Makada 21 wajitosa kinyang’anyiro uongozi kanda ya kati Chadema

Dodoma. Dirisha la uchukuaji na urejeshaji fomu kuwania uongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Kati limefungwa, huku wanachama 21 wakijitosa kuwania nafasi mbalimbali kati yao watano wakiwania uenyekiti.

Miongoni mwa nafasi zinazowaniwa ni mwenyekiti, makamu mwenyekiti na mweka hazina, uwakilishi katika baraza la wanawake (Bawacha), baraza la wazee (Bazecha) na vijana (Bavicha). Dirisha hilo lilifunguliwa Desemba 3 na limefungwa leo Jumatatu, Desemba 9, 2024 saa 10:00 jioni.

Makada hao 21 baada ya kurejesha fomu, watasubiri kuitishwa kwa kikao cha kamati kuu kwa ajili ya usaili, kisha tarehe ya kufanyika kwa uchaguzi itatangazwa na kikao hicho. Kanda hiyo ni miongoni mwa kanda mbili na ya Kaskazini zilizokuwa hazijafanya uchaguzi.

Katibu msataafu  wa Chadema kanda ya kati, Iddi Kizota baada ya kurudisha fomu ya kugombea uenyekiti wa chama hicho kanda ya kati. Picha na Sharon Sauwa.

Kukamilika kwa uchaguzi wa kanda zote 10 za Chadema, kunatoa fursa kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa chama hicho unaotarajiwa kufanyika mapema mwakani. Miongoni mwa nafasi zinazowaniwa kwenye uchaguzi huo ni unyekiti, makamu mwenyekiti na wajumbe wa kamati kuu.

Baada ya dirisha kufungwa kwenye kanda hiyo ya kati yenye mikoa ya Morogoro, Singida na Dodoma, Ofisa uhusiano wa chama hicho kanda ya kati, Juma Omary amesema: “Kilichobaki hivi sasa ni kamati kuu, sisi shughuli imeishia hapa kwa sababu jukumu tulilokuwa tumepewa kugawa na kupokea fomu na mwisho ni leo.”

Amewataja waliochukua fomu kwa nafasi ya uenyekiti ni watano ambao ni Devota Minja, David Jumbe, Shujaa Evarest, Iddi Kizota, Ezeckiel Chisinjila na kwa upande wa makamu wenyeviti yuko Jackson Jingu, Charles Manyanya, Daniel Butale na Imelida Maleyi.

Nafasi uenyekiti wa kanda ya kati ipo wazi baada ya aliyekuwa akishikilia Lazaro Nyalandu kurejea Chama cha Mapinduzi CCM) Aprili 30, 2021.

Nyalandu aliyewahi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, alitangaza uamuzi huo mbele ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan katika mkutano mkuu wa chama hicho uliofanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.

Nyalandu alijitoa CCM Oktoba 30, 2017 na baadaye kujiunga na Chadema ambako alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa chama hicho kanda ya kati.

Nafasi ya makamu mwenyekiti ilikuwa ikishikiliwa na Asha Luja ambaye kwa taarifa za chama hicho amehamia nje ya nchi.

Related Posts