NIKWAMBIE MAMA: ‘Yaliyopita si ndwele’ hadi lini?

Hatimaye tumeuvuka uchaguzi wa serikali za mitaa kwa mbinde kwelikweli. Wagombea wa vyama vya pande zote wamebaki kama waliotumia mbinu za kitaalamu kupunguza miili na uzito, kumbe wapi! Wamekondeshwa na hekaheka za kuumiza vichwa na misuli zilizodumu chini ya mwezi mmoja tu. Ilikuwa ni pepo na jehanamu kulingana na tofauti ya wagombea; wengine waliona utamu na wengine uchungu.

Vituko vyote hivi ni katika uchaguzi wa mtaani. Najiuliza hapo mwakani kwenye uchaguzi wa mjengoni iwapo tutapata fursa ya kupumua.

Kama unazimia kwenye geti la Horombo wakati wa kupanda Mlima Kilimanjaro, unategemea kufika vipi kwenye kilele cha Uhuru?

Au unapigwa katika raundi ya kwanza kwenye vitasa vya uzito wa unyoya, unapata wapi jeuri ya kufika raundi ya kumi dhidi ya bingwa wa uzito wa juu?

Lakini kama kawaida tutakumbushwa “yaliyopita si ndwele” ili kuachana na yanayopita na kuganga yatakayokuja mbele. Mtindo huu umekuwa ni kawaida yetu kwa maana ukitaka kumficha jambo Mswahili, mwandikie kwenye shajara. Kila msimu wa masika atasema “Hakujatokea mvua kama hii” kwa kuwa hana kumbukumbu ya masika yaliyopita. Hivyo tutayaona makosa kama yaliyotendwa kwa mara ya kwanza.

Matatizo mengine ni aibu hata kuyasema. Kwenye shughuli kubwa kama uchaguzi, ni ajabu tume kukosa muda, vifaa au utaalamu kiasi cha kubandika karatasi za majina ya wapigakura zilizoandikwa kwa mkono na bila mpangilio wa alfabeti. Hilo limewatatiza wenye haki yao ambao baadhi walifika alfajiri na kutafuta majina yao hadi saa tano kabla ya kukata tamaa na kuondoka.

Tujiulize maswali rahisi: Kwa nini barua ya maombi ya kazi ichapwe kwa mwandiko wa Times New Roman, ukubwa uanzie alama 12 na rangi iwe nyeusi? Ni kwa sababu kila mmoja ana mwandiko wake.

Mikono mingine inaweza kuleta mbwembwe kiasi mtu akiandika herufi “c” inasomeka “e”. Au kalamu yake ikagoma kumalizia kidoti cha juu cha “i” na kusababisha isomeke “l”.

Kilichotokea kilikuwa sawa na kumwaga gunia la mbigiri kwenye uwanja wa chandimu. Mkicheza peku mtajichoma kwenye uwanja na wageni waalikwa, ndicho kilichotokea kwenye uchaguzi huu wa serikali za mitaa.

Kambi ya upinzani imelia, lakini tumeona wahafidhina wa chama tawala wakisikitishwa na mwenendo mzima wa zoezi hilo lililo na umuhimu wa kipekee katika demokrasia ya nchi.

Waziri Mkuu mstaafu na Mwanasheria nguli nchini, Jaji Joseph Warioba amesema licha ya jitihada kubwa kufanyika hadi kupitishwa sheria za uchaguzi ili yasijirudie yaliyojitokeza katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2019, mambo yale yale yamejitokeza kwenye uchaguzi wa Novemba 27, 2024.

Warioba alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari na wahariri juu ya kile alichokiona kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu.

Jaji Warioba hakuridhishwa na uenguaji wa wagombea wa upande mmoja. Alisema haiwezekani mpaka sasa tunateswa na kura bandia, na akafafanua kuwa zamani wagombea ndio walioziandaa wakati hivi sasa kura bandia zinaandaliwa na wasimamizi wa uchaguzi.

Jambo hili linaitia doa Serikali na kuiweka katika lawama, kwani inapaswa kusimamia vyama vyote vilivyosajiliwa nayo.

Katika msimu huu wa Uchaguzi Mkuu unaoanzwa na huu wa Serikali za Mitaa, Tume ya Uchaguzi ilifanyiwa marekebisho ya kiutawala na kuitwa Tume Huru ya Uchaguzi.

Lakini jambo la ajabu ilikuwa kama isiyojua kazi yake sawasawa. Ilikuwa ikikiuka baadhi ya kanuni kwa makusudi, na kuwaelekeza waathirika kwenda kukata rufaa katika muda mfupi sana uliosalia.

Lengo la kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi ni kuyafuta mapungufu yaliyowahi kujitokeza chini ya usimamizi wa Tume ya Uchaguzi iliyokuwepo.

Tulitegemea malalamiko yangepungua, lakini hivi karibuni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) alisema rufaa 5,589 (tu) kati ya 16,309 zilizokatwa na wagombea ndizo zilizokubaliwa kusikilizwa. Sasa hapo ni padogo?

Kwangu matatizo ya uchaguzi ni sawa na moto wa nyikani.

Huanzishwa na njiti moja tu lakini huteketeza miti mikubwa, wanyama wakali na kila kilichomo. Matatizo ya uchaguzi wa mwaka 2000 yaliyotokea Zanzibar yalianzwa na mambo madogo kama haya yanayotokea sasa, lakini yakasababisha maandamano, vurugu kubwa, majeruhi na vifo.

Mwaka huu vyama havilaumiani, bali vyote vinailaumu Serikali. Niliwahi kuona filamu ya kigeni, ambayo ilimuonesha bingwa wa ngumi za jela akimwadhibu chawa aliyemsaidia kupata ushindi.

Bila shaka chawa huyo alikuwa akijihakikishia nafasi yake, lakini bingwa alikasirika, kwani hakutoa maagizo hayo na alikuwa na uhakika wa kushinda pasipo rafu kuchezeka.

Hivyo Serikali inapaswa kuangalia upya haya yanayojitokeza. Tunaingia kwenye kipindi kigumu kilichoyasambaratisha baadhi ya mataifa baada ya figisu za chaguzi.

Mambo ya “yaliyopita si ndwele” nayo yalishapitwa na wakati, tuyagange pamoja na haya tuliyonayo sasa.

Related Posts