Siri kuangushwa kwa utawala wa Rais Assad Syria

Ni tukio la kihistoria kwa wananchi wa Syria kushuhudia Rais wa nchi hiyo, Bashar al-Assad akiikimbia nchi hiyo baada ya waasi wa Syria kuchukua udhibiti wa mji mkuu wa nchi hiyo.

Kumekuwa na sherehe mitaani katika mji wa Damascus, mji mkuu wa Syria, kufuatia habari kwamba Rais Assad ameondoka nchini humo akikimbilia Moscow, Russia akipewa hifadhi na swahiba wake, Rais Vladmir Putin.

Familia ya Assad imeliongoza taifa hilo kwa zaidi ya miongo mitano, huku serikali zilizoongozwa na wanafamilia hiyo zikitawaliwa na rushwa na ukandamizaji wa demokrasia na matumizi ya mabavu katika uendeshaji wake.

Tangu mwaka 2011, vita vya wenyewe kwa wenyewe vimekuwa vikiendelea nchini Syria, vikundi tofauti vikigombania kutwaa madaraka ya nchi hiyo.

Maelfu ya watu wamepoteza maisha na mamilioni wamekimbia nchi ili kuokoa maisha yao.

Waziri Mkuu wa Uingereza, Sir Keir Starmer alisema: “Wananchi wa Syria wamepitia mateso makubwa chini ya utawala wa kikatili wa Assad kwa muda mrefu sana na tunafurahia kuondoka kwake.”

Lakini nini kimejiri nchini Syria katika siku chache zilizopita?

Novemba 27, 2024, mojawapo ya vikundi vya waasi—Hayat Tahrir al-Sham (HTS)—kwa msaada wa vikundi vingine vya waasi, kilianzisha shambulizi la kushtukiza dhidi ya vikosi vya kijeshi vinavyounga mkono serikali.

Baada ya mapigano ya siku 12, waasi walitwaa na kuidhibiti Aleppo, ambao ni mji wa pili kwa ukubwa nchini Syria, kisha Hama na Homs, mji wa tatu kwa ukubwa nchini humo.

Jumapili, Desemba 8, waasi wanaoongozwa na HTS walisema wameingia katika mji mkuu wa Damascus na kuwaachilia huru watu waliokuwa katika gereza hatari la kijeshi nchini humo, Saydnaya.

Chini ya saa mbili baadaye, waasi walitangaza kuwa “dikteta Bashar al-Assad amekimbia” baada ya habari kuenea kwamba Rais Assad na maofisa wake wakuu wameondoka nchini kuelekea Russia.

Waziri Mkuu wa Syria, Mohammed al-Jalali, alisema katika video kuwa yuko tayari kushirikiana na uongozi wowote utakaochaguliwa na wananchi wa Syria.

Lakini nini kilichochochea hadi vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria vikaanza? Familia ya Assad imekuwa ikitawala Syria kwa zaidi ya miaka 53.

Bashar al-Assad, alichukua urais baada ya kifo cha baba yake, Hafez, mwaka 2000, ambaye alikuwa rais wa nchi hiyo tangu mwaka 1971.

Familia ya Assad ilijulikana kwa kuwa watawala wa kiimla waliokuwa wakitoa adhabu kali kwa watu waliopingana nao.

Wakati huo, wananchi wa Syria walikuwa hawaridhishwi na hali ya ukosefu wa ajira, tabia mbaya za maofisa wa serikali na kuminywa kwa uhuru wa kisiasa chini ya utawala wa Bashar al-Assad.

Hata hivyo, tukio lililosababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe lilianza mwaka 2011.

Mwaka huo, katika mji wa Deraa, wananchi waliamua kuandamana baada ya wanafunzi 15 wa shule 15 kukamatwa na kuteswa kwa kuandika kwenye ukuta maandishi ya kupinga serikali.

Awali, maandamano yalikuwa ya amani, yakidai watoto hao waachiwe, demokrasia iruhusiwe na kuwe na uhuru zaidi kwa wananchi wa nchi hiyo.

Serikali ilijibu kwa hasira na Machi 18, 2011, jeshi liliwafyatulia risasi waandamanaji na kuua watu wanne. Siku iliyofuata, waliwafyatulia risasi waombolezaji waliokuwa kwenye maziko ya waathirika na kuua mtu mwingine.

Watu walishangazwa na kukasirishwa na kilichotokea na hivi karibuni maandamano yalianza kuenea katika maeneo mengine ya nchi.

Mwanzoni, waandamanaji walitaka tu demokrasia na uhuru zaidi, lakini baada ya vikosi vya serikali kufyatua risasi kwa waandamanaji waliokuwa katika maandamano ya amani, watu walianza kumtaka Rais Bashar al-Assad ajiuzulu.

Hata hivyo alikataa, jambo lililowafanya waandamanaji kukasirika zaidi.

Rais Assad bado alikuwa na wafuasi wengi nchini Syria waliomuunga mkono yeye na serikali yake, hivyo wakaanza kupigana dhidi ya watu waliokuwa kinyume cha serikali.

Vikundi vingine, ikiwa ni pamoja na makundi ya Kiislamu yenye msimamo mkali, pia vilijiunga katika mapambano dhidi ya Rais Assad na mara nyingine walipigana wenyewe kwa wenyewe.

Mapigano hayo yaliendelea kwa zaidi ya miaka 12, yakiua maelfu ya watu na kusababisha mamilioni kukimbia makazi yao.

Hali hiyo ilizidi kuwa ngumu kwa sababu nchi nyingine zilihusika kwenye mgogoro huo.

Wanaomuunga mkono Rais Assad walikuwa ni pamoja na Russia na Iran wakati Marekani, Uturuki na Saudi Arabia ziliunga mkono vikundi tofauti vya waasi.

Uingereza, Ufaransa, na nchi nyingine za magharibi pia zilitoa msaada wa aina mbalimbali kwa kile walichokiita waasi “wastani”.

Hayat Tahrir al-Sham (HTS) ni kikundi cha wanamgambo wa Kiislamu kinachoongozwa na Abu Mohammed al-Jawlani, ambaye sasa ameanza kutumia jina lake halisi: Ahmed al-Sharaa.

Nchini Uingereza na Marekani, kikundi hiki kwa sasa kimeorodheshwa kama shirika la kigaidi, kutokana na uhusiano wake wa zamani na kundi la kigaidi la al-Qaeda ambao wanadaiwa walishiriki katika shambulio la Septemba 11 nchini Marekani, mwaka 2001.

Hata hivyo, HTS walisema wamekatisha uhusiano wao na al-Qaeda mwaka 2016.

Serikali ya Uingereza imesema sasa itafikiria upya iwapo HTS inapaswa kuendelea kuorodheshwa kama shirika la kigaidi chini ya Sheria ya Ugaidi ya mwaka 2000.

Pat McFadden, Waziri wa Baraza la Mawaziri la Uingereza, alisema: “Ndiyo, hilo lazima liangaliwe. Wameorodheshwa kwa muda mrefu sasa…Kiongozi wa kikundi hicho amejiweka mbali na baadhi ya mambo yaliyosemwa huko nyuma.

“Anazungumza baadhi ya mambo sahihi kuhusu ulinzi wa wachache, na haki za watu. Tutalichunguza hilo katika siku zijazo.”

Viongozi duniani wanasemaje?

Waziri Mkuu wa Uingereza, Sir Keir Starmer, alisema: “Wananchi wa Syria wamepitia mateso makubwa chini ya utawala wa kikatili wa Assad kwa muda mrefu sana, na tunakaribisha kuondoka kwake.”

Hata hivyo, alisema pia bado ni mapema kuamua jinsi Uingereza itakavyoshirikiana na wale waliomwondoa madarakani Rais Assad.

Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya (EU), Kaja Kallas alielezea kuanguka kwa Assad kama “maendeleo mazuri yaliyosubiriwa kwa muda mrefu.”

Ikulu ya Marekani ilisema Rais Joe Biden na timu yake walikuwa wakifuatilia kwa karibu matukio ya ajabu nchini Syria na wakiwa na mawasiliano ya mara kwa mara na washirika wa kikanda.

Uturuki ilisema Syria sasa ipo katika hatua ambapo wananchi wa Syria wataamua mustakabali wa nchi yao wenyewe.

Waziri wa Mambo ya Nje, Hakan Fidan, alisema serikali mpya “lazima iundwe kwa utaratibu mzuri” na akatahadharisha kuwa “kanuni ya ujumuishi haipaswi kamwe kupuuzwa.”

Iran ilielezea matumaini ya “kumalizika haraka kwa migogoro ya kijeshi, kuzuia matukio ya kigaidi na kuanza kwa mazungumzo ya kitaifa” yanayojumuisha jamii zote za Syria.

Russia ilisema ilikuwa “ikifuatilia kwa wasiwasi mkubwa matukio ya kushtua nchini Syria.”

Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia ilitoa wito kwa “pande zote zinazohusika” kwenye mgogoro wa Syria “kuachana na matumizi ya vurugu na kutatua masuala yote ya utawala kupitia njia za kisiasa.”

Pia, ilisema kwamba kambi za kijeshi za Russia nchini Syria ziko katika tahadhari ya hali ya juu, ingawa hakuna tishio kubwa kwa usalama wao.

Bashar al-Assad alimrithi baba yake, Hafez al-Assad, kama Rais wa Syria mwaka 2000 na kuhudumu hadi 2024 alipong’olewa madarakani baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka 13.

Hafez al-Assad alifariki dunia Juni 10, 2000. Saa chache baada ya kifo chake, Bunge la kitaifa liliidhinisha marekebisho ya katiba yaliyoshusha umri wa chini wa kugombea urais kutoka miaka 40 hadi 34, umri wa Bashar al-Assad wakati huo.

Juni 18, 2000, Assad aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa chama tawala cha Ba’ath, na siku mbili baadaye, mkutano wa chama ulimteua kama mgombea wa urais; uteuzi huo uliidhinishwa na bunge la kitaifa.

Julai 10, Assad alichaguliwa kwa muhula wa miaka saba bila kupingwa, lakini sasa amelazimika kukimbia nchi.

Related Posts