Huyu ndiyo Profesa Janabi usiyemjua

Dar es Salaam. Wakati Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akitaja jina la Profesa Mohamed Janabi kama pendekezo la nchi na ajiandae kugombea nafasi ya aliyekuwa Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, Dk Faustine Ndugulile, Mwananchi imekusogezea wasifu wake.

Akizungumza baada ya kuwaapisha viongozi mbalimbali leo Jumanne, Desemba 10, 2024 kwenye Ikulu Ndogo ya Tunguu, Zanzibar Rais Samia amesema wamepitia wasifu zaidi ya tano na kubaini kwamba Profesa Janabi ana sifa ya kurithi mikoba hiyo.

“Naomba nifichue siri hapa, tumepitia zaidi ya CV tano na tukaona Profesa Janabi anafaa kuchukua nafasi ya Dk Ndugulile. Hivyo, tunakuandaa kwenda kugombea nafasi hiyo muda utakapofikia. Ujiandae,” amesema Rais Samia.

Mshauri huyo wa masuala ya kiafya, wengi wamekuwa wakimfahamu kama Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete na baadaye Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), lakini Profesa Janabi ni zaidi ya nafasi hizo.

Profesa Mohamed Yakub Janabi ni Ofisa Mkuu Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) tangu mwaka 2022 hadi sasa. Ni mwanataaluma mbobezi katika sekta ya sayansi ya tiba akiwa na shahada tatu.

Shahada ya Awali ya Udaktari wa Tiba (MD), Shahada ya Uzamili ya Udaktari (MSc) na Shahada ya Uzamivu katika Sayansi ya Tiba (PhD).

Mtaalamu huyo wa sayansi ya tiba, ujuzi wake haujatamalaki nchini Tanzania pekee kwa kazi za kibobezi anazofanya kwenye utafiti na tiba, pia zimetandaa ulimwenguni kote.

Aidha, Profesa Janabi ni mhadhiri Mshiriki wa Chuo Kikuu cha Magonjwa ya Moyo cha Marekani (FACC). Pia, ni Mkaguzi wa matibabu wa usafiri wa anga aliyeidhinishwa na Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Marekani (FAA-USA).

Kabla ya kuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Muhimbili, Profesa Janabi alifanya kazi ya kibobezi katika Taasisi ya Magonjwa ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) ambako alikuwa Ofisa Mkuu Mtendaji kati ya mwaka 2015 hadi mwaka 2022.

Kuanzia mwaka 2005 hadi sasa, Profesa Janabi amekuwa daktari mkuu wa Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Jakaya Kikwete.

Nafasi nyingine alizonazo Profesa Janabi ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kuanzia mwaka 2000 hadi sasa na Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Tiba cha South Carolina, Marekani kuanzia mwaka 2003 hadi sasa.

Profesa Janabi anahudumu kama mjumbe wa bodi kwenye taasisi kubwa za huduma ya tiba nchini zikiwamo, Baraza la MUHAS kuanzia 2022 hadi sasa, JKCI, Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), Bodi ya Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA).

Pia ni mtafiti na mwanasayansi mwandamizi wa majaribio ya chanjo ya Ukimwi (TaMoVac) kuanzia mwaka 1989 hadi mwaka 2002. Pia, ni Daktari Mkurugenzi katika Shirika lisilo la kiserikali la madaktari wa Afrika lenye makao makuu yake Marekani.

Kwa miaka mingi ya utumishi wake kwenye tasnia ya sayansi ya tiba ndani na nje ya Tanzania, amejihusisha na tafiti nyingi na amefanikiwa kutoa machapisho 83.

Chapisho la mtindo wa maisha na afya yako, ni juhudi binafsi za Profesa Janabi za kuhamasisha Watanzania kutambua jambo moja kubwa kuhusu afya zao, kwamba mtindo wa maisha ni kichocheo kikubwa cha ama kuwa na afya njema au kinyume chake.

Katika kitabu hiki ambacho ni mchango wake kwa jamii, anatoa elimu pana kuhusu mtindo wa maisha, ulaji wa chakula na uhusiano wake na magonjwa mengi yasiyoambukiza.

Profesa Janabi ni mume na baba wa watoto wanne. Anazungumza na kuandika vyema lugha kadhaa ukiachana na Kiswahili anakijua vema Kiingereza, Kirusi na Kijapani.

Related Posts