Ileje. Wazazi na walezi mkoani Songwe wameonywa kumalizana kindugu juu ya Kesi za ukatili wa kijinsia kwa watoto, ili wahusika wanaotekeleza vitendo hivyo wachukuliwe hatua za kali za kisheria.
Rai hiyo imetolewa na Kaimu Mkuu wa kitengo cha dawati la jinsia kutoka Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Eletisia Mtweve, katika maadhimisho ya Siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia yaliyofanyika kimkoa katika Wilaya ya Ileje leo Desemba 10 2024.
Mtweve amesema dawati la polisi la jinsia licha ya kupokea taarifa ya vitendo vya ukatili lakini hushindwa kuendelea na michakato ya kisheria ili haki kutendeka, kutokana na kukwamishwa na baadhi ya wazazi na walezi, ikiwemo jamii kushindwa kutoa ushirikiano ikiwemo kumalizana nyumbani.
Amesema katika siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia , dawati limeadhimisha siku hizo kwa kutoa elimu maeneo mbalimbali pamoja na kupokea waathirika 41 ambapo wa kike ni 36 na wanaume watano.
Asimwe Nyondo Mkazi wa Isongole amesema wanashindwa kuripoti matukio ya ukatili kutokana na vitisho wanavyopewa dhidi ya wananchi, kwani baadhi yao hutenda makosa hayo kutokana na imani za kishirikina.
“Matukio ya ubakaji ,ulawiti yapo lakini tunaogopa kuripoti kwani tunahofia maisha yetu, lakini elimu tuliyoipata leo kwenye maadhimisho haya tutakuwa mstari wa mbele kuripoti ili wahusika washughulikiwe,” amesema Nyondo.
Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Frida Mgomi ametumia jukwaa hilo kutoa wito kwa kila mtu kutathmini majukumu yake na kwa nafasi aliyonayo katika jamii kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Mgomi amesema mkoa huo umeendelea kutoa elimu ya ukatili na madhara yake kwa jamii, kupitia wataalamu mbalimbali wakiwemo maofisa ustawi wa jamii, polisi dawati la jinsia, wanasheria, maofisa maendeleo wa jamii, madaktari, wauguzi na wadau.
Amesema wataalamu hao hukutana na kuwahudumia waathirika wa changamoto wakiwamo wa jinsi zote.
Amewataka waathirika wa matukio ya ukatili kutoa taarifa ndani ya saa 72 za uwepo wa kiashirikia au matendo ya ukatili miongoni mwao kuanzia ngazi ya halmashauri, kata, vitongoji na vijiji.
Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya ametoa onyo kwa Jeshi la Polisi juu ya malalamiko ya kuchepusha ushahidi kwenye kesi za matukio ya ukatili wa kijinsia kama ulawiti na ubakaji, ikiwemo kuchukua rushwa.
Malalamiko ya polisi kushindwa kutenda haki kwenye upelelezi kwa kuchepusha ushahidi, ikiwemo vyombo vya sheria kushindwa kutenda haki kwenye matukio ya ukatili wa kijinsia kama ulawiti na ubakaji yaliibuliwa na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Radiwello Mwampashi, wakati akitoa salama za chama katika maadhimisho hayo.