Dk Hulda Zelothe: Safari ya mafanikio ya udaktari bingwa wa mifupa katika umri mdogo

Dar es Salaam. Dk Zelothe, ni daktari bingwa wa mifupa na majeraha wa kike mwenye umri mdogo zaidi nchini Tanzania, ni kielelezo cha uvumilivu, bidii na maono thabiti ya kubadilisha mfumo wa huduma za afya nchini. 

Alizaliwa mkoani Kilimanjaro mwaka 1995 akiwa mtoto wa mwisho miongoni mwa ndugu wanne. Safari ya Dk Zelothe ilikuwa ni ndoto yake ya tangu utotoni. 

“Nilipokuwa na umri wa miaka tisa, nilijua nataka kuwa daktari,” anakumbuka kwa tabasamu. “Fikra ya kuokoa maisha ilinivutia sana, na nilihisi ni wito wa baraka.”anasema Dk Zelothe alipokuwa kwenye mahojiano na gazeti dada la The Citizen. 

Safari yake ilianza kwa msingi thabiti wa mafanikio ya kitaaluma. Alisoma Shule ya Msingi Green Acres jijini Arusha na kusoma kidato cha kwanza hadi cha nne katika Shule ya Sekondari ya St. Mary’s Mazinde Juu mkoani Tanga. Masomo yake ya kidato cha tano na cha sita  aliyakamilisha katika Shule ya Sekondari ya Tanzania Adventist iliyopo Arusha. 

Bidii yake ilimpatia nafasi ya kusomea udaktari nje ya nchi, ambapo alihitimu shahada ya kwanza katika Chuo Kikuu cha Matibabu cha Zhejiang nchini China. 

“Kusoma nje ya nchi kulibadilisha mtazamo wangu. Nilifundishwa na profesa wa upasuaji wa uti wa mgongo ambaye alinipa hamasa ya kubobea katika tiba ya mifupa.” Shauku na utaalamu wake vilinichochea kuleta maarifa hayo nyumbani Tanzania.”anasema. 

Aliporejea nyumbani, Dk Zelothe alikumbana na changamoto zinazowakumba madaktari wengi vijana, zikiwamo ukosefu wa nafasi za ajira na matatizo ya kifedha.

Hata hivyo, hakutetereka na aliendelea kufuatilia malengo yake kwa kujiunga na shahada ya uzamili ya mifupa na majeraha katika Chuo Kikuu cha Kilutheri cha Kikristo cha Kilimanjaro (KCMUCo). 

Hivi sasa akiwa muhitimu wa karibuni, ni mmoja wa madaktari bingwa wa mifupa wa kike wasiozidi 30 nchini Tanzania, akivuka vikwazo na kuhamasisha kizazi kijacho cha wataalamu wa afya. 

Kwa mujibu wa Taasisi ya Kitaifa ya Utafiti wa Matibabu, Tanzania yenye idadi ya watu zaidi ya milioni 60 ina madaktari bingwa wa mifupa 118 pekee, sawa na daktari mmoja kwa kila wananchi 508,000.

Kwa kulinganisha, Marekani ina daktari bingwa mmoja wa mifupa kwa kila wananchi 10,800. Tofauti hii inaonyesha haja ya dharura ya kuongeza idadi ya wataalamu katika fani hii. 

“Ni heshima kubwa na pia jukumu zito kuwa sehemu ya kundi hili dogo. Lengo langu ni kuwahamasisha wanawake vijana kuona fani hii kama taaluma inayowezekana na yenye kutosheleza,” anasema daktari huyo kijana. 

Majeraha ya mifupa yanaongezeka nchini Tanzania, hasa kutokana na ajali za barabarani, ambazo zinachangia karibu nusu ya kesi zote za majeraha. 

“Mahitaji ya huduma za mifupa ni makubwa, lakini rasilimali na nguvu kazi ni ndogo,” anasema Dk Violet Lupondo, makamu wa pili wa rais wa Shirika la International Orthopedic Diversity Alliance.

Dk Violet Lupondo anabainisha kuwa maeneo ya vijijini ndiyo yanayokumbwa zaidi na changamoto ya ukosefu wa huduma za afya. “Ni asilimia 20 tu ya madaktari wanaofanya kazi vijijini, wakati asilimia 73 ya Watanzania wanaishi huko. Hali hii ya kutokuwa na uwiano lazima ishughulikiwe ili kuhakikisha upatikanaji wa huduma za afya kwa usawa,” anasema. 

Daktari bingwa wa majeraha na mifupa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dk Silas Kiwelu, anasisitiza umuhimu wa mbinu mbalimbali za kushughulikia pengo hili. 

“Serikali inapaswa kuanzisha vituo vya ubingwa wa mifupa katika ngazi za mikoa ili kutoa mafunzo na nafasi za ushauri kwa wahitimu wa udaktari wanaovutiwa na upasuaji,” anapendekeza Dk Kiwelu.

Aidha, utoaji wa ufadhili wa masomo kwa ajili ya ubobezi wa tiba ya mifupa unaweza kuwahamasisha wanafunzi wengi kuingia katika fani hiyo, huku akisisitiza umuhimu wa teknolojia. “Vifaa vya kisasa vya uchunguzi na matibabu, kama mashine za picha za ndani ya mwili na roboti za upasuaji, vinaweza kuongeza ufanisi wa madaktari bingwa wa mifupa na kufanya fani hii kuvutia zaidi kwa wataalamu vijana,” anasema. 

Mtaalamu wa sera za afya, Dk Regina Mbunda, anaeleza changamoto nyingine inayochangia tatizo hili kuwa ni ukosefu wa uelewa kuhusu tiba ya mifupa miongoni mwa jamii na wanafunzi wa udaktari. 

“Wanafunzi wengi wa udaktari hawajui fursa zilizopo kwenye tiba ya mifupa kwa sababu ya ukosefu wa mafunzo maalumu katika programu zao za masomo. Tunapaswa kuingiza programu za mifupa kwenye mitaala ya shahada ya kwanza na pia kutoa nafasi za mafunzo kwa vitendo katika vituo vya majeraha,” anasema Dk Regina. 

Anaamini kuwa Dk Hulda Zelothe anaweza kuchukua nafasi muhimu kama mshauri.

“Kulingana na historia na mafanikio yake, anaweza kuwahamasisha wengine kujiunga na fani hii. Dk Zelothe ni mfano halisi wa mabadiliko tunayoyahitaji,” Regina anasisitiza. 

Safari ya Dk Zelothe haikuwa rahisi

Kulinganisha mahitaji makubwa ya masomo ya udaktari na matarajio ya kijamii kama mwanamke lilikuwa moja ya changamoto zake kubwa. 

“Nilikuwa na nyakati za kutilia shaka uwezo wangu,” anakiri. “Fani ya mifupa kwa kawaida inatawaliwa na wanaume na ni rahisi kujihisi umetengwa.” 

Anasema kuwa mafanikio yake yametokana na uvumilivu, msaada wa familia, na imani yake thabiti. “Nilishinda changamoto hizi kupitia maombi na usaidizi wa wale waliokuwa na imani nami,” anasema. 

Changamoto za kifedha pia ziligubika safari yake, kwani alijigharamia masomo yake ya uzamili. Hata hivyo, dhamira yake ya kufikia ndoto zake ilimpa nguvu ya kuendelea. 

Dk Zelothe ana ndoto zinazovuka mafanikio yake binafsi,  anaiona Tanzania yenye upatikanaji wa huduma za mifupa kwa kila mtu, bila kizuizi cha ukosefu wa huduma. 

“Lengo langu kuu ni kupanua upatikanaji wa huduma bora za mifupa kote nchini Tanzania, hasa katika maeneo ya vijijini ambayo hayahudumiwi ipasavyo,” anasema. 

Anapanga kuanzisha programu za kufikia jamii, kuwafundisha madaktari vijana na kushawishi sera zinazoboresha miundombinu ya huduma za afya.

Hitaji la mabadiliko ya kimuundo 

Ripoti ya ‘Lancet Commission on Global Surgery’ inakadiria kuwa angalau wataalamu 20 hadi 40 wa upasuaji wanahitajika kwa kila watu 100,000. Hata hivyo, Tanzania iko mbali sana na kiwango hiki cha kimataifa. 

Mtaalamu wa uchumi wa afya, Dk Alex Malamsha, anaonya kwamba bila kuchukua hatua za haraka, mzigo wa magonjwa ya mifupa yasiyotibiwa utaendelea kuongezeka kwa kasi kubwa. 

“Ajali za barabarani peke yake zinagharimu Tanzania mabilioni kila mwaka kutokana na gharama za matibabu. Kuwekeza katika huduma za mifupa si jukumu la kimaadili tu, bali pia ni hitaji la kiuchumi,” anasema Dk Malamsha. 

Anapendekeza Serikali kuhamasisha uwekezaji wa sekta binafsi katika hospitali za mifupa na kuimarisha ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi ili kupunguza pengo la huduma. 

Matokeo ya Dk Hulda Zelothe tayari yameanza kuonekana. Kama miongoni mwa wanawake wachanga wa kwanza katika fani yake, amekuwa kielelezo cha kuigwa na madaktari wanaochipukia. “Nataka kuwaonyesha wanawake vijana kwamba kwa bidii na shauku, nao wanaweza kuvuka vizuizi katika fani hii,” anasema. 

Dk Rutwaza Ndaki kutoka Chuo, Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi. Muhimbili (MUHAS) anakubaliana na mtazamo huu. “Historia ya Dk Zelothe ni ushahidi wa kile kinachowezekana tunapowekeza katika elimu na ushauri. Yeye ni mwakilishi wa mustakabali wa huduma za mifupa nchini Tanzania,” anasema. 

Kuhamasisha wanawake zaidi kuingia katika fani ya mifupa kunahitaji mabadiliko ya kimuundo. Dk Zelothe anaamini kuwa programu za ushauri, ufadhili wa masomo ya udaktari na sera zinazojumuisha jinsia zote ni muhimu. 

“Kushirikisha historia za wanawake waanzilishi kunaweza kuhamasisha wengine. Tunahitaji pia kuwapa wanafunzi nafasi ya kufahamu tiba ya mifupa mapema katika mafunzo yao ili kuwachochea kuvutiwa na fani hii,” anasema. 

Kwa upande wake, Dk Lupondo anapendekeza kuongezwa kwa msaada wa kifedha kwa wanafunzi wa udaktari wa kike na kuanzishwa kwa ratiba za kazi zinazobadilika, ili kuvutia wanawake wengi zaidi kuingia katika taaluma inayohitaji kujitolea kama upasuaji. 

Safari ya Dk Zelothe inakuja wakati muhimu kwa sekta ya afya ya Tanzania. Kwa mujibu wa takwimu, majeraha yanachangia asilimia tisa ya vifo duniani, na asilimia 90 ya vifo hivi hutokea katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati kama Tanzania. Mahitaji ya huduma za mifupa hayajawahi kuwa ya dharura kama sasa. 

Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2025 inalenga kutoa huduma bora za msingi za afya kwa wote, lakini kufanikisha lengo hili kunahitaji kushughulikia uhaba wa wataalamu wa fani maalumu. 

Licha ya changamoto, Dk Zelothe anaendelea kuwa na matumaini. “Ninaiona Tanzania ambako huduma za mifupa zinapatikana kwa wote,” anasema. “Hakuna mgonjwa anayepaswa kuteseka kwa sababu ya eneo au hali yake ya kifedha.” 

Dhamira yake ya kuleta mabadiliko katika mfumo wa afya inahamasisha kizazi kipya cha madaktari wanawake wa upas

Related Posts