SAA chache baada ya uongozi wa Coastal Union kutangaza kumalizana na kipa wake Ley Matampi, Mkongomani huyo ameibuka na kutaja sababu za kuachana na kikosi hicho.
Matampi ambaye ndiye kipa bora wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita akimpindua Djigui Diarra wa Yanga aliyebeba tuzo hiyo misimu miwili mfululizo, amesema jambo lililofanya kufikia uamuzi wa kuvunja mkataba uliosalia ni ishu ya kudai masilahi yake.
Mkongomani huyo aliyejiunga na Coastal Union Agosti 2023, mkataba wake ulitarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu baada ya msimu uliopita kutoa mchango wake mkubwa katika kuifanikisha timu hiyo kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Taarifa ya Coastal kuachana na kipa huyo ilisema: “Tumefikia makubaliano baina ya klabu yetu na kipa Ley Matampi ya kumaliza huduma ya pande zote mbili. Uzoefu wako umechangia kwa asilimia kubwa mafanikio yetu ya msimu uliopita.
“Shukrani za kipekee kwa kocha wa magolikipa Mansour Ally ambaye alitumia nguvu kubwa ya kurudisha uwezo na kiwango chako ukawa msaada mkubwa eneo la kulinda lango letu. Tunakutakia kheri nyingi na mafanikio zaidi katika maisha yako.”
Akizungumza na Mwanaspoti, Matampi alisema moja kati ya sababu kubwa la kufikia uamuzi huo wa kuvunja mkataba ni suala la malipo ambayo yamechelewa kwa kipindi kirefu kidogo jambo ambalo lilimfanya ashindwe kutumika vizuri.
“Nilipewa barua wiki iliyopita na kwangu naona ni uamuzi mzuri tu ambao klabu imefikia kwani sikuwa napata haki yangu kama ilivyotakiwa. Sijalipwa mshahara wangu miezi mitatu, suala ambalo sio zuri kwa upande wangu, niko tayari sasa kwa changamoto mpya,” alisema Matampi ambaye msimu huu hakuonekana uwanjani muda mrefu nafasi yake akicheza Chuma Ramadhan.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Coastal Union, Omar Ayoub alisema; “Klabu inafanya maamuzi ya wachezaji kutokana na ripoti ya benchi la ufundi, kwa hiyo tumeona uamuzi mzuri ni pande mbili kukaa na kufikia maamuzi ambayo tumetangaza.”
“Tumefanya maamuzi haya mapema ili tumpe nafasi mchezaji kutafuta klabu nyingine itakayomfaa ili na sisi Coastal Union tuendelee na maisha yetu, Matampi ni kipa mzuri na mkongwe tumejivunia kuwa sehemu ya klabu yetu kwa muda ambao ameitumikia.”
Wakati Ayoub akiyasema hayo, taarifa za ndani kutoka Coastal Union zinasema maamuzi hayo yametokana na kipa huyo kuwa na makosa mengi kwenye mechi ambazo alicheza msimu huu.
Bosi mmoja wa juu wa Coastal Union alisema kipa huyo amekuwa akiwagharimu kutokana na makosa aliyokuwa akiyafanya jambo lililowalazimu kumweka benchi na nafasi yake ikichukuliwa na kipa mzawa Chuma Ramadhan.
“Kuna mechi ambazo mabao yake yametugharimu sana ndio maana makocha wakaamua kumweka benchi ili ajitafakari, huyu ni kipa wa kigeni gharama zake kumhudumia ni kubwa sana, nadhani mechi alizocheza nyie waandishi mtaona wenyewe, fuatilieni mtaona kwa kipa wa viwango vyake ni vigumu kukubaliana na mnachokiona.
“Kwa sasa tunamtumia Chuma lakini mnaona namna tulivyo tulia ingawa sio sana lakini kuna unafuu, pia unapoamua kipa kama Matampi akae benchi lazima kiuongozi uangalie gharama zake, alikuwa amebakiza kama miezi mitano mkataba wake umalizike, tukaona ili kupunguza gharama ni bora tukaachana naye sasa kwa wema ili klabu nayo ijipunguzie mzigo wa gharama.”