KOCHA wa Simba, Fadlu Davids ameweka wazi hesabu zake kimbinu katika mchezo ujao wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya CS Sfaxien ya Tunisia kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa utakuwa tofauti na ilivyokuwa kule Algeria ambako walipoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya CS Constantine.
Kwa nini? Msauzi huyo, alisema anahitaji kuishambulia zaidi CS Sfaxien huku akidumisha nidhamu ya kulinda kwa wachezaji wake walioonekana kujisahau mwanzoni kipindi cha pili kule Algeria kiasi cha kuruhusu mabao mawili ndani ya dakika tano jambo ambalo hakulitegemea.
Fadlu anahitaji kuweka mkazo katika hilo ili kuwa salama wakati wakisaka ushindi wao wa pili kwenye michauno hiyo ya CAF.
Simba ambayo ipo nafasi ya pili sawa na Onze Bravos Do Maquis ya Angola katika msimamo wa kundi A, wanahitaji pointi tatu za kwa Mkapa ili kuweka sawa hesabu zao kabla ya kwenda Tunisia kumalizana nao.
Katika mchezo uliopita, Fadlu alitumia zaidi ya wachezaji sita wenye uwezo mkubwa wa kulinda huku akionekana kushambulia kimkakati mpango ambao ulifanya vizuri ndani ya dakika 45 za kipindi cha kwanza.
Lakini nidhamu ya kulinda ilipungua jambo ambalo liliwafanya kupoteza mchezo huo, “Kwa kweli, kucheza nyumbani ni faida kubwa kwetu. Tutakuwa na programu za mazoezi kwa siku chache zilizopo mbele yetu ili kuwa tayari kwa mchezo huu. Nitahakikisha mpango wetu wa kimbinu ni tofauti na ule tulioutumia kule Algeria.”
“Nidhamu ya kulinda itakuwa sehemu muhimu ya mchezo wetu, lakini tunahitaji kuwa na mashambulizi ya haraka na kuzuia makosa tuliyofanya kwenye mchezo wa awali,” alisema Fadlu.
CS Sfaxien ndio wanaoburuza mkia katika msimamo wa kundi A ambao unaongozwa na CS Constantine wenye pointi sita, Watunisia hao bado hawajapata pointi hata moja.
“Lengo ni kuhakikisha kuwa tunapata matokeo mazuri na kuweka hesabu zetu sawa katika michuano hii ya CAF,” aliongeza kocha huyo.
Takwimu zinaonyesha CS Sfaxien imeshinda mara mbili tu na ni dhidi ya Soliman (4-1) na (US Tataouine) katika michezo minane iliyopita ya mashindano yote, wamefungwa mara mbili katika kombe la shirikisho dhidi ya CS Constantine (1-0) na Bravos (3-2), huku wakitoa sare nne mfululizo katika ligi yao ya ndani, dhidi ya Club Africain (0-0), Zarzis (1-1), Olympique Beja (0-0) na Monastir (1-1). Hii itakuwa mara ya kwanza kwa klabu hizi mbili kukutana.
Kuhusu wapinzani hao, Fadlu alisema; “Tulifanya tathimini ya jumla kuhusu wapinzani wote lakini tulitoa uzito wa maandalizi yetu kulingana na aina ya mpinzani tunayekabiliana naye, natoa wito kwa mashabiki wetu kutuunga mkono, wanatakiwa kusahau kilichotokea Algeria.”
Wakati huku Tanzania Bara Simba ikishika nafasi ya pili katika ligi ikiwa na pointi 28 katika michezo 11, wamefunga mabao 22 na kuruhusu matatu, wapinzani wao, CS Sfaxien ipo nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi ya Tunisia ikiwa na pointi 17 baada ya mechi 10, wamefunga mabao 13 na kuruhusu sita.