Uzalishaji chakula ulivyosaidia kupunguza mfumuko wa bei 2024

Dar es Salaam. Kuimarika kwa uzalishaji wa chakula nchini kumetajwa kuwa  moja ya sababu ya kudhibiti mfumuko wa bei wa Taifa, ambapo umesalia kuwa asilimia tatu katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Uzalishaji unaoifanya Tanzania kuwa na akiba ya chakula na kuuza kingine nje kwa ajili ya kupata fedha za kigeni pia unatajwa kuwa sababu ya kuimarika kwa sarafu yake, hali inayofanya uchumi kuwa imara.

Haya yanaelezwa wakati ambao mfumuko wa bei katika mwaka ulioishia Oktoba, 2024 umeshuka hadi kufikia asilimia tatu kutoka asilimia 3.2 kipindi kama hicho mwaka 2023,  kwa mujibu wa Takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).

Kiwango cha mfumuko wa bei kilichokuwapo Oktoba 2023 ndicho kikubwa kuwahi kutokea kwa miezi 12 mfululizo.

Kiwango hiki kinabaki kuwa ndani ya lengo la Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ambayo imeweka ukomo wa asilimia 10 hali inayozidi kuleta nafuu kwa familia na wafanyabiashara.

Akizungumzia hali hiyo, mtaalamu wa uchumi kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dk Yohana Lawi anasema kilimo kinasaidia kudhibiti mfumuko wa bei kwa kuwa kinapunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje.

Uzalishaji wa chakula nchini ni asilimia 128 ikiwa juu ya kiwango kilichopangwa, huku baadhi ya mazao ya chakula yakiuzwa nje ya nchi.

Taarifa ya Wizara ya Kilimo inaonyesha uzalishaji wa chakula kwa msimu wa kilimo wa 2022/2023 ulitosheleza mahitaji ya chakula ya tani 16,390,404 kwa mwaka 2023/2024 na kuwepo kwa ziada ya tani 4,011,611.

Kutokana na hali hiyo, Taifa limejitosheleza kwa chakula kwa asilimia 124 ikilinganishwa na utoshelevu wa asilimia 114 wa mwaka 2022/2023, huku utoshelezi wa chakula ukitarajiwa kufikia asilimia 130 ifikapo mwaka 2025.

“Ni vyema kuwekeza zaidi katika kilimo kutosheleza mahitaji yetu kwani kadri tunavyozalisha ndivyo bei ya chakula inashuka sokoni,” anasema Dk Lawi.

Anasema mfumuko unaweza kubaki ulipo ikiwa nchi itaongeza uzalishaji utakaowezesha iuze nje bidhaa zake kuliko kununua kutoka nje, kutumia rasilimali za ndani kukidhi mahitaji na kuondoa utegemezi.

“Tuvutie wawekezaji wa nje wa moja kwa moja hii itatusaidia kuimarisha thamani ya Shilingi yetu, ni vyema pia kuhakikisha uzalishaji unaendana na mahitaji,” anasema.

Dk Lawi anasema kudhibitiwa mfumuko wa bei ni kiashiria cha kuimarika kwa Shilingi ya Tanzania, ambayo inaweka urahisi katika ununuzi wa bidhaa bila kutumia fedha nyingi.

Matumizi hayo anasema ni ununuzi wa mafuta na bidhaa za viwandani jambo linalofanya gharama ziwe nafuu.

Uwepo wa mfumuko wa bei unaotabirika unatajwa kuwa moja ya jambo linalovutia wawekezaji, kwani wanakuwa na uhakika wa kupata faida katika uzalishaji wanaolenga kufanya bila bidhaa kuathiriwa na mabadiliko ya bei.

Hali hiyo inatokana na kuwapo soko tulivu lisiloyumba, huku wananchi wakiwa na uwezo wa kununua bidhaa kwa ajili ya matumizi ya kila siku.

Mtaalamu wa uchumi na biashara, Dk Balozi Morwa anasema kwa uhalisia mfumuko wa bei unaposhuka unaleta ahueni katika maisha ya watu kwa kufanya thamani ya fedha ionekane mifukoni mwao.

Akitoa mfano anasema, “kushuka mfumuko wa bei kunafanya mtu akiwa na Sh10,000 kuwa na uhakika wa kupata mahitaji ya siku kutokana na bei nafuu ya vyakula, tofauti na hali inapokuwa kinyume chake.”

“Mfumuko wa bei kipimo chake rahisi kuonyesha ahueni kwenye maisha ya watu. Sasa nashindwa kupata ukweli wa hili kwa sababu kama ingekuwa chini basi ingefanya vitu kupungua lakini haijaonekana hasa katika uchumi huu unaendeshwa na mafuta katika uzalishaji,” anasema Dk Morwa.

Hata hivyo, anasema kiwango cha mfumuko wa bei kinapokuwa kidogo huvuta wawekezaji wanaotaka kuwekeza hela zao Tanzania.

Anatoa angalizo namna zinazotumika kuchambua mfumuko wa bei nchini ili kuleta uhalisia wa kile kinachozungumzwa kwa kugusa pande tofauti za nchi.

“Tutumie bidhaa zinazotumiwa na watu wengi, tuangalie upatikanaji wa takwimu ukoje, huenda tunatumia takwimu za Dar es Salaam pekee kuchambua mfumuko wa bei wa nchi nzima ni vyema kuangalia kila kanda, kama ni kiberiti tujue kila sehemu bei ikoje,” anasema.

Mchambuzi wa masuala ya uchumi, Rashid Aziz anasema mfumuko wa bei ni kama moto kwani unaweza kuwa rafiki au adui. Ukiwa umedhibitiwa, unaweza kuleta manufaa, lakini ukiachwa, unaweza kuharibu.

Katika andiko lake la Novemba 28, 2024 kupitia Mwananchi anasema kudhibiti ‘moto’ huo wa kiuchumi hudhibitiwa kwa kutumia sera madhubuti za kifedha na kibajeti kwa umakini mkubwa.

Hilo linafanya bei kupanda kwa wastani unaokadiriwa, siyo kwa kasi ya kudhuru ukuaji uchumi na BoT ndiyo imekuwa nguzo ya mafanikio hayo.

“Kwa mfano, kwa kuweka kiwango cha riba cha Benki Kuu kuwa asilimia sita na kusimamia kwa uangalifu mzunguko wa fedha, kumeweza kusawazisha mahitaji ya uchumi. Mathalani, katika msimu wa juu wa kilimo Septemba 2024, Benki Kuu iliongeza Sh2.1 trilioni katika mzunguko ili kukidhi mahitaji ya fedha za wanunuzi wa mazao. Hatua hii ilihakikisha shughuli za kiuchumi zinaendelea bila kusababisha mfumuko wa bei kupanda,” anasema.

Anasema utulivu wa bei si takwimu ya kiuchumi tu, ni uti wa mgongo wa maisha ya kila siku: “Mkulima anayepanga, msimu ujao wa kupanda mazao au mzazi anayebuni bajeti ya ada ya shule hutegemea kutabirika kwa bei. Wakati mfumuko wa bei unadhibitiwa, unaleta ujasiri si tu kwa masoko, bali pia kwa mustakabali wa watu, si jambo la kubeza.”

“Ili kujenga msingi thabiti zaidi, Tanzania inapaswa kuimarisha mifumo ya kilimo, kupanua chaguo za nishati mbadala na kuboresha ufanisi wa masoko ili kupunguza mfumuko wa bei wa chakula na nishati,” anasema.

Related Posts