Dar es Salaam. Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima amesema kwa kushirikiana na wizara nyingine za kisekta wanaandaa sheria kuhusu usimamizi wa huduma za kada ya ustawi wa jamii.
Amesema hayo leo Desemba 11, 2024 katika mahafali ya 48 ya Chuo cha Ustawi wa Jamii, Kijitonyama na mahafali ya saba ya tawi la Kisangara yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Mahafali hayo yamehusisha wahitimu 3,121 wa ngazi ya astashahada, stashahada, shahada ya kwanza na shahada ya juu.
Dk Gwajima amesema sheria itakwenda kuinua huduma za ustawi wa jamii kwa viwango vingine, pia italinda taaluma ili huduma inayotolewa na maofisa wa ustawi kutovamiwa na watu wanaotoa zilizo chini ya viwango na kuwauzia kesi maofisa hao.
“Sheria hii pia itawaruhusu kusajiliwa na msajili wenu na kupewa vibali vya kufungua huduma zenu binafsi za ustawi wa jamii kama ilivyo kwenye huduma nyingine za binafsi,” amesema.
Amesema watoa huduma za kijamii wanakutana na changamoto za aina mbalimbali, zikiwamo mauaji hivyo tiba zikiwa hazijasajiliwa watu hudanganywa ni mambo ya ushirikina.
“Kwa sababu mpo katikati ya jamii, mtakuwa mnatoa huduma zenu na kujiajiri kama ambavyo sekta nyingine ina huduma binafsi, hii ni hatua kubwa kwenu muiombee sheria hii ipite,” amesema.
Dk Gwajima amesema huu ni wakati wa kuinua kada ya ustawi wa jamii na huduma zao kutokana na uhitaji wa dunia katika sekta hiyo.
“Juzi saa 5.47 usiku nilipokea ujumbe wa maneno kutoka Dodoma, Mtaa wa Iyumbu kwamba kuna mtoto anapigwa, Mungu alinisaidia nilikuwa macho ningepeleka wapi hili suala? Mtu wa kwanza nilimuamsha ofisa ustawi wa jamii wa Dodoma.
“Naye akamtafuta mtu wa dawati la jinsia wakafanya kazi usiku hadi katika eneo la tukio walikuta mtoto ameumizwa, yeye na binti wa kazi. Kufuatilia ni mtoto wa ndugu yake alimchukua kwa ajili ya kusoma,” amesema.
Baada ya uchunguzi amesema wamegundua wahusika wana tatizo la kisaikolojia ambalo lilikuwa linahitaji huduma kutoka kwa wahusika wa masuala hayo.
“Changamoto hizi zinatokea katika jamii na watu hawasemi mpaka yatakapotokea madhara,” amesema.
Amesema watu wana kiu ya wataalamu wa ustawi wa jamii ambao wakiwezeshwa kufika maeneo mbalimbali inaweza kusaidia kumaliza matatizo yaliyopo kwa namna ya tofauti.
Dk Gwajima ametoa maagizo kwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk Seif Shekalaghe kushirikiana na uongozi wa chuo hicho kufanya tathimini ya gharama za ujenzi wa madarasa na majengo mengine yanayohitajika kwa ajili ya kujumuisha kwenye bajeti ya maendeleo ya mwaka ujao wa fedha.
Ameagiza watafutwe wadau wa maendeleo na kuandaliwa kikao kuwapa mpango uliopo ili kusaidia chuo hicho kuendelea kupinga masuala ya ukatili wa kijinsia na watoto.
Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya Magavana ya Chuo cha Ustawi wa Jamii, Sophia Simba amesema kimeanzisha programu ya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto.
“Katika kuitikia wito wa Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu mapambano ya ukatili wa aina zote ule wa kimwili, kisaikolojia, kingono na kiuchumi; chuo chetu kinatoa elimu, ushauri nasaha na msaada wa kisaikolojia kwa jamii,” amesema.
Amesema wanashirikiana kwa karibu na taasisi mbalimbali kuhakikisha watu wanapata huduma za kisaikolojia hasa kwa waliopoteza ndugu, jamaa na marafiki katika majanga ya maafa.
Aliyekuwa rais wa serikali ya wanafunzi wa chuo hicho, Mickdad Uhuru amesema wataendelea kujiimarisha na kuwa bora zaidi na kutoa thamani ya kile walichojifunza watakapokwenda kuhudumia jamii.
“Elimu ni silaha yenye nguvu zaidi unayoweza kuitumia kubadilisha dunia,” amesema.