Ulimwengu unaadhimisha siku ya kimataifa ya Haki za Binadamu, huku ofisi ya haki za binadamu ya umoja wa Mataifa ikieleza kuguswa na kuendelea kuongezeka kwa vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu kwenye mataifa mengi. Huko nchini Sudan, kwa mfano, shirika la Human Rights Watch limesema kwamba vikosi vya wapiganaji wa RSF vimewauwa raia kadhaa, kuwajeruhi, kuwabaka na kuwateka nyara wengine.
Mashambulizi hayo yamefanywa toka Desemba 2023 hadi Machi mwaka huu kwenye miji ya Habila na Fayu kwenye jimbo la Kordofan Kusini.
Uhalifu wa kivita
Ripoti ya shirika la Human Rights Watch iliotolewa leo imesema mashambulizi hayo yaliwalenga hasa watu wa kabila la Nubana kwamba hayajaripotiwa sana. Kwa mujibu wa shirika hilo mauwaji hayo ni uhalifu wa kivita.
Jean-Baptiste Gallopin, mtafiti mkuu wa migogo katika shirika la Human Rights Watch amesema kuwa unyanyasaji wa vikosi vya wapiganaji wa kundi la RSF dhidi ya raia huko Kordofan Kusini ni ishara ya kuendelea kwa ukatili kote nchini Sudan. Gallopin amesema matokeo haya mapya yanasisitiza haja ya dharura ya kutumwa kwa ujumbe wa kikosi cha kulinda raia nchini Sudan.
“Tunahitaji kuzuia utiririshaji wa silaha Sudan”
Kwenye mkutano na waandishi habari mjini Geneva, Mkuu wa Tume ya Haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, Volker Turk alitoa mwito wa kusitishwa ununuzi wa silaha katika maeneo ya migogoro duniani ikiwemo Sudan.
“Tunahitaji kuzuia utiririshaji wa silaha katika Haiti, Sudan na Myanmar; kuwajulisha wale wanaotoa silaha, ikiwa ni pamoja na Israel na wahusika wasio wa Kiserikali wenye silaha huko Lebanon, Syria, eneo la Palestina linalokaliwa kwa mabavu, kwamba sheria ya kimataifa inazitaka Mataifa kuchukua tahadhari kwamba silaha wanazotoa hazitumiwi kufanya ukiukaji wa haki za binadamu.”, alisema Turk.
Wito wakupelekwa wanajeshi wa kulinda amani Sudan
Shirika la Human Rights Watch liliorodesha mauaji ya watu 56 wasio na silaha katika mashambulizi kwenye miji miwili ya jimbo la Kordofan Kusini, wakiwemo wanawake 11 na mtoto 1. Ushuhuda umeonyesha kuwa wapiganaji wa kundi la RSF waliwauwa watu hao kwa mtindo wa kunyongwa majumbani au kwa kuwapiga risasi mitaani. Pia wanawake na wasichana 79 walibakwa katika kipindi hicho.
Takwimu halisi zinaweza kuwa kubwa zaidi limesema shirika hilo la Haki za Bindamu.
Shirika la Human Rights watch limeseikitishwa kuona kwamba Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika bado chukua hatua madhubuti ya kuwalinda raia wa Sudan.
Tangu kuanza kwa machafuko ya Sudan, maelfu ya watu wameuawa huku raia milioni 11 wakipoteza makaazi yao na kusababisha moja ya mgogoro mbaya zaidi wa kibinaadamu kuwahi kushuhudiwa duniani. Hiyo ni kulingana na Umoja wa Mataifa.