Dar es Salaam. Wabunge watatu majeruhi wa ajali ya basi la Kampuni ya Shabiby waliokuwa wamelazwa katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, wamehamishiwa katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili-MOI kwa matibabu zaidi.
Desemba 6 mwaka huu, wabunge 16, maofisa wawili wa Bunge na dereva wa basi hilo walijeruhiwa katika ajali ya gari iliyotokea eneo la Mbande, wilayani Kongwa baada ya basi walilokuwa wakisafiria kwenda kwenye michezo ya Afrika Mashariki, Mombasa nchini Kenya, kugongana na lori lililokuwa likitoa Morogoro kuelekea Dodoma.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne, Desemba 10, 2024 Meneja Mawasiliano MOI, Patrick Mvungi amesema wamepokea wabunge watatu kwa ajili ya matibabu zaidi.
Mvungi amewataja wabunge hao kuwa ni Mwakilishi wa Jimbo la Magomeni Zanzibar, Mwanakhamis Kassim Said, Mwakilishi wa Jimbo la Amani Zanzibar, Abdul Yusufu Maalim pamoja na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mwanza, Furaha Matondo.
“Tumewapokea na kwa sasa wanapatiwa matibabu na wanaendelea vizuri, hatuwezi kufafanua zaidi,” amesisitiza Mvungi.
Wabunge waliokuwa wamelazwa katika Hospitali ya Kanda ya Benjamini Mkapa baada ya kupata ajali hiyo wameruhusiwa baada ya kupata matibabu.
Akizungumza leo mmoja wa maofisa wa Bunge, Patson Sobha amesema, “taarifa nilizonazo ni kwamba wabunge wote waliokuwa wamelazwa Benjamini Mkapa wameruhusiwa isipokuwa wale watatu ambao walipelekwa Muhimbili.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, George Katabazi amesema ajali hiyo ilisababisha jumla ya majeruhi 23 ambao ni Laurent Kyombo (Nkenge), Asia Abdulkarim Halmaga (Manyara-Viti Maalumu), Nicodemus Maganga (Mbogwe) na Grace Tendega (Viti Maalumu-Iringa).
Wengine ni Suma Fyandomo (Viti Maalumu (Mbeya), Zulfa Mmaka Omar (Kusini Pemba), NIcholaus Ngassa (Igunga), Juliana Shonza (Viti Maalumu-Songwe) na Catherine Magige (Viti Maalumu- Arusha).
Wengine ni Shamsia Mtamba (Mtwara Vijijini), Jesca Msambatavangu (Iringa Mjini), Sasisha Mafuwe (Hai), Furaha Matondo (Viti Maalumu).
Amewataja watumishi waliojeruhiwa kuwa ni Angela Haule na Elizabeth Masishanga wakati polisi waliojeruhiwa katika ajali hiyo ni Koplo Oscar na Nyamweko.
Pia amesema katika ajali hiyo dereva Bahati Juma alijeruhiwa.
Ajali hiyo ilihusisha basi la Kampuni ya Shabiby ambalo lilikuwa limebeba wabunge na maofisa wa Bunge na lori hilo lilikuwa likitokea Morogoro kuelekea Dodoma.
“Chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa gari hilo la Shabiby ambalo lilikuwa limebeba wabunge na maofisa wabunge kutochukua tahadhari alipotaka kulipita gari lililokuwa mbele yake, hivyo kugongana na lori hilo,” alieleza Katabazi katika taarifa yake kwa vyombo vya habari aliyoitoa Desemba 6.
Alisema dereva wa basi anashikiliwa na polisi kwa sababu yeye ndiye aliyesababisha ajali hiyo kwa kutochukua tahadhari.