Maisha baada ya uraibu: Safari ya muhitimu UDOM kurudisha uaminifu

Dar es Salaam. Katika pembe tulivu ya Jiji la Dar es Salaam, Almasi Rajabu Almasi, mwenye umri wa miaka 46 na mmoja wa wanafunzi wa kundi la kwanza wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), anaketi kwenye benchi la zamani, akisimulia hadithi ya maisha yake yaliyoingia katika giza, yakiwa yametekwa na mtego usioachilia wa uraibu wa heroini.

Almasi alizaliwa Mwanza lakini akakulia Dar es Salaam. Safari yake ilianza katika familia yenye watoto watatu, akiwa mwanafunzi mahiri ambaye umahiri wake wa kitaaluma ulificha pengo lililokuwa likikua ndani yake.

“Nilianza kuvuta bangi nikiwa darasa la nne pale Shule ya Msingi Mapambano,” anasema.

Ilipofika mwaka 1998, akiwa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari St Antony, tayari alikuwa ameanza kujaribu matumizi ya dawa za kulevya aina ya heroini. Alijikuta akifuata njia aliyoonyeshwa na marafiki waliomshawishi kutumia dawa hizo hatari.

“Rafiki yangu mmoja alitumia sare za shule kusafirisha na kuuza dawa hizi kwa watumiaji mitaani. Awali, heroini ilitolewa bure,” anasimulia.

Kulingana na anavyosimulia, hii ilikuwa mbinu iliyopangwa na wauzaji kuwavutia watumiaji wapya katikati ya miaka ya 1990.

Jaribio la kwanza liligeuka kuwa utegemezi na maisha ya Almasi yakabadilika kabisa.

Licha ya akili yake kubwa na mafanikio ya kitaaluma akiwa mara kwa mara miongoni mwa wanafunzi watano bora darasani, uraibu ulianza kumtawala.

“Baada ya kumaliza kidato cha nne, nilianza kutumia heroini mara kwa mara. Marafiki walileta dawa na sikuweza kuacha. Ilionekana kama ndiyo kitu pekee nilichohitaji,” anasema.

Anabainisha kuwa siku hizo familia yake ilifurahia alipoacha pombe, bila kujua kuwa alikuwa ameibadilisha na kuanza kutumia heroini.

Ndoto ya kutumia kwa kiasi ilitoweka haraka uraibu ulipozidi kuwa mkubwa. Uraibu ulileta mtikisiko mkubwa katika maisha ya familia ya Almasi.

“Niliwaibia wazazi na ndugu zangu. Iliwaumiza sana, na mwishowe, waliniona kama adui,” anakiri.

Mwaka 2010, baada ya kuhitimu Shahada ya Elimu katika Chuo Kikuu cha Dodoma, Almasi alilazwa katika Hospitali ya Amana kwa ajili ya kuondoa sumu mwilini.

“Wazazi wangu waliniunga mkono wakati huo, lakini niliporudia kutumia, walikata tamaa. Kurudi nyumbani hakukuwa chaguo tena.”

Uraibu wake ulivunja uhusiano wa familia, hata juhudi za kupatanisha zilijaa shaka.

“Walikuwa wakibeba funguo za vyumba vyao, wakiogopa ningeiba tena,” anasema kwa sauti iliyojaa majuto.

Gharama ya uraibu kwa Almasi ilikuwa kubwa mno. Aliuza viwanja viwili na mali nyingine nyingi ili kumudu gharama za matumizi ya dawa.

Uhusiano pia ulivunjika, ukiwamo na mwanamke mmoja aliyewahi kujaribu kumsaidia lakini hatimaye akachoka, akishindwa kuona mustakabali mzuri pamoja.

“Alivumilia mengi, lakini nilipoanza kuuza hata vitu nilivyomnunulia, aliachana nami,” anakumbuka.

Licha ya kulazwa mara kadhaa katika nyumba za kurekebisha tabia Dar es Salaam na Zanzibar, mzunguko wa kupona na kurudia dawa uliendelea.

“Nimepoteza mengi kwa sababu ya uraibu,” anasema. “Kama ningekuwa na uwezo wa kurudi nyuma, nisingegusa kamwe dawa za kulevya.”

Leo, Almasi yupo kwenye kipindi cha mpito. Bila kipato cha kudumu, hufanya kazi za muda ili kuishi.

“Husafisha sehemu mbalimbali pale ninapopata nafasi, lakini mara nyingi nalala nje,” anasema.

Kwa maoni yake, mitaa ni bora zaidi kuliko kurudi nyumbani ambako uaminifu ulishaanguka.

“Si rahisi kujenga upya uhusiano. Familia yangu inaogopa kuwa ninaweza kuiba tena,” anasema.

Almasi ana ujumbe kwa jamii na serikali

“Watu wanaopambana na uraibu wanahitaji msaada wa kujumuika tena katika jamii. Serikali inapaswa kuzingatia kupunguza gharama za vituo vya kurekebisha tabia

Sh2.4 milioni si rafiki kwa wengi,” anashauri.

Anapendekeza pia kuwapo kwa programu za kifedha kuwasaidia waraibu waliopona kujijenga upya.

“Mikopo au ruzuku inaweza kutusaidia kuanzisha biashara ndogo na kuwa huru kifedha. Bado nina matumaini ya maisha bora. Lakini, tunahitaji watu watuone kama binadamu, wenye uwezo wa kubadilika.”

Safari yake inaendelea, hatua moja baada ya nyingine, kuelekea maisha anayoyatamani, maisha ya uaminifu, utulivu na heshima.

Related Posts