Coastal yaachana na Ley Matampi

UONGOZI wa Coastal Union, umetangaza kuachana na kipa wake, Ley Matampi baada ya kufikia makubaliano ya pande mbili kuvunja mkataba huku mwenyewe akisema kwamba ni uamuzi sahihi.

Matampi ambaye alibeba Tuzo ya Kipa Bora wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita 2023-2024, alijiunga na timu hiyo Agosti 2023 akitokea Jeunesse Sportive Groupe Bazano ya nchini kwao DR Congo huku mkataba wake ukitarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu.

Taarifa ya Coastal Union iliyotolewa mapema leo Jumanne Desemba 10, 2024, imeeleza hivi: “Tumefikia makubaliano baina ya klabu yetu na kipa Ley Matampi ya kumaliza huduma za pande zote mbili.

“Uzoefu wako umechangia kwa asilimia kubwa mafanikio yetu ya msimu uliopita. Shukrani za kipekee kwa kocha wa magolikipa Mansour Ally ambaye alitumia nguvu kubwa ya kurudisha uwezo na kiwango chako ukawa msaada mkubwa eneo la kulinda lango letu”.

“Tunakutakia kheri nyingi na mafanikio zaidi katika maisha yako.”

Akizungumzia hilo, Matampi ambaye msimu uliopita alichangia kwa kiasi kikubwa Coastal Union kumaliza nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu Bara na kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu, amesema huo ni uamuzi mzuri kwake.

“Nilipewa barua Wiki iliyopita na kwangu naona ni uamuzi mzuri tu ambao klabu imefikia,” amesema kipa huyo aliyemaliza ligi msimu uliopita na clean sheet 15 akiwa kinara.

Related Posts