Hali ya haki za binadamu Somalia inatia wasiwasi – DW – 09.05.2024

Katika mkutano na waandishi wa habari, Isha Dyfan ambaye ni mjumbe wa Umoja wa Mataifa ameweka bayana na kuelezea wasiwasi wake kutokana ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu nchini Somalia inayokabiliwa na machafuko ya kivita.

“Kuhusu hali ya usalama nchini humo, Somalia inazidi kukabiliwa na changamoto si haba. Raia na hasa wanawake na watoto wangali wanaathirika pakubwa kutokana na mashambulizi mengi yanayofanywa na kundi la kigaidi la Al-Shabaab.”

Kadhalika mtaalamu huyo huru wa haki za binadamu amewalaumu wale wote wanaohusika katika vita nchini Somalia kwa kutozingatia haki za binadamu hali ambayo imechangia ongezeko la visa vya unyanyasaji dhidi ya raia.

Soma pia: Kenya na Somalia zafungua ukurasa mpya wa ushirikiano

“Operesheni ya pamoja inayofanywa na jeshi, maafisa wa usalama na vikundi vilivyojihami vya kiraia, kwa lengo la kuwatimua wapiganaji wa al Shabaan pia imesababisha vifo vya raia wasio na hatia, sambamba na kuharibu miundo mbinu muhimu.”

Bi. Dyfan amezihimiza pande zote katika mzozo wa Somalia kuheshimu haki za binadamu kuambatana na mkataba wa kimataifa na utawala wa kisheria, akisema ni sharti pande hizo zikomeshe unyanyasaji wa raia na kuwaruhusu kupokea misaada.

Waandishi na watetezi wa haki za binadamu Somalia washambuliwa

Waandishi wa habari nchini Somalia mjini Mogadishu
Waandishi wa habari nchini Somalia mjini MogadishuPicha: Mohamed Dahir/AFP/Getty Images

Isha Dyfan amesema wakati wa ziara yake nchini Somalia, amekutana na kufanya mashauriano ya ana kwa ana na viongozi wa ngazi za juu serikalini, wakiwemo mawaziri, wawakilishi wa mashirika ya kutoa misaada, wanaharakati wa kutetea haki za binadamu na asasi za kiraia nchini humo.

Aidha Dyfan amesikitishwa na ripoti za hivi karibuni kuhusu matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu dhidi ya waandishi wa habari na watetezi wa haki za binadamu nchini Somalia, akisema zinatia wasiwasi mkubwa.

Soma pia: Al-Shabaab wawauwa zaidi ya askari 50 Somalia

Mtaalamu huyo kutoka Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa hakusita kuzungumzia vita vinavyoendelea nchini humo, hasa mashambulizi yanayoendeshwa na Wanamgambo wa Al-Shabaab.

“Ninashutumu vikali mauaji yanayoshuhudiwa kutokana na mashambulizi yanayofanywa na kundi la kigaidi la al-Shabaab, na ningependa kuihimiza serikali ichukue hatua madhubuti ili kulinda maisha ya raia.”

Ziara ya mjumbe huyo nchini Somalia ilichukua muda wa siku tano.

Hii ni mara yake ya tatu kuzuru nchi hiyo inayokumbwa na vita tangu alipoteuliwa na Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa mnamo Mei mwaka 2020 kuhudumu kama mtaalamu huru wa haki za binadamu wa Somalia. 

 

Related Posts