Bukoba. Kesi ya mauaji ya mtoto mwenye ualbino, Asimwe Novath iliyokuwa isikilizwe leo Desemba 11 imesogezwa hadi Februari 17, 2025 baada ya Mahakama kukosa majibu ya vipimo vya mshtakiwa namba moja, Padri Elipidius Rwegoshora.
Padre Rwegoshora alipelekwa Gereza Kuu la Isanga mkoani Dodoma kupimwa afya ya akili tangu Oktoba 25, 2024.
Kesi hiyo namba 15513/2024 inayowakabili washtakiwa tisa iliitwa leo Desemba 11, 2024 kwa ajili ya kusikilizwa, imeshindwa kuendelea baada ya Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba, Emmanuel Ng’igwana kusema hajapokea majibu ya vipimo vya mshatakiwa huyo.
Awali, mwendesha mashtaka wa Serikali, Erick Mabagala aliiambia mahakama kuwa wao kama Jamhuri hawamuoni mshtakiwa namba moja, Padri Rwegoshora mahakamani hapo, hivyo wanaiomba kama kuna taarifa kamili kuhusu mshtakiwa huyo wazijue na kama hazipo, basi Mahakama itaje tarehe nyingine ya kusikilizwa kesi hiyo.
Ndipo Jaji Emmanuel Ng’igwana anayesikiliza kesi hiyo alimuuliza wakili Mathias Rweyemamu anayemtetea Padri Rwegoshora kama ana hoja, naye akajibu kuwa wanasubiri maamuzi ya mahakama.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote kuhusu mwenendo wa kesi hiyo, Jaji Ng’ingwana amesema tangu Oktoba 25, 2024 mahakama hiyo ilitoa siku 42 za Padri Rwegoshora kupelekwa Isanga ili kupimwa afya ya akili baada ya Wakili Rweyemamu anayemtetea mshtakiwa huyo kudai ana matatizo hayo.
“Baada ya kupokea taarifa kutoka kwa wakili anayemtetea mshtakiwa huyo kuwa ana matatizo ya afya ya akili, basi na sisi mahakama tulijiridhisha kwa kufanya mahojiano kidogo na mshtakiwa tukaona ni kweli tukaona apelekwe Isanga apimwe kwanza.
“Siku 42 zimeisha na tarehe ya leo alipaswa awepo, ila mpaka sasa mahakama haijapokea taarifa kamili kuhusu vipimo alivyofanyiwa baada ya kupelekwa huko,” amesema Jaji Ng’igwana.
Jaji Ng’igwana amesema kuwa kesi hiyo itaendeshwa baada ya kupokea taarifa mwenendo wa vipimo alivyofanyiwa Padri Rwegoshora, hivyo ameahirisha kesi hiyo hadi Februari 17, 2025 itakapoitwa tena kwa ajili ya kusikilizwa.