Dar es Salaam. Tanzania inahitaji viongozi waliobobea, wasimamizi na maofisa wa kuthibiti ubora wa shule ili kuhakikisha matumizi sahihi ya rasilimali chache zilizopo na utoaji wa elimu bora kama inavyotarajiwa, wadau wameeleza.
Kauli hiyo inakuja wakati ambapo sekta ya elimu nchini inakabiliwa na mageuzi makubwa, ikiwemo kuanza kutumika kwa mtalaa mpya, mabadiliko ya sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014 (Toleo la mwaka 2023), na marekebisho ya sheria za elimu.
Ushirikiano kati ya Taasisi ya Aga Khan ya Maendeleo ya Elimu, Afrika Mashariki (AKU-IED, EA) na Wakala wa Maendeleo ya Usimamizi wa Elimu (ADEM) ni jibu mwafaka kwa changamoto zilizopo.
Hilo linatokana na taasisi hizo kuweka mpango thabiti wa kuwezesha Watanzania kupata ujuzi muhimu katika uongozi wa elimu, usimamizi na uthibiti ubora wa shule.
Mwaka 2024, jumla ya wahitimu 998 walimaliza programu mbalimbali za elimu kupitia ADEM, iliyopo Bagamoyo mkoani Pwani wakiwemo 47 kutoka AKU-IED, EA.
Asia Athuman ni mmoja wa wahitimu hao, aliyepata Stashahada (Diploma) ya Usimamizi na Utawala wa Elimu (DEMA).
Akizungumza leo Jumanne, Desemba 10, 2024 kuhusu mafunzo yake amesema: “Programu hii imenipa nyenzo za kusimamia rasilimali kwa ufanisi na pia kuwasaidia walimu na wanafunzi. Niko tayari kuleta ubunifu shuleni na kuhakikisha viwango vya elimu vinapanda.”
Mhitimu mwingine, Tegemea Tweve aliyesomea Cheti cha Uongozi, Usimamizi na Utawala (CELMA) kutoka ADEM, amesema mafunzo yake yalilenga changamoto za vitendo.
“Wakufunzi wetu walisisitiza hali halisi ya maisha, na kutusaidia kuelewa jinsi ya kukabiliana na masuala kama motisha kwa wafanyakazi na utekelezaji wa sera. Ujuzi huu ni muhimu wakati ambapo shule zinakabiliwa na mahitaji makubwa,” ameeleza.
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Charles Mahela amesisitiza ushirikiano wa AKU-IED na ADEM ni ufunguo wa kufanikisha lengo hilo.
“Kwa kufundisha maofisa zaidi wa kuhakikisha ubora wa shule, tunaweza kuhakikisha shule zinakidhi viwango vilivyowekwa. Ushirikiano huu ni muhimu tunaposhughulikia mahitaji ya sasa ya sekta ya elimu,” amesema Dk Mahela.
Amidi wa AKU-IED, EA, Dk Jane Rarieya, ameeleza uwezo mkubwa wa kubadilisha hali iliyopo kupitia ushirikiano wao na ADEM.
“Uongozi wa mafundisho na ufundishaji ni kiini cha mafunzo bora ya elimu. Viongozi wanapaswa kwenda zaidi ya kusimamia rasilimali; wanapaswa kuwa vinara wa kufundisha na kujifunza,” amesema katika hotuba iliyotolewa na Profesa Fortidas Bakuza wa AKU-IED, EA.
Dk Rarieya, pia, amesisitiza umuhimu wa usawa wa kijinsia katika uongozi, akisema: “Usawa wa kijinsia siyo tu kuhusu idadi, bali ni juu ya kuunda mazingira ambayo kila mtu anajisikia kuthaminiwa na kuwezeshwa.”
Profesa Bakuza ameongeza kuwa AKU-IED inaendelea kujitolea kutoa fursa za mafunzo ya juu kwa Watanzania.
“Tunawaalika Watanzania zaidi kujiunga na programu zetu za uzamili ili kuimarisha uongozi na usimamizi wa elimu nchini,” amesema.
Muhitimu wa ADEM, Halima Said, aliyemaliza Diploma ya Uhakikisho wa Ubora wa Shule (DSQA), anaamini mafunzo hayo yameandaa uwezo wake wa kuziba mapengo muhimu.
“Kuna hitaji halisi la maofisa wa uhakikisho wa ubora waliohitimu katika shule zetu. Mafunzo yangu yamenipa uwezo wa kutathmini na kuhakikisha shule zinakidhi viwango vilivyowekwa,” amesema.
Wataalamu wanakubaliana kuboresha uongozi wa elimu na uhakikisho wa ubora ni muhimu ili kufanikisha malengo ya Dira ya Maendeleo ya 2025 ya Tanzania. Kwa rasilimali chache zilizopo, nchi inahitaji wataalamu wenye ujuzi wa kusimamia mifumo ya elimu kwa ufanisi huku wakiongoza ubunifu.
“Ushirikiano kati ya AKU-IED na ADEM umekuja wakati mwafaka,” alisema mshauri wa elimu Dk Benjamin Msuya.
“Ushirikiano huu hauimarishi tu uwezo wa wasimamizi wa elimu bali pia unahakikisha mageuzi yanayoendelea yanatekelezwa kwa ufanisi,” ameongeza.