Dk Medard Kaiza: Kutoka kuchunga mbuzi Bukoba hadi mtafiti wa saratani Marekani

Marekani. Hadithi ya Medard Kaiza inafanana na muswada wa filamu ya Hollywood; nafasi yake ya kufika kileleni katika uwanja wa sayansi, akiwa bega kwa bega na wanasayansi maarufu katika vyuo vikuu vya Japani na Marekani, inaonekana kama hadithi ya kufikirika.

Dk Kaiza alikulia akichunga mbuzi katika kijiji kilichozungukwa na milima ya Bukoba, maisha ya kijijini ambayo bado anayafurahia hadi leo, akiwa katika kazi yake ya utafiti katika Chuo Kikuu cha Pittsburgh, ambapo ni mtaalamu wa utafiti wa saratani katika Kituo cha Saratani cha Binadamu.

“Kazi yangu inahusu saratani ya mapafu na kichwa na shingo; lengo langu ni kupata tiba ya saratani na pia kuhakikisha juhudi zote zinachukuliwa ili wagonjwa wa saratani waishi maisha bora na ya muda mrefu,” alielezea Dk Kaiza alipokuwa akizungumza na gazeti dada la The Citizen.

Utafiti wa Dk Kaiza unalenga katika elimu ya kinga maradhi, akizingatia kuelewa seli za saratani katika uvimbe unaokua kwa wagonjwa na kusaidia kukuza kinga dhidi ya uvimbe.

Kazi yake ni ya mikono; anatoa tishu za uvimbe kutoka kwa wagonjwa na anawasiliana nao kuona jinsi wanavyoendelea.

Furaha yake inatokana na kuona maisha ya wagonjwa yanavyoboreka. Licha ya kuwa na shughuli nyingi za kazi na miradi ya utafiti, hakuwahi kupuuza kurudi nyumbani Tanzania; anajivunia asili yake na hiyo imefanya nyumbani kuwa sehemu ya vipaumbele vyake. Novemba 2024, alirudi nyumbani, na vijana walimtazama kwa mshangao kwa mafanikio aliyoyapata.

“Wananiuliza kila mara jinsi ambavyo Mtanzania kama mimi anavyofanya kazi katika Chuo Kikuu cha Pittsburgh cha heshima. Wanadhani ni kutoka familia tajiri au baba yangu ni mtu maarufu Tanzania. Si hivyo, mimi natoka kijiji kidogo sana Bukoba,” alisema.

Wazazi wa Dk Kaiza walifariki kwa ugonjwa wa Malaria alipokuwa mdogo. Kifo cha wazazi wake kilimfanya kujikita zaidi katika utafiti wa Malaria baadaye katika maisha yake ya masomo, akitumaini kwamba hakuna mtoto wa Kitanzania atakayepitia maumivu aliyopitia yeye alipowapoteza wazazi wake kwa ugonjwa unaoweza kutibika.

Alisoma katika Shule ya Sekondari ya Kibaha baadaye aliendelea na shahada yake ya kwanza katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Safari yake ilibadilika alipokubali fursa ya masomo aliyopewa, kinyume na ushauri wa marafiki zake, iliyompeleka Japan, ambapo Shahada ya uzamivu  katika Taasisi ya Tiba ya Tropiki ya Chuo Kikuu cha Nagasaki, Kitengo cha Malaria. Alikaa Japan kwa miaka mitano akipambana kujifunza na kutafuta njia ya kutokomeza Malaria Afrika juhudi zinazosukumwa na wazazi wake kufariki kwa ugonjwa huo.

Ameandika makala kadhaa zinazozungumzia kwa kina kazi yake kuhusu Malaria.

Baada ya miaka mitano Japan, alikubaliwa kufanya kazi Marekani katika Taasisi ya Kitaifa ya Afya (NIH), iliyopo Bethesda, Maryland, karibu na Washington, DC, ambapo aliendelea kufanya utafiti wake.

“PhD yangu ilikuwa katika magonjwa yasiyoambukiza, hasa Malaria, hivyo nilikwenda Maryland na kuendelea na utafiti wangu na wanasayansi wazuri pale,” anakumbuka.

Muda wake katika NIH ulikuwa na mafanikio makubwa, ambapo utafiti alioshiriki uliacha alama, ukiwa umechapishwa katika vyombo vya habari.

Utafiti wao ulilenga Malaria na jinsi vimelea vya ugonjwa huo vinavyoshambulia kinga ya mwili ya binadamu. Kwa ufupi, mtu anapopatwa na maambukizi, vimelea vya Malaria vinapata hifadhi inayowasaidia kuvamia mfumo wa kinga.

Baadaye, aligeukia utafiti wa saratani, jambo ambalo lilikuwa likimvutia tangu awali, na ndipo alipojiunga na Kituo cha Saratani cha Chuo Kikuu cha Pittsburgh. Kazi yake inahusu uchunguzi wa tishu za saratani.

Baada ya mgonjwa kupata matibabu kutoka kwa daktari, tishu za mwili huziondoa, na kwa idhini ya familia ya mgonjwa, tishu hizo hufika kwenye meza yake kwa ajili ya utafiti zaidi, akilenga kupata mapinduzi na njia bora za kupigana na magonjwa hayo yanayotesa.

“Tunaweza kuchukua uvimbe na kuchunguza seli zake na kuona hali ya mgonjwa, na hiyo itasaidia kuamua dawa atakazopatiwa na daktari,” alisema.

Katika zama hizi za kisasa, utafiti wa tiba ya saratani bado umejificha, lakini umakini na mfululizo wa juhudi ni vitu vinavyowawezesha madaktari kama Kaiza kuwa na matumaini kwa siku zijazo.

“Katika utafiti, mara nyingi asilimia 99 inafanikiwa, lakini tunazingatia asilimia moja ambayo haifanikiwi, na tunaifanyia kazi,” alieleza. Hivi sasa, NIH inatengeneza chanjo ya Malaria kulingana na matokeo ya utafiti wao.

Dk Kaiza amekuwa akirudi nyumbani kila mara; bado anastaajabu kwa mafanikio aliyoyapata. Kijiji chake, hadi leo, kinakutana na changamoto za barabara mbovu na upungufu wa maji, jambo ambalo anatumai atafanikiwa kulitatua hivi karibuni.

“Kwa mwenye kupata mengi, inatarajiwa kutoa mengi, najihisi kuwa na jukumu la kuchangia kiakili kwa watu wangu. Mimi bado ni sehemu ya jamii yangu,” alisema.

Jamii anayotoka inaonyesha jinsi maisha yake yalivyokuwa ya unyenyekevu na jinsi umakini na uthubutu unavyoweza kumjenga mtu hadi kufikia mafanikio.

Dk Kaiza haoni kuwa yeye ni mwerevu au mwenye kipaji cha kipekee, bali alifaidi fursa zilizojitokeza mbele yake.

Alipokuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akitafuta ufadhili wa masomo kwenda Japan, alizungumza na marafiki zake na kuwahimiza nao waombe. Walikuwa wote hawana ajira, na marafiki zake walikataa fursa hiyo kwa sababu ilihitaji kujifunza Kijapani kwa miezi sita.

Kwa Dk Kaiza, ilikuwa ni faida kupata kujifunza lugha mpya bure. Maisha hayakumpatia kila kitu kwa urahisi, akiwa yatima alijua kuwa kila fursa aliyopewa ilikuwa ni baraka, na alijua kuwa njia pekee ya kutoka kwenye umasikini ilikuwa ni elimu. Hakuwa katika familia ambayo ingeweza kumsaidia kwa mamilioni kwa ajili ya mtaji wa biashara.

“Watu wanasema elimu ni msaada mkubwa, na nakubaliana na hilo,” aliongeza. Wakati akiwa katika NIH, Washington, DC, Dk Kaiza tayari alikuwa ameanzisha juhudi za kubadilishana maarifa kati ya NIH na taasisi mbalimbali nchini Tanzania.

Kuhusu taarifa potofu zilizojaa duniani kuhusu sayansi, hasa kuhusu chanjo baada ya janga la Covid-19, zinazochochewa na machapisho mtandaoni yanayouliza maswali kuhusu sayansi. Dk Kaiza alisema kuwa ili kujua jinsi chanjo zinavyofanya kazi, lazima uangalie kipindi cha mwanzoni mwa miaka ya 1800.

Maisha yalikuwa na matarajio ya umri wa miaka 40, lakini leo hii ni katika miaka 90, na kile kilichobadilika ni maendeleo ya chanjo mbalimbali kama za polio na homa ya mapafu, ambazo zilisaidia watu kuishi maisha bora na kujilinda dhidi ya magonjwa haya, na yote hayo ni matokeo ya sayansi.

Akizungumzia hali ya saratani nchini Tanzania, anatumai kuwa kama Taifa tunaweza kuiga yale waliyofanya mataifa yaliyostawi kuhusu huduma kwa wagonjwa na miundombinu ya matibabu ya saratani.

Anatumaini kuwa hadithi yake itachochea upendo kwa sayansi na ndoto kubwa miongoni mwa vijana wa Kitanzania.

“Bila shaka wazazi wangu wangekuwa hai wangefurahia kile ninachochangia katika nyanja ya sayansi, hasa katika saratani na Malaria.”

Related Posts