Una ujuzi hauna vyeti, FundiSmart itakuwezesha kuvipata na ajira

Dar es Salaam. Kama wewe ni fundi wa ujenzi au umeme na hadi sasa unakula msoto wa kukosa ajira, fursa hii inakuhusu kuhakikisha unapata kazi na kujikwamua kiuchumi.

Suala la ama una cheti au hauna si tatizo, fursa hizo za kazi, zinahitaji uwezo wako wa kutekeleza shughuli za ufundi husika.

Hiyo ni baada ya kampuni ya FundiSmart kuanzisha utaratibu wa kuwaunganisha mafundi hao na wadau wanaojishughulisha na masuala hayo.

Kampuni hiyo inayojishughulisha na mafundi ili kufanya ufundi wao kibiashara zaidi utakaowawezesha kuishi maisha ya ndoto zao.

Lakini hata wale mafundi wenye ujuzi ambao hawakufanikiwa kwenda darasani sasa watapata vyeti kwa kuwekewa mazingira mazuri ya kusoma, ili kupata cheti kitakachowawezesha kutambulika.

Akizungumzia fursa hiyo jana Jumatatu Desemba 9, 2024, Mkurugenzi wa FundiSmart, Fredy Herbet amesema wamedhamiria kuwasaidia mafundi ikiwemo kuwakutanisha na taasisi za kifedha zitakazowasaidia.

“Mafundi wengi hawajui wakitaka kukopa wanafanyaje? Au atakopa wapi ila wakijiunga na FundiSmart na kutambuliwa itakuwa rahisi kwao kuzipata fursa hizo.

“Tunawasaidia kuwakutanisha na kazi mbalimbali zinazotokea na tumesaini makubaliano na Mamlaka ya Elimu ya Ufundi Stadi nchini (Veta) katika kutelekeza jukumu hili,” amesema Herbet.

Kwa mujibu wa Herbet, makubaliano hayo yatawezesha pia wale mafundi wa fani mbalimbali wasiokuwa na vyeti kuvipata, sambamba na kuunganishwa na fursa zitakazojitokeza.

“Moja ya jambo lililosababisha tusaini makubaliano haya sisi tunao mafundi lakini hawana vyeti, ila wamefanya ufundi muda mrefu labda utakuta mtu ni fundi cherehani tena mzuri tu lakini hajasomea na anapata wateja.”

“Sasa ikitokea fursa yoyote iliyopo kwenye mfumo hawezi kuipata kwa sababu hana cheti ila ni fundi mzuri, lakini hajarasimishwa. Haya makubaliano tuliosaini nchini nzima yatawezesha mafundi kusoma na kupata vyeti,” amesema Herbet.

Herbet ametoa wito kwa mafundi wasiokuwa na vyeti lakini wana ujuzi, watapata fursa ya masomo yatakayowawezesha kupata cheti ili kupata kazi katika miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali.

Mkurugenzi huyo amesema makubaliano hayo yanafungua fursa kwa mafundi kurasimisha ufundi wao kupitia vyuo vyote vya Veta, akisema hadi hivi sasa zaidi ya mafundi 30,000 wameshafikiwa nchini nzima.

Ametoa wito kwa taasisi za kifedha, bima, watengenezaji na wasambazaji wa vifaa vya ujenzi,  vipuri vya magari na wasambazaji wa oil na vilainishi vingine, kushirikiana na FundiSmart katika kufanikisha hilo.

Related Posts