BoT Kuzindua Mfumo wa kidigitali wa utatuzi wa malalamiko Januari 2025

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imetangaza mipango ya kuzindua Mfumo wa Kidigitali wa Utatuzi wa Malalamiko ya Wananchi (FCRS) ifikapo Januari 2025. Mfumo huo utamwezesha mtumiaji wa huduma za kifedha kuwasilisha malalamiko yake kupitia mtandao, hatua inayolenga kuboresha upatikanaji wa haki kwa haraka na kwa urahisi.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Desemba 10, 2024, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma Jumuishi za Fedha wa BoT, Nangi Massawe, alisema mfumo huo umekamilika, na kwa sasa taasisi za kifedha zinaelimishwa jinsi ya kuutumia kabla ya uzinduzi rasmi.

“Mfumo umetengenezwa na kukamilika. Tunatoa elimu kwa taasisi za kifedha ili zijue jinsi ya kuutumia kabla ya Januari 2025. Lengo letu ni kuhakikisha mteja anawasilisha malalamiko kwa haraka na kupata suluhisho kwa wakati,” alisema Massawe.

Aliongeza kuwa mfumo huo ni sehemu ya juhudi za BoT za kuimarisha ushirikishwaji wa kifedha na kujenga imani kwa watumiaji wa huduma za kifedha nchini.

Dk. Hadija Kishimba, Kaimu Meneja wa Kumlinda Mtumiaji wa Huduma za Kifedha, alisema mfumo wa FCRS unalenga kurahisisha utatuzi wa changamoto kwa wateja moja kwa moja kupitia mtandao.

“Mfumo huu utasaidia mteja kuwasilisha malalamiko akiwa mahali popote bila kulazimika kutembelea tawi la benki. Hii ni hatua kubwa katika kuhakikisha huduma za kifedha zinapatikana kwa uwazi na kwa haraka,” alisema.

Aliongeza kuwa kwa sasa malalamiko yanapokelewa kupitia njia za kawaida kama barua pepe, simu, na matawi ya benki, lakini mfumo wa kidigitali utaharakisha zaidi utatuzi wa changamoto hizo.

Manufaa ya Mfumo Mpya

Mfumo wa FCRS utahakikisha:

  1. Upatikanaji wa haki kwa haraka – Malalamiko yatawasilishwa moja kwa moja kwa BoT na kushughulikiwa mara moja.
  2. Kupunguza changamoto za wizi wa fedha – Wateja watapata suluhisho kwa malalamiko kama vile wizi wa fedha kupitia ATM au kadi za benki.
  3. Uimarishaji wa elimu kwa wateja – Mfumo utahimiza uelewa wa usalama wa kifedha, ikiwa ni pamoja na kuepuka kushiriki namba za siri.
Mtoa huduma za fedha wa benki ya CRDB, Lugano Mponjoli, alisema mfumo huo utaleta mabadiliko makubwa katika sekta ya fedha kwa kutatua malalamiko ya wateja kwa haraka.

“Mfumo huu utasaidia sana, hasa katika kushughulikia changamoto kama wizi wa fedha kwa njia za kidigitali. Tunatarajia mabadiliko chanya,” alisema Mponjoli.

Kwa upande wake, Meneja wa Huduma kwa Wateja wa benki ya NMB, Elizabeth Mhina, alisema mfumo huo utarahisisha kazi na kuboresha huduma kwa wateja.

“Yapo malalamiko mengi tunayopokea kila siku, hasa kuhusu wizi wa fedha kupitia ATM. Mfumo huu utapunguza changamoto hizo na kuwasaidia wateja kupata suluhisho kwa haraka,” alisema Mhina.

BoT inatarajia kuwa mfumo huu wa kidigitali utasaidia kuimarisha imani ya wananchi katika huduma za kifedha rasmi na kuchangia ukuaji wa ushirikishwaji wa kifedha nchini.

Related Posts