Iringa. Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Iringa imeanzisha rasmi huduma mpya ya kujifungua, huku ndugu au mweza wako akishuhudia namna tukio hilo linavyotokea.
Akizungumza na mwananchi ofisini kwake December 10, 2024 Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo Dk Alfred Mwakalebela amesema huduma hiyo ni mpya katika mkoa huo, hivyo mjamzito atapaswa kwenda na mwenza au ndugu wa karibu wakati yupo katika hatua za uchungu.
“Mtu anayetaka kuja naye, mjamzito ndiyo atachagua kati ya mweza au ndugu yake wa karibu na wataweza kuingia wote katika chumba cha kujifungulia,” amesema Dk Mwakalebela.
Aidha Dk Mwakalebela amesema kuwa baada ya wawili hao kuingia katika chumba cha kujifungulia, mweza au ndugu atapewa kazi ya kumliwaza mama mjamzito anayetarajia kujifungua kwa kumsemesha maneno huku akimpapasa sehemu ya mgogoni kwa sababu kwa kufanya hivyo uchungu huwa kupungua.
Dk mwakalebela amesema huduma hiyo itaambatana na namna ya kujifungua kwa sababu walikuwa wanajifungua kwa aina moja, lakini kwa sasa mjamzito atachagua anahitaji kujifungua akiwa amekaa, amesimima au amelala.
Daktari bingwa wa magonjwa ya kina mama na uzazi, Dk Scolastica Malangalila amesema kuwa wameanza kampeni ya kutoa elimu kwa umma kuhusu ujio wa huduma hiyo ikiwemo kuendelea kutoa elimu kwa ndugu pamoja na wenza juu ya huduma hiyo.
“Kwa sasa tunaendelea kutoa elimu kwa watoa huduma namna ya kutoa elimu kwa wanaume (wenza) kwa sababu ni kitu kipya, wakati wanapoanza kliniki kwa ajili ya kupima ndipo wataanza kuwaelekeza mjamzito ampange mtu gani ambaye atakwenda naye siku ya kujifungua,” amesema Dk Malangalila
Wakitoa maoni yao kuhusu huduma hiyo baadhi ya wazazi wamesema kuwa wameipokea vizuri kuanzishwa kwa huduma hiyo wakati wa kujifungua kwenda na ndugu au mume kwa sababu itasaidia kuongeza upendo katika familia.
“Kwa sasa vijana wengi tunaongoza kubeba mimba ukizingatia tunakuwa tunachaguana tukiwa vijana wadogo hivyo huduma hii itasaidia wenza wetu kukujali na kukuthamini baada ya kuona namna ambavyo unajifungua sanjari na kuongeza upendo kwa mama yake,” amesema Jahida Juma.
Naye Ally Hussein (sio jina lake halisi) amesema huduma hiyo ni nzuri kwa sababu itasaidia kupunguza tatizo ya kuibiwa na kubadilishiwa watoto, kwa sababu mume mwenyewe atakuwa ameshuhudia namna mtoto wake alivyozaliwa.