Gekul aendelea kung’ang’aniwa, anayedai kushambuliwa akata rufaa

Arusha. Kijana, Hashim Ally ameendelea kumng’ang’ania mbunge wa Babati Mjini (CCM), Pauline Gekul baada ya kuwasilisha taarifa Mahakama ya Rufani Tanzania ya kusudio la kukata rufaa kupinga uamuzi uliotolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Manyara.

Hashim aliyekuwa mfanyakazi wa mbunge huyo, kupitia kwa wakili wake, Peter Madeleka, amewasilisha notisi hiyo katika Masjala ya Mahakama Kuu Kanda ya Manyara na kupokelewa Mei 7, 2024, akisema nia ni kupinga sehemu ya uamuzi huo.

Hashim anapinga uamuzi wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara uliotolewa na Jaji Devotha Kamuzora, Aprili 15, 2024 uliotupilia mbali rufaa aliyokuwa amekata dhidi ya mbunge , ambaye pia alikuwa Naibu Waziri wa Sheria na Katiba.

Wakili Madeleka mwenyewe kupitia ukurasa wake wa X (zamani Twitter) saa 2:17 asubuhi ya leo Mei 9, 2024 ameandika: “Rufaa dhidi ya Pauline Gekul katika Mahakama ya Rufani Tanzania, imepokelewa katika Masjala ya Mahakama Kuu Manyara Mei 7, 2024.”

Awali, Aprili 15, 2024, Mahakama Kuu Kanda ya Manyara ilitupilia mbali rufaa iliyokuwa imefunguliwa na Hashim dhidi ya mbunge huyo, baada ya kukubaliana na hoja moja kati ya tatu za pingamizi zilizowasilishwa na mbunge huyo kupitia wakili wake.

Uamuzi wa Jaji unaopingwa

Jaji Kamuzora katika hukumu yake, alieleza kuwa baada ya Mahakama kupitia hoja za pande zote mbili kuhusiana na pingamizi la awali, amekubaliana na hoja moja ya pingamizi hilo kwamba Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza rufaa hiyo.

Alieleza kuwa uamuzi wa hoja hiyo moja unatosha kumaliza rufaa hiyo kwa kuitupilia mbali na kwamba, haoni sababu ya kuangalia hoja nyingine mbili za pingamizi la awali lililowasilishwa na mjibu rufaa ambaye ni Gekul.

Baada ya rufaa yao kutupwa, Wakili Madeleka akizungumza na  wanahabari nje ya Mahakama aliweka wazi kuwa walikuwa hawajaridhishwa na uamuzi huo wa Jaji Kamuzora na wanatarajia kukata rufaa Mahakama ya Rufani kuupinga.

Wakili Madeleka alienda mbali na kueleza kuwa kama wakikosa haki katika Mahakama hiyo, watakata rufaa Mahakama ya Haki za Binadamu ya Afrika.

Katika rufaa hiyo, mrufani alikuwa na sababu sita za rufaa hiyo akipinga uamuzi wa Mahakama ya Wilaya ya Babati kuifuta kesi yake na alipoziwasilisha kortini, mjibu rufaa (Gekul) aliwasilisha pingamizi akiiomba Mahakama hiyo iitupilie mbali rufaa hiyo.

Sababu za rufaa pamoja na pingamizi la Gekul, zilizisikilizwa kwa pamoja Machi 21, 2024, kisha Jaji Kamuzora akaahirisha shauri hilo hadi Aprili 15, 2024 kwa ajili ya uamuzi.

Awali, Desemba 27, 2023 Mahakama ya Wilaya ya Babati iliifutilia mbali kesi ya jinai ukatili iliyokuwa ikimkabili mbunge huyo, iliyohusu tuhuma za unyanyasaji dhidi ya Hashim aliyepata kuwa mfanyakazi wake.

Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Victor Kimario, aliifuta kesi hiyo baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), kuwasilisha taarifa ya kutokuwa na nia ya kuendelea na mashitaka chini kifungu 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) Sura ya 20 kama kilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2022.

Gekul alikuwa akikabiliwa na shitaka moja la shambulio na kusababisha madhara ya mwili chini ya kifungu cha 241 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, marekebisho ya mwaka 2022, mashitaka ambayo hayakufikia hatua ya Gekul kupanda kizimbani.

Related Posts