Dk Mwinyi aonya watakaofuja mali za umma, akizindua rasimu ya Dira 2050

Unguja. Wakati Watanzania milioni 1.1 wakishiriki kutoa maoni kuhusu Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema wakati wa utekelezaji wake watatoa adhabu kali kwa watakaojaribu kufuja mali za umma.

Wengine watakaokumbana na kibano hicho ni watakaotoa huduma zisizoridhisha kwa wananchi, kusimamia vibaya fedha za walipakodi na kushindwa kufikia malengo.

Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Jumatano, Desemba 11, 2024 alipozindua rasimu ya dira hiyo, Unguja. Amesema matarajio ya dira hiyo lazima yajengwe katika msingi imara wa uongozi, amani, ulinzi na utulivu.

“Wakati wa utekelezaji wa dira hii tunatarajia kupongeza watendaji wanaofanya vizuri kwenye maeneo yao ya kazi, lakini tutatoa adhabu kali kwa wale watakaojaribu kufuja mali za umma, utoaji huduma usioridhisha kwa wananchi, kusimamia vibaya fedha za walipakodi,” amesema.

Amesema katika kuyafikia matarajio hayo, ni lazima wakubaliane kuwa utekelezaji wa dira ya 2050 unahitaji kwanza uchumi imara, jumuishi na shindani.

Dk Mwinyi amesema Serikali ina wajibu wa kuweka mazingira rafiki na mazuri, ili kuvutia biashara na uwekezaji, kukuza ushirikiano na wadau hususani sekta binafsi, kuwekeza katika kujenga na kukuza ujuzi wa watu na kuleta ustawi wa jamii.

“Kwa msingi huo, kila mmoja wetu katika nafasi yake anawajibika kuchagua uongozi bora, kulinda amani, usalama, utulivu na umoja wa Taifa letu, bila uongozi, amani, usalama, utulivu na umoja katika nchi yetu hakuna shughuli ya kimaendeleo inayoweza kufanyika,” amesema.

Kwa upande wa Serikali, Dk Mwinyi amesema: “Tunawajibu wa kuweka mazingira rafiki na mazuri, ili kuvutia biashara na uwekezaji, kusimamia ajenda ya utunzaji wa mazingira na kuweka nguvu katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.”

Amesema mafanikio ya utekelezaji wa Dira 2050 yatachochewa na miundombinu fungamani, sayansi na teknolojia, tafiti na maendeleo ikijumuisha uvumbuzi na mageuzi ya kidijitali.

Amesema mipango katika ngazi zote itachochewa na kunufaika na fursa adhimu ya miundombinu bora iliyofungamana na sayansi na teknolojia, tafiti na uvumbuzi wa teknolojia mpya na zijazo.

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi (kulia) akimkabidhi Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kitabu cha rasimu ya dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 baada ya kuzinduliwa leo Desemba 11, 2024 Unguja Zanzibar.

Amesema mafanikio ya utekelezaji wa Dira 2050 yatatokana na uwepo wa sekta chache za kimageuzi zenye kutoa fursa kubwa katika mnyororo mzima ambazo zitakuwa injini ya kuzalisha ajira nyingi, fursa ya mauzo nje na mchango kwa sekta nyingine na zenye kuchangia usimamizi wa mazingira.

“Kwa msingi huo, wakati wa utekelezaji sekta zenye sifa hizo zitapewa kipaumbele hata katika bajeti ili zileta mageuzi makubwa katika uchumi na jamii, hatimaye kuifanya nchi iwe yenye hadhi ya kipato cha kati cha juu na kuleta maendeleo ya watu ifikapo mwaka 2050,” amesema.

Amesema utekelezaji wa dira utakuwa wa tofauti, wakitarajia kusimamia na kulinda rasilimali za nchi, ikiwemo fedha zinazokwenda kwenye miradi na programu za maendeleo na zile zinazoendesha shughuli za kila siku kwenye ofisi za umma.

Licha ya mipango ya muda mrefu kuwa takwa la kikatiba, Dk Mwinyi amesema dira kwa Taifa ni muhimu na yenye manufaa. Amesema kutokana na ushiriki wa wananchi mchakato huo utaimarisha mshikamano na umoja wa kitaifa.

Pia utawezesha muunganiko wa sera, mipango na mikakati ya kisekta, sekretariati za mikoa na mamlaka za Serikali za mitaa kuweka muktadha wa maendeleo ya kitaifa katika mwelekeo wa makubaliano au mipango ya kikanda na kimataifa.

Dira ya 2050 itakuwa na malengo makuu matano ya kuwa Taifa lenye uchumi himilivu na jumuishi wa kipato cha kati cha juu ambao utamilikiwa na makundi yote.

Mengine ni kuwa Taifa lililoweka kipaumbele cha maendeleo bora ya watu wote, maisha bora na ustawi kwa wote, mfumo wa utawala jumuishi, ulio wazi na wenye kuwajibika na kuwa Taifa linalotunza uoto wa asili, mazingira na rasilimali kwa kizazi kijacho ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Awali, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amesema tangu mchakato wa maandalizi ya dira pamoja na nyenzo za utekelezaji wake uzinduliwe Aprili 3, 2023 na Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango, kazi kubwa imefanyika chini ya kamati iliyoundwa na timu ya dira kuhakikisha itawapeleka kuzingatia mabadiliko makubwa yanayoendelea kote duniani.

Amesema wajumbe walishiriki makongamano katika nchi nzima kuhakikisha wananchi wanachukuliwa maoni yao, hivyo kamati imekuwa ikishauri na itaendelea kushauri ili kupata dira bora na nzuri.

“Kamati imetimiza wajibu wake kuhakikisha wananchi wanatoa maoni yao kadri iwezekanavyo na kuhusisha Watanzania wengi waliopo ndani na nje ya nchi (Diaspora) kwa njia mbalimbali, ikiwemo mitandao ya kijamii. Naweza kusema rasimu hii ni ya Watanzania,” amesema.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema mpaka kufikia rasimu ya kwanza, imepitia hatua 11 ikiwa ni pamoja na kuandaa miongozo na kuchukua maoni kwa watu mbalimbali ambapo jumla ya wananchi milioni 1.1 wametoa maoni yao.

Amesema baada ya uzinduzi wa rasimu hiyo ya kwanza, itaandaliwa ya pili ambayo itawasilishwa serikalini na kuifanyia uamuzi, kisha itawasilishwa bungeni katika mkutano wa bajeti mwaka 2025 na ikitoka huko inatarajiwa kuzinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kati ya Mei au Juni, 2025.

Ametaja baadhi ya shabaha za jumla za dira hiyo ni Tanzania kuwa nchi ya hadhi, kuondoa umaskini, Kiswahili kuwa lugha ya heshima duniani, kuwa taifa linalojitegemea na kila Mtanzania angalau awe na elimu ya kidato cha nne ifikapo mwaka 2025.

Waziri Fedha na Mipango, Dk Saada Mkuya amesema Zanzibar imeshiriki kikamilifu katika uandaaji wa dira hiyo kwa hatua mbalimbali na kwamba wataendelea kusimamia kuhakikisha maoni ya Wazanzibari yanazingatiwa katika dira hiyo.

Related Posts