Shinyanga. Mkazi wa Mtaa Dome Kata ya Ndembezi Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga mkoani humo, Leah George (40) anadaiwa kusombwa na maji alipokuwa akivuka mto baada ya mvua kunyesha.
Tukio hilo limetokea jana Desemba 09, 2024 muda wa saa 12 jioni katika daraja la mto Mumbu baada ya mvua kubwa na kusababisha maji kujaa.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Ofisa Oparesheni Jeshi la Zima Moto na Uokoaji Mkoa huo, Edward Selemani amesema baada ya kupokea taarifa hizo hatua za kuutafuta mwili huo zinaendelea.
“Jana Desemba 9, 2024 saa mbili usiku tulipokea taarifa ya mtu kusombwa maji, tukafika eneo la tukio lakini kutokana na muda ulikuwa usiku hatukuweza kufanya lolote,” amesema.
Selemani ameongeza kuwa “Leo saa 12 tukaanza tena kuutafuta mwili kuanzia sehemu alipozamia hadi maeneo ya Manonga ambapo ndio mkondo wa maji unapoelekea lakini hatujafanikiwa, tutaendelea na shughuli hiyo baadaye maji ya mto yakipungua” amesema Selemani Akisimulia namna alivyopokea taarifa hizo Mama Mzazi wa Leah, Rachel Jeremiah amesema tangu jana usiku simu yake baada ya kupigwa haikupatikana jambo ambalo sio la kawaida kwake, ambapo leo alipigiwa simu na kuambiwa alisombwa na maji.
“Niliondoka asubuhi nikawaacha wamelala nikaenda kwenye kibarua changu, nilivyorudi sikumkuta nikajua labda ameenda matembezi nimekaa mpaka saa 2 usiku nikaanza kupiga simu haipatikani, nikajiuliza mbona leo hapatikani wakati siku zote nikipiga anapokea, nikafanya hivyo mpaka saa 3 hapatikani sisi tukalala” amesema.
Ameongeza kuwa hata baada ya kuamka leo asubuhi na kujaribu kumuuliza binti yake alijibiwa hajarudi jambo ambalo hakulitilia maanani na kuamua kwenda kwenye vibarua akiamini amelala kwa marafiki zake.
“Nilipokuwa kazini nikapigiwa simu nije kuna tukio nilipouliza tukio gani na wao wakaniuliza Nkwemba (Leah) amelala nyumbani? Nikawaambia hajalala nikaambiwa alitumbukia mtoni alikuwa anatokea mtaa wa Tambuka Reli” amesema.
Jirani wa familia hiyo, Janeth Suleimani amesema baadhi ya wananchi walisikia kelele zake akiomba msaada wakati akisombwa na maji.
“Mimi niliamka asubuhi na majukumu yangu sikuelewa kinachoendelea baada ya kurudi nikakuta watu wamejaa wanasema huyu mama mwanaye ametumbukia kwenye maji, maana alikuwa anapiga kelele nisaidieni! nisaidieni! lakini maji yakawa yamemzidia,” amesema Janeth.