KIUNGO mshambuliaji wa zamani wa Simba, Jimmyson Mwanuke na beki Faria Ondongo wapo hatua ya mwisho ya mazungumzo ya kujiunga kwa mkopo Fountaine Gate wakitokea Singida Black Stars.
Ondongo msimu huu alikuwa akikipiga kwa mkopo Tabora United baada ya Singida kumpeleka huko, lakini hivi karibuni ilielezwa klabu mama aliyokuwa akiichezea imemrudisha kabla ya kuelezwa Fountain Gate kuanza mazungumzo na Singida ili kumchukua.
Huenda mazungumzo hayo yakaenda vyema kutokana na ukweli nyota hao wawili hawana namba katika kikosi cha kwanza cha Singida Black, kutokana na mastaa wanaocheza katuika nafasi hiyo ndani ya timu hiyo.
Chanzo cha kuaminika kutoka Singida BS kililiambia Mwanaspoti, kuwa wachezaji hao wanatolewa kwa mkopo ili kwenda kuendeleza vipaji vyao kutokana na kukosa nafasi ya kucheza.
“Kukosa nafasi ya kucheza Singida Black Stars haina mana hawana uwezo wa kufanya vizuri nje ya timu yetu, tuna kila sababu ya kujivunia vipaji walivyonavyo na tuna imani kubwa wanapokwenda watakuwa bora na watapambana kurudi tena,” alisema chanzo hicho na kuongeza;
“Wachezaji wameomba kutolewa kwa mkopo na sisi kama viongozi tumefanya jitihada ya kuzungumza nao na kuwatafutia timu ambayo watakuwa na wakati mzuri wa kucheza kama ilivyo kwa mshambuliaji na kinara wa mabao kwa sasa wa Ligi Kuu, Seleman Mwalimu ‘Gomez’.”
Alisema tayari viongozi wamefanya makubaliano ya kuwapeleka nyota huo Fountaine, wakiamini itakuwa timu itakayowapa nafasi ya kucheza ili kulinda viwango vyao.
Wachezaji hao endapo dili lao litakamilika wataungana na Israel Mwenda aliyetambulishwa jana na Yanga akienda kwa mkopo, huku Habib Kyombo akitajwa kujiunga na Pamba Jiji, Kelvin Nashon aikielezwa anajiandaa kutua Yanga na Najim Mussa aliyetua Namungo.