Wagonjwa wa kipindupindu wafikia 22 Mbeya, mamalishe, vilabu vya pombe hatarini

Mbeya. Jiji la Mbeya limeanza kuchukua hatua za kudhibiti maambukizi ya ugonjwa wa kipindupindu kutokana na watu wanaougua ugonjwa huo kufikia 22.

Hatua hizo ni pamoja na kufunga visima vya maji, mama na baba lishe pamoja na vilabu vya pombe ambavyo havikidhi viwango vinavyohitajika.

Hata hivyo, licha ya ongezeko la wagonjwa, hakuna kifo kilichoripotiwa na wagonjwa wote wametengewa maeneo maalumu kwa ajili ya matibabu.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumatano, Desemba 11, 2024, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Yesaya Mwasubila amesema idadi ya wagonjwa imeongezeka kutoka 17 walioripotiwa siku tatu zilizopita hadi kufikia 22 usiku wa kuamkia leo.

Kwa mujibu wa Dk Mwasubila, halmashauri imeanzisha operesheni maalumu ya kukagua visima vya maji, masoko na vyombo vya moto kama bajaji na pikipiki.

Aidha, maeneo ya vilabu vya pombe za kienyeji na mama lishe wasiozingatia kanuni za usafi amesema yatafungwa.

“Tumetoa maelekezo kwa madereva wa bajaji na bodaboda kuchukua tahadhari kwa abiria wanaotumia vyombo hivyo,” ameongeza.

Amesema kati ya visima saba vilivyokaguliwa, vitatu vimepatikana na vimelea vya kipindupindu na ukaguzi zaidi wa visima 286 umeanza.

“Kuanzia kesho tutaanza pia kukagua vibali na kupima ubora wa maji hayo ya visima,” ameeleza.

Dk Mwasubila amewataka wananchi kushirikiana katika kipindi hiki cha operesheni, huku akisisitiza umuhimu wa kunawa mikono, kunywa maji yaliyochemshwa na kula vyakula safi na vya moto, hasa kwa kuzingatia hali ya mvua zinazoendelea.

Amesema halmashauri imeongeza juhudi za kuzolewa taka kwa wakati na kufuatilia hali ya wagonjwa waliobainika.

Kyela yaendelea kuchukua tahadhari

Kwa upande wa Wilaya ya Kyela, Mganga Mkuu wa halmashauri hiyo, Dk Saumu Kundisaga amesema hakuna mgonjwa aliyeripotiwa, lakini wanaendelea na juhudi za upimaji afya za watu katika maeneo mbalimbali.

“Hata kabla ya taarifa za viashiria vya ugonjwa, tumekuwa na utaratibu wa kufuatilia hali ya afya kupitia idara ya afya ya kinga, hasa katika maeneo ya mpaka wa Kasumuru,” amesema na kuongeza kuwa tayari wameweka vitakasa mikono kwenye mipaka ili kudhibiti magonjwa ya mlipuko.

Akizungumzia mlipuko huo, Huruma Denis, mkazi wa Kata ya Ruanda, amepongeza mkakati wa kufunga visima na kusafisha maeneo machafu, lakini ameonya ukosefu wa huduma za maji safi unaweza kuathiri utekelezaji wa mikakati hiyo.

“Kwa mfano, hapa kwetu tumekaa siku nne bila maji. Serikali inapaswa kujua hali hii inaathiri vipi maisha ya kila siku ya watu na ukizingatia kipindupindu ndiyo hicho kimelipuka,” amesema.

Naye Tedius Joseph, ameshauri Serikali kuongeza juhudi katika ukarabati wa miundombinu, hasa ya maji ili kudhibiti uchafu unaosababisha magonjwa ya mlipuko.

“Kipindupindu ni matokeo ya uchafu na kukiwa na upatikanaji wa maji safi na salama, changamoto kama hizi zinaweza kupungua,” amesema.

Related Posts