Haya ndio maisha ya ombaomba kwenye majiji, Serikali yataja mkakati

Dar/Mikoani. Watu wenye uhitaji maalumu wameeleza magumu wanayopitia kuendesha maisha yao na kugeuka kuwa ombaomba katika maeneo ya miji na majiji nchini, huku Serikali ikitoa mwelekeo na msimamo juu ya kundi hilo.

Huenda si jambo jipya unapokuwa katika majiji ya Dar es Salaam, Mwanza, Dodoma, Arusha na au Mbeya, ukakutana na watu mbalimbali wakiwa katika maeneo tofauti wakiomba misaada.

Baadhi yao ni watu wenye ulemavu wa viungo ama miguu, mikono, wasioona, wagonjwa, wazee, masikini na vikongwe kila mmoja akitumia njia zake kutafuta chochote ili kuendesha maisha.

Wapo wanaotumia viti mwendo, wanaotembea na watoto mgongoni wakiwa wamekaa au kutembea ofisini, vituo vya mabasi na sehemu zenye watu wengi na wengine kutumia watoto wao kuomba misaada.

Hata hivyo, pamoja maisha hayo, yapo magumu wanayopitia watu hao, muda mwingine kunyanyapaliwa, dharau, kejeli, imani potofu, dhihaka na kutengwa na baadhi ya watu.

Pia wapo baadhi ya watu hutumia makundi hayo kwa kuwafanya vitegauchumi wakiwapanga barabarani au kupita ofisini na madukani kueleza shida zao kuomba fedha.

Frida John mkazi wa Shinyanga, ambaye ni mlemavu wa miguu amedai kuletwa Arusha kwa ajili ya kufanya kazi ya kushona viatu vya asili kwa makubaliano ya kulipwa mshahara wa Sh150,000 kwa mwezi, lakini hali imekuwa tofauti na kugeuzwa ombaomba jijini humo.

“Mwaka juzi nilikutana na mwenzangu mlemavu, ambao tunaishi wote nyumba moja (Makao Mapya), ambapo nimejikuta kuwa ombamba na mahesabu nampa mwenye nyumba,” amesema.

“Nilikuja kwa ajili ya kazi ila nilichokutana nacho ni tofauti, nimekuja kwa niliyekuwa nawasiliana naye, akaniambia kazi tofauti muda wote nipo hapa mataa kwa kuwa napata mahitaji yote kwa mwenye nyumba” anasema Frida.

Naye Neema Philipo ambaye ni mkazi wa Simiyu, anayeishi eneo la Unga Limited, amesema aliletwa jijini Arusha kwa ajili ya kufanya kazi za ndani ila amejikuta akifanya kazi ya kusukuma kiti cha mlemavu na yule mlemavu akiwa anaomba.

“Niliahidiwa kuja kufanya kazi za ndani ila nilivyokuja sijapelekwa nilikoahidiwa, kwa sasa tunaishi kwenye nyumba moja kule Unga Limited na baada ya kazi usiku tunaulizwa makusanyo,” amesema.

“Nina miezi saba tangu nije Arusha na tukishamaliza kuomba jioni tunarudi nyumbani na kugawana kiasi kilichopatikana na yule aliyetupa hifadhi kwa siku tunaweza kupata Sh15,000 hadi Sh20,000 na tunamgawia bosi wetu,” anasema Neema.

Christina Christopher, mwenye watoto sita mkazi wa Mbalizi, Mbeya amesema anapitia magumu kwakuwa hata mume wake naye ana changamoto ya kutoona, hali inayowapa ugumu kufanya shughuli za kuwaingizia kipato.

Mmoja ya ombaomba katika Mtaa wa Makoroboi nje ya msikiti wa Hinduism jijini Mwanza akiwa amekaa chini akiendelea kuomba msaada kwa wapita njia. Picha na Anania Kajuni

Amesema miaka minne nyuma alipata msamaria mwema aliyempa mtaji mdogo ambapo alifanikiwa kujenga boma lakini alikosa fedha za kuezeka.

“Ninaishi Mbalizi nina watoto sita, sina kazi yoyote na maisha yangu nategemea misaada hapa hapa Kabwe, nyumba yangu niliyojenga nilikosa fedha za mabati”

“Mume wangu naye ana tatizo kama hili hili langu, tunaishi maisha magumu ninaomba Serikali inilee na familia yangu,” amesema Christina.

Ameongeza hakuzaliwa na tatizo hilo kwani ilimkuta akiwa na miaka saba ambapo licha ya juhudi za kujipambania,  haikuwezekana na kuwa anaishi kwa matumaini.

“Huwa naomba msaada kupandishwa kwenye gari na mtoto wangu ananiongoza siwezi kupotea, huwa kila siku natoka Mbalizi kuja hapa Kabwe” amesema.

Naye Said John mwenye ulemavu wa miguu amesema maisha yake ni kutegemea misaada ya wasamaria wema wanaopita barabarani, licha ya kwamba wapo wanaomdharau na kumnyanyapaa.

“Suala la mkopo sijawahi kufuatilia na sijajua utaratibu ukoje, lakini hitaji langu ni Sh 3 milioni, ambazo zinaweza kunisaidia kuendesha maisha na kuondokana na ombaomba,” anasema John.

Kwa upande wake, Abdallah mkazi wa jijini Mwanza mwenye ulemavu wa miguu, amesema baada ya kupata ugonjwa wa ukoma mwaka 1969,  aliuza mali zake zote kwa ajili ya matibabu na kujikuta akibaki masikini hadi kutengwa na ndugu

“Nilizunguka sana kutafuta tiba ambapo fedha nyingi zilitumika hali iliyopelekea kuuza mali na sina wa kunisaidia nikaamua kuwa ombaomba ili kupata chochote,” anasema na kuongeza:

“Serikali haitusaidii chochote zaidi ya kutafuta namna ya kutufukuza mitaani sijui tukale wapi, mfano kulikuwa na kambi ya wazee eneo la Bukumbi Misungwi hata mimi nimewahi kuishi pale lakini imesambaratishwa,” anasema Abdalah.

Daudi Yohana mkazi wa Ilemela Mwanza, mwenye ulemavu wa macho, amesema kutokana na tatizo hilo,  ameshindwa kufanya shughuli yoyote hivyo kuamua kuwa ombaomba kuendesha maisha.

“Nikiwa mtoto niliugua ugonjwa wa surua ambao ulisababisha nisione kwahiyo tangu nimekuwa mtu mzima nikaona njia pekee ya kuendesha maisha ni kuombaomba,” anasema Yohana.

Bertha Mdachi mkazi wa Nzuguni jijini Dodoma amesema analazimika kuja mjini kuomba, kwa sababu kwa umri alionao na ulemavu wa macho, hawezi kufanya kazi yoyote ya kumwingizia kipato.

Amesema alipata upofu miaka 17 iliyopita baada ya kuumwa macho na tangu hapo alikuwa anashinda nyumbani bila kufanya kazi yoyote hivyo alikuwa na hali ngumu ya maisha.

“Niliamua kuja kuomba mjini kwa msaada wa wajukuu zangu ambao huwa wananiongoza njia kwa watu ambao huwa wananipa msaada, siwezi kuajiriwa popote umri wangu umeenda na sina macho,” amesema Bertha.

Mariam Abdalla ambaye ni mwenyeji wa Mkoa wa Shinyanga amesema amekuja jijini Dodoma kufanya kazi ya kuomba ili aweze kuwasomesha watoto wake ambao bado ni wadogo.

Mariamu amesema kuwa aliletwa jijini hapa na msamaria mwema ili afanye kazi hiyo na kuitunza familia yake kwakuwa hawezi kufanya kazi nyingine kutokana na ulemavu wa miguu.

“Kuna msamaria mwema ambaye huwa ananileta mjini kwenye kiti mwendo na kuniacha hapa niendelee kuomba na inapofika jioni ananirudisha nyumbani na ndio msaada wangu wa kuishi” anasema Mariam.

Pamoja na kukiri uwapo wa ombaomba katika majiji hayo, viongozi wa halmashauri  katika mikoa hiyo, wameeleza mkakati, mwelekeo na msimamo wao katika kukabiliana na kundi hilo.

Christina Christopher mwenye ulemavu wa macho akiwa na familia yake mtaa wa Kabwe Mbeya.

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Jabir Shekimweri amesema kuna watu wanapitia changamoto mbalimbali kwenye maisha na ndiyo maana wanajikuta mitaani wakiomba kwa watu ili waweze kutimiza mahitaji yao ya kila siku.

“Hii mitihani ikiwa haijakukuta huwezi kujua wanayoyapitia watu ambao wanaomba mitaani hasa ukiwa umevaa tai au ukiwa ofisini kwenye kiti cha kuzunguka ni lazima hutaelewa”

“Lakini ukivaa viatu vyao ndipo utajua kuwa kuna watu wana changamoto kubwa sana wanazokabiliana nazo kwenye maisha, wapo wanaopiga simu kuomba, wengine kulazimisha,” amesema Shekimweri.

Hata hivyo, amesema kwa sasa hana takwimu sahihi za idadi ya watu wanaoomba jijini Dodoma kwani kwa sasa Dodoma limekuwa ni jiji na makao makuu ya nchi hivyo kila mtu anakimbilia fursa.

Amesema kwa sasa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya haitoi kibali cha watu kuomba fedha za matibabu kwa mtu yeyote kutokana na malalamiko mengi kutoka kwa watu kusumbuliwa kwenye ofisi zao na maeneo ya starehe.

“Hii nimeipiga marufuku kwa sasa kinachoombewa kibali ni wafadhili ambao wanahitaji kumsaidia mtu mwenye uhitaji hivyo wanapewa utambulisho kutoka kwa Mkuu wa Wilaya” amesema Shekimweri

Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba ametaja sababu ya ombaomba kuwepo mtaani kuwa ni  jamii kuacha kusaidia watu wenye mahitaji maalumu.

“Suala la kuwasaidia wazee ni suala la jamii sio la Serikali, hilo ndilo jukumu la jamii sasa kwa sababu imebadilika haisaidii watu wanaowazunguka hayo ndio madhara yake,”

“Mwaka 2020 tuliwakamata na kuwaondoa wote na kuwapeleka majumbani kwao kwa magari na ndugu zao walikuwa wanawapokea, sasa waulize nauli ya kuwaleta tena mjini waliipata wapi” amesema Kibamba.

Hata hivyo, Kibamba amesema wanaendelea na oparesheni za kuwaondoa ombaomba mitaani ikiwemo watoto ambapo hata hivyo wanakabiliwa ugumu kwani wengi hawataki kuondoka.

“Kuna oparesheni za kuwaondoa mjini zinaendelea kwa mfano hawa watoto wa mitaani kuna kituo Ilemela tunawapeleka na kuwasomesha lakini hawataki kusoma ila wanataka kuomba fedha,” amesema.

Ofisa Ustawi wa Jamii Jiji la Mbeya, Eva John amesema hatua ya kuwaondoa ombaomba hao ni ngumu kwa sasa kutokana na jambo hilo kuanzia kwenye jamii.

Amesema iwapo watafikia uamuzi huo lazima kuishirikisha jamii kwani wengine wanawatumia kwa mambo ya kiimani hivyo ili kutoleta mgogoro ni kuwashirikisha wananchi.

Amefafanua halmashauri inayo programu ya mikopo kwa makundi ya walemavu, vijana na wanawake hivyo kundi hilo maalumu halina masharti mengi.

“Zaidi tunachoweza kusaidia ni ile asilimia mbili ambazo hazihitaji wawe katika kundi, hata mtu mmoja au wawili wanaweza kupewa kwa ajili ya kuendesha maisha”

“Mkakati wetu lazima tushirikishe jamii kwakuwa kuna baadhi hutoa misaada yao kwa ajili ya ibada, hatuwezi kuwakurupusha haraka” amesema Eva.

Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii Halmashauri ya Jiji la Arusha, Isaya Doita, amekiri kuwepo kwa kundi hilo akieleza mapendekezo yao ni kutoa mkopo wa asilimia 10 za halmashauri.

 “Tulishajadili suala hilo na kupeleka kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ili wasimamie watu hao wasiende kuomba barabarani kwani ni hatari kwa usalama wao, ila utekelezaji umekuwa mdogo,” amesema.

“Ukiangalia kwenye taa za kuongozea magari, askari wa usalama barabarani wapo na wanaona hao ombaomba ila hawachukui hatua, kila mmoja akitimiza wajibu tutaondokana nalo,” anasema Mwenyekiti huyo.

Kamishna Msaidizi wa Ustawi wa Jamii, Tullo Masanja amesema kwanza Serikali haikubaliani na watu kuomba mitaani kwakuwa inao uwezo wa kuwasaidia kwa kuwalea.

Amesema Wizara ya Ustawi wa Jamii haitaki mtu aombe ndio maana kuna vituo vya kulelea watoto wasio na makwao pamoja na wazee wasiojiweza.

“Kuna kundi la ombaomba kama wazee au wale wenye ulemavu tuna vituo kuwahudumia wale wasiio na msaada kwa kuwapa chakula mavazi na makazi,” amesema Masanja.

“Kama Serikali huwa tuna mikakati kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais- Tamisemi, kuna wakati tunafanya operesheni kuwakamata na kuwaondoa kupitia msako na tunawapeleka  makwao na kwa wale wasio na familia tunawalea,”amesema.

Amesema changamoto moja wapo kwenye familia wengine hawakubaliki, hivyo wanaona suluhisho ni kuomba.

Amesema wengine wanaiga kutokana na mtindo wa maisha ya kwao kukosa uhuru wanaamua kuanza kuomba.

“Kwa wazee nao familia ikimtenga anakosa mahitaji analazimika kwenda kuomba. Wengine wanaomba kama biashara ila kwa wahitaji wanahangaika hadi pale jamii inapowatambua,” amesema.

Akitaja vituo vya kulelea ombaomba amesema vipo zaidi ya 437 vya watoto yatima huku vya Serikali vipo viwili ambapo watoto kuna watoto zaidi ya 350 na vya wazee vipo 13 huku vituo binafsi vya wazee vikiwa zaidi ya 16.

“Kwa takwimu za hivi karibuni kuna wazee zaiid ya 700 wanaohudumiwa. Tunawakumbusha Tamisemi kunapokuwa na ombaomba wengi watolewe kwakuwa wanaweza kuhudumiwa na Serikali.

Kila mkoa tunawakumbusha kufanya operesehni kuwaondoa watoto na wazee.” Amesema.Amesema nia ya Serikali ni kutokuwa na ombaomba kwakuwa ina uwezo wa kuwahudumia wakaondoka mitaani.

Imeandikwa na Saddam Sadick (Mbeya), Rachel Chibwete (Dodoma), Anania Kajuni (Mwanza) na Janeth Mushi (Arusha)

Related Posts