Tabora. Mtoto wa mwaka mmoja na miezi minane aliyefahamika kwa jina la Martine Ndaro amefariki dunia baada ya kupigwa shoti na waya wa kushikikilia nguzo ya umeme jirani na nyumba yao.
Pia mtoto mwingine anayeitwa Vaileth Ndaro mwenye umri wa miaka miwili, amenusurika katika ajali hiyo iliyotokea jana Jumanne Desemba 10, 2024.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano Desemba 11, 2024 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao amesema; “Ni kweli tuna tukio la watoto wawili kupigwa shoti ya umeme na kusababisha kifo cha mtoto mmoja.”
Amesema tukio hilo lilitokea kwenye nyumba ambayo iko Mtaa wa Shule eneo la CG Nation Manispaa ya Tabora.
Amedai kuwa watoto hao watoto hao walishika waya unaoshikilia nguzo za umeme na ulikuwa na umeme, wakapigwa shoti na kusababisha kifo cha mtoto mmoja.
“Huyu wa miaka miwili alipomuona mwenzake amenaswa aliekwenda kumshika na yeye akapigwa na shoti ya umeme. Hata hivyo mtoto huyo alijeruhiwa na anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Tabira Kitete,” amesema kamanda huyo.
Abwao amesema mwili wa marehemu unaendelea kufanyiwa uchunguzi katika Hospitali ya Kitete na baada ya kukamilika utakabidhiwa kwa ndugu ili ukafanyiwe taratibu za mazishi.
Eneo ambako eo tukio lilimetokea salama Shirika la Umeme Tanesco Mkoa wa Tabora limechukua hatua stahiki kuhakikisha hakuna hatari nyingine iliyotokea.
Hata hivyo, Abwao ametoa wito kwa wazazi na walezi kuwa na uangalizi mzuri kwa watoto wao ili wasiendee kucheza kwenye maeneo ambayo ni hatarishi hususani kipindi hiki cha mvua.
Mwananchi Digital ilimtafuta Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Mkoa wa Tabora, Mhandishi Amina Ng’amba ambaye amesema atalizungumzia suala hilo kesho kwa sababu yuko safarini wilayani Nzega.
“Kwa sasa niko Wilayani Nzega, nitatoa taarifa rasmi kesho kuhusiana na hili lililotokea,” amesema kwa kifupi baada ya kupigiwa simu.
Akizungumzia tukio hilo, Eduard Wilson, ambaye ni jirani wa familia ya watoto hao, amesema kabla ya ajali hiyo, alikuwa na watoto hao nyumbani kwake. Hata hivyo, muda mfupi baada ya watoto kutoka nje, akasikia kelele za taharuki zilizomfanya atoke haraka akakuta wamenaswa na umeme.
“Tulitafuta fimbo kavu na kusogea kwenye nguzo hiyo yenye umeme mkubwa. Nikawasukuma nayo wakaanguka chini lakini hawakupumua. Nilidhani wamekufa wote, lakini baada ya muda mmoja akaanza kupumua,” amesimulia Wilson.
Amesema aliwawahisha Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kitete ambako walipokewa na baada ya kuwekea gesi, mtoto mmoja, Vaileth alizinduka na kupiga kelele.
“Lakini Martine madaktari wakasema alikuwa tayari amekufa,” amesema jirani huyo.
Hata hivyo, jirani mwingine Venonsa Masao amesema kuwa nguzo hiyo nguzo ina hitilafu kwa muda mrefu sasa.
“Mafundi wa hufika eneo hili mara kwa mara kwa ajili ya kufanya matengenezo lakini huwa hawatoi tahadhari kwa watu inaonekana ina shida ya kuvujisha umeme,” amedai jirani huyo.
Baba wa watoto hao, Nyangi Ndaro ambaye ni mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Wavulana Tabora, amesema hakuwapo nyumbani wakati wa ajali hiyo. Hata hivyo, majirani walijitahidi kuwaokoa watoto wake.
“Tukio limetokea nikiwa kwenye mashamba ya shule kule Tabora Boys. Nilipopata taarifa, nilikimbilia hospitalini. Nilipofika nikaambiwa mtoto wangu mdogo amefariki dunia, lakini mwingine anaendelea vizuri na amesharuhusiwa kurudi nyumbani,” amesimulia Ndaro.
Ameongeza kuwa, kwa kuwa yeye ni mtumishi wa umma, anasubiri taratibu za kiutumishi ili kusafirisha mwili wa mtoto wake kwa ajili ya maziko Wilaya ya Malinyi, Mkoa wa Morogoro.
Diwani wa Kata ya Kitete, Mussa Kayolo amesema nyaya za nguzo hiyo zimechoka na zimesogeleana na waya unaoshuka ardhini. Ameitaka Tanesco kufanya ukaguzi wa nguzo zote ili kuepusha madhara zaidi.
“Nyaya nyingi za nguzo hii ziko wazi na zimekaribiana na waya unaoshuka ardhini kwa ajili ya kuimarisha nguzo. Tanesco wanapaswa kukagua nguzo zote ili kuepusha ajali zaidi,” amesema Kayolo.