Dar/Dodoma. Wakati dunia ikiadhimisha siku ya haki za binadamu, imeelezwa kuwa watetezi wa haki za binadamu wanapitia mazingira magumu kutokana na sheria kandamizi, udhaifu wa mfumo wa haki na udhibitiwa kwa vyombo vya habari.
Hayo yameelezwa leo Desemba 10, 2024 katika kongamano la haki za binadamu lililoandaliwa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) jijini hapa.
Akizungumzia wajibu wa vyombo vya habari katika utetezi wa haki za binadamu, mwandishi wa habari mkongwe nchini, Jenerali Ulimwengu amesema kutokana na kubanwa kwa sheria vyombo vya habari vimepoteza mwelekeo.
“Hali inazidi kuwa mbaya, sheria zinazopitishwa na Bunge, maelekezo yanayotolewa mara kwa mara, naona tunakwenda kuzibwa,macho, midomo na masikio,” amesema Ulimwengu.
Ameelezea uzoefu wake alipokuwa mbunge miaka ya 1990, kuwa walitoa mchango mkubwa licha ya kuwa katika mfumo wa chama kimoja.
“Nikiwa bungeni mwaka 1995, kulikuwa na wabunge 55 tulifanya makubwa ndani ya chama kimoja. Mojawapo ilikuwa ni Loliondo mwaka 1990, tuliiuliza Serikali ikajibu.
“Visiwa vya Mbudya hapa Dar es Slaam ilikuwa viuzwe kwa Waarabu, tukazuia.
Mimi nilipeleka hoja ya viongozi kutaja mali zao na wanahabari wapate bafasi ya kuona na kila mwaka viongozi wasaini.
Je, bado mnapata fursa ya kuona mali za viongozi, mawaziri, wakuu wa mikoa, wilaya?” amehoji.
Naye Wakili, Mpale Mpoki amesema licha ya Mahakama kuwa mamlaka ya kutoa haki na kuangalia utendaji wa utawala na Bunge, sheria ya utekelezaji wa haki za msingi inakwamisha haki hizo.
“Kati ya mihimili mingine, Mahakama imepewa mamlaka ya kuingilia vyombo vingine, kwani mbali na kutoa haki inakuwa na wajibu wa kuchunguza vyombo vingine kuhakikisha havifanyi kupita mamlaka yake.
Amesema baada ya haki za binadamu kuingizwa kwenye Katiba mwaka 1984, ilitakiwa itungwe sheria ya kuzitekeleza, lakini haikutungwa hadi mwaka 1994.
“Baada ya hapo ikatungwa Sheria ya Bradea ambayo badala yake ikaweka mazingira magumu zaidi, kwa kuwa walitunga pia kanuni ambazo ukifungua kesi na kukosea kanuni shauri linatupwa,” amesema Mpoki.
Amesema ugumu wa kutetea haki za binadamu unakuwa shakani kutokana na taratibu za mahakama, hasa mtu anapofungua shauri la kikatiba.
Amesema Mahakama ina masjala nyingi, lakini ukifungua kesi ya kikatiba inabidi iende Masjala Kuu Dodoma ndipo ipangiwe jaji eneo husika, jambo linalozidisha ugumu wa kupata haki.
Mbali na hilo, limejitokeza tatizo la Serikali kutoptekeleza hukumu za mahakama kama alivyoeleza Mkurugenzi wa Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (Tawla), Tike Mwambipile.
Akitoa mfano wa tatizo hilo, Mwambipile amesema miongoni mwa kesi ambazo walishinda na hukumu yake haikutekelezwa ni ya watoto wa kike waliopata mimba kuruhusiwa kurudi shule.
Awali, akizungumza katika mkutano huo, Mratibu wa THRDC, Onesmo Olengurumwa alisema licha ya Rais Samia kuonyesha utashi wa kisiasa kwa kurekebisha baadhi ya mambo yaliyolalamikiwa, suluhisho la mambo yote hayo ni kuwa na katiba mpya.
Wakati huo huo, akizungumzia miaka 28 baada ya Ripoti ya Hali ya Rushwa ya Jaji Mstaafu, Joseph Warioba itolewe, Mkurugenzi wa mashtaka na ufuatiliaji wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, (THBUB), Philipo Sungu amesema bado inatakiwa kufanyiwa kazi.
Sungu amesema hayo katika kongamano la watumishi wa umma la tathmini uzingatiaji wa haki za binadamu na kuepuka rushwa, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya maadili na haki za binadamu.
Amesema ripoti mbalimbali za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) za kuanzia mwaka 2020/21 hadi mwaka 2023/24, zinaonyesha changamoto ya rushwa bado ipo.
Sungu amesema rushwa imeripotiwa kuongezeka katika nyanja za uchumi, huduma na siasa nchini.
“Unaona ripoti ya Warioba ya mwaka 1996 ni kama imetolewa leo. Hizo taarifa za CAG, zinabaanisha kuwa bado kuna rushwa katika taasisi za umma…Bado ripoti ya Warioba inatakiwa kufanyiwa kazi,” amesisitiza.
Amesema ripoti hiyo ya Warioba inafafanua kuwa bado kuna rushwa katika ofisi za umma na hata sasa bado inaendelea katika taasisi hizo.
Suala jingine lililojitokeza katika kongamano hilo ni haki ya faragha na usalama wa mtu kama inavyozungumzwa katika ibara ya 16 ya Katiba ya Tanzania, lililoibuliwa na Dk Ombeni Msuya, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom).
Amesema wakati haki hiyo kwa kiasi kikubwa inasimamiwa na mamlaka ambazo zimepewa kusimamia usalama wa raia na mali, vyombo hivyo pia vinalalamikiwa kuzivunja.
“Sasa kuna mahala pamefika pameibuka mitizamo tofauti, ambayo kimsingi ni hasi kwa vyombo hivyo, kiuwa wakati mwingine vinachukua majukumu ambayo si halali kwa wananchi, ndiyo maana misuguano haiishi na watu wanapoteza imani juu ya vyombo hivyo,” amesema.
Dk Msuya amesema siku ambayo watajenga jamii ya Watanzania ikaamini kwamba majeshi yao na vyombo vingine havifanyi kazi kwa weledi wa kuwalinda, itakuwa ni hatari zaidi.
“Kwa sababu hatutaweza kukaa tena, tukazungumza habari ya kusherekea hizi siku za haki za binadamu kama tayari amani yetu itakuwa imevurugika. Sisi kama watumishi wa umma, kama Taifa ni lazima hatuna chaguo ya kujenga tena mtazamo upya kwa jamii, mtazamo ambao ni chanya,” amesema.
Akifungua kongamano hilo, Mwenyekiti wa THBUB, Jaji Mstaafu Mathew Maimu amewataka watumishi wa umma ambao ndio injini ya Serikali, kuzingatia maadili na haki za binadamu katika kutekeleza falsafa nne za Rais Samia Suluhu Hassan.