Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Serikali imesisitiza dhamira yake ya kuchukua hatua kali dhidi ya taasisi za fedha zinazotoa mikopo ya “umiza” yenye riba kubwa zinazowakandamiza wananchi. Onyo hili limetolewa leo Desemba 10, 2024, jijini Dar es Salaam na Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, wakati wa uzinduzi wa Jukwaa la Kwanza la Wadau wa Sekta ya Fedha kwa mwaka 2024.
Dk. Nchemba amesema taasisi zisizo rasmi zimekuwa zikiwakandamiza wananchi kwa kutoa mikopo yenye masharti magumu na kupanga njama za kufilisi mali za wadaiwa.
“Wananchi wanapaswa kutofautisha taasisi rasmi na zisizo rasmi. Lazima tuwaelimishe kuwa benki ni mahali salama zaidi kwa huduma za kifedha,” alisema Dk. Nchemba.
Amezitaka benki na wadau wa sekta ya fedha kuhakikisha wananchi wanapewa elimu ya umuhimu wa kutumia huduma rasmi za kifedha, ikiwemo kupata mikopo na kuhifadhi fedha zao katika taasisi zilizosajiliwa.
Waziri huyo pia ameeleza wasiwasi kuhusu unyonyaji unaotokea wakati wa minada ya mali za wadaiwa.
“Mteja aliyelipa asilimia 80 ya mkopo wake hastahili kufilisiwa kwa sababu ya asilimia 20 aliyobaki nayo. Hii siyo njia ya kujenga sekta ya fedha wala ustawi wa jamii,” alisisitiza Dk. Nchemba.
Aliziagiza benki kuhakikisha watumishi wao na madalali hawatumii minada kama fursa ya kuwadhulumu wadaiwa.
Dk. Nchemba aliwataka wadau wa sekta ya fedha kuhimiza matumizi sahihi ya mikopo, akieleza kuwa mikopo inapaswa kuelekezwa katika miradi ya uzalishaji mali ili kurahisisha marejesho.
“Fedha za mkopo zinapaswa kutumika kwenye shughuli za uzalishaji, kama inavyofanyika kwa fedha za mikopo ya miradi ya maendeleo ya kitaifa,” alisema.
Amebainisha kuwa Tanzania ni mojawapo ya nchi mbili pekee barani Afrika zilizo na uhimilivu wa deni, huku ikiendelea kuongoza katika Afrika Mashariki na SADC kwa usimamizi bora wa deni la taifa.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, alisema Serikali itaanzisha mtaala mpya wa masomo ya fedha na ujasiriamali ifikapo mwaka 2025. Somo hili litakuwa la lazima kwa wanafunzi ili kuwaandaa kujiajiri baada ya masomo.
“Tunakaribisha maoni kutoka kwa wadau kuhusu mtaala huu ili kuhakikisha unakidhi mahitaji ya jamii,” alisema Prof. Mkenda.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk. Natu El-maamry Mwamba, alisema Jukwaa hili limeandaliwa ili wadau kubadilishana mawazo, uzoefu, na mbinu bora za kuboresha sekta ya fedha.
Malengo ya jukwaa ni pamoja na: Kutathmini utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha (2020/21-2023/24). Kukuza matumizi ya teknolojia na uvumbuzi katika sekta ya fedha. Kuimarisha ushirikiano kati ya wadau wa sekta ya fedha. Kutoa taarifa za maboresho ya kisera na kisheria yaliyofanyika.
Dk. Mwamba alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuchukua hatua madhubuti kuboresha mazingira ya sekta ya fedha na kuwahamasisha wananchi kutumia huduma rasmi kwa ajili ya ustawi wa kifedha na kiuchumi.