Majadiliano ya kukabidhiana madaraka yaanza Syria – DW – 10.12.2024

Wakati jumuiya ya kimataifa ikitoa wito wa kufanyika makabidhiano ya madaraka kwa njia ya amani, Qatar imetangaza kuwa wanadiplomasia wake walifanya mazungumzo na  kundi kuu la waasi nchini Syria la Hayat Tahrir al-Sham (HTS) , wakati mataifa kadhaa ya kanda hiyo yakijaribu kuanzisha mawasiliano na kundi hilo ambalo limefanikiwa kuuangusha utawala wa Bashar al-Assad.

Kwa upande wake, Marekani imesema bado inalichukulia kundi hilo kama la kigaidi lakini hilo halitowazuia kufanya nao mazungumzo ikiwa itahitajika. Pia, waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken ametahadharisha kuwa kundi la kigaidi linalojiita Dola la Kiislamu linaweza kutumia hali hii ya kuanguka kwa utawala wa Assad na sintofahamu ya uongozi ili kujizatiti tena nchini Syria, lakini akasisitiza kuwa Washington itafanya kila liwezekanalo kulizua hilo kufanyika.

Assad akimbia nchi, waasi waukamata Damascus

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Hata hivyo Waziri mkuu wa serikali iliyoangushwa ya Assad, Mohammed Jalali, amesema wameanza majadiliano ya kukabidhi madaraka kwa kundi la waasi hao lakini akasisitiza kuwa hilo linaweza kuchukua siku kadhaa ili kukamilika.

Katika hatua nyingine, mataifa ya Uingereza, Ujerumani, Ufaransa, Italia na nchi nyingine kadhaa za Ulaya zimesema katika kusubiria kujua mustakabali wa taifa hilo, zitasitisha maombi yote ya Wasyria walioomba hifadhi huku Austria ikisema itawarejesha hivi karibuni wakimbizi nchini Syria.

Furaha ya Wasyria na hofu ya Israel

Mamilioni ya Wasyria wameendelea kusherehekea kitendo cha kuangushwa utawala wa rais Bashar Assad huku maelfu ya wengine wakiendelea kuingia nchini humo kwa matarajio ya kuwa na taifa huru lenye amani na usalama licha ya kuwa safari bado ni ndefu.

Viongozi wa Israel wakilitembelea eneo la milima ya Golan mpakani na Syria
Viongozi wa Israel wakilitembelea eneo la milima ya Golan mpakani na SyriaPicha: Kobi Gideon/Israel Gpo via ZUMA Press Wire/picture alliance

Lakini kuangushwa kwa utawala wa Assad kumezidisha pia  hali ya wasiwasi kwa majirani wa Syria hasa Israel ambayo inahofia kuwa machafuko hayo yanaweza kuenea hadi katika eneo lake na ndio maana imefanya mashambulizi makubwa ndani ya Syria na kulenga maeneo zaidi ya 100.

Israel pia inautazama mwisho wa utawala wa Assad kama fursa ya kusambaratisha uwezo wa Iran wa kusafirisha silaha kupitia Syria kwenda nchini Lebanon ili kulisaidia kundi la Hezbollah.

Jeshi la Israel lilianza kuchukua udhibiti wa eneo la Syria lililoundwa mwaka 1974 kama sehemu huru ili kusitisha mapigano kati ya nchi hizo. Israel imedai hatua hiyo ni ya muda na yenye lengo la kuulinda mpaka wake.

Lakini uvamizi huo umezusha hisia huku wakosoaji wakiishutumu Israel kwa kukiuka makubaliano na kutumia machafuko nchini Syria ili kujinyakulia  maeneo zaidi.

Soma pia: Netanyahu: Hatua za Israel Mashariki ya Kati zimesaidia anguko la Assad Syria

Marekani imeitaka Israel kuchukua hatua hiyo kwa muda tu huku Saudi Arabia ikisema kwamba vitendo hivyo vinadhihirisha ni ya Israel ya kuvuruga fursa ya Syria kurejesha hali ya usalama. Ikumbukwe kuwa Israel bado inadhibiti sehemu ya Syria ya Milima ya Golan, hatua ambayo haitambuliwi na jumuiya ya kimataifa lakini Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema eneo hilo linalokaliwa na Israel kwa karibu miaka 60, litasalia daima kuwa chini ya udhibiti wake.

(Vyanzo: AP, DPA, Reuters, AFP)

 

Related Posts