Benki ya Dunia yakoshwa utendaji vituo jumuishi, kuongeza vingine tisa

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma amesema Benki ya Dunia imekubali kujenga vituo jumuishi tisa vya masuala ya familia kutokana na mafanikio yaliyopatikana katika vituo vilivyopo kikiwemo cha Temeke ambacho kimefanya vizuri zaidi.

Ametoa kauli hiyo Desemba 10,2024 wakati akifungua kongamano la miaka mitatu ya Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke pamoja na uzinduzi wa ripoti ya utendaji kazi wa kituo hicho.

Amesema Mahakama za Afrika zinaweza kupata fedha za Benki ya Dunia na kuboresha mifumo ya utoaji haki na kwamba kufanikiwa kwa Tanzania kutafungua njia kwa mahakama zingine katika Bara za Afrika Serikali zao ziweze kuwatafutia fedha za kuboresha mifumo ya utoaji haki.

“Kituo Jumuishi cha Temeke na vituo jumuishi vingine sita vimefanya vizuri sana kiasi kwamba Benki ya Dunia imekubali na inajenga vituo jumuishi vingine tisa, walipokuja kutukagua wanaona faida kubwa.

“Mheshimiwa rais wakati anazinduia vituo sita alisema kwamba Serikali inafadhili mahakama kwa sababu inatekeleza dira ya taifa ya maendeleo, shughuli za kituo jumuishi ni sehemu ya kuifikisha Tanzania katika matarajio ya maendeleo ya taifa 2025,” amesema Profesa Juma.

Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, Mwanabaraka Mnyukwa, akizungumza wakati wa kongamano la miaka mitatu ya kituo hicho.

Amesema vituo tisa vitajengwa katika baadhi ya Mikoa ya Songwe, Ruvuma, Njombe, Singida, Lindi na Pemba na hadi kufikia mwisho wa mwaka ujao hakutakuwa na mkoa ambao hauna kituo cha mahakama.

Aidha amewataka Watanzania ambao wana mashauri ya mirathi katika mahakama mbalimbali nchini kutoa taarifa kama wakiona hayaendi vizuri.

Amesema kati ya mwaka 2021 hadi 2024 Mahakama imelipa fedha za mirathi Sh bilioni 101.8 na kwamba kituo hicho kimeweka mifumo kupunguza ushawishi wa kudokoa fedha na kuhakikisha zinawafikia walengwa.

“Wasimamizi wa mirathi unapopewa jukumu la kusimamia mirathi ni utawala bora, unapogeuza mali ya mirathi kama ni yako unakuwa umevunja utawala bora,” amesema.

Naye Jaji Mfawidhi wa Kituo hicho, Mwanabaraka Mnyukwa, amesema iwapo usuluhishi utaruhusiwa katika kushughulikia mashauri ya mirathi utachagiza wananchi kupata haki zao kwa wakati bila kuacha chuki kwa wanafamilia na kutoa wito wa kufanyika mabadiliko ya sheria kuruhusu usuluhishi katika mashauri ya familia.

“Kwa kipindi cha miaka mitatu tumejikita katika kuhakikisha tunatoa haki kwa wakati kwa kuzingatia uadilifu na uwazi. Uzoefu unaonesha usuluhishi unahitajika sana ili kupunguza migogoro ya familia na kuongeza kasi ya umalizaji wa mashauri ya familia,” amesema Jaji Mnyukwa.

Takwimu zinaonyesha tangu kuanzishwa kwa kituo hicho hadi kufikia Agosti 26 mwaka huu kimehudumia wateja 580,610 na kati yao wanaume ni 265,985, wanawake 311,183 na watoto ni 3,442.

Related Posts