Kuimarika kwa Shilingi kuna maana gani kwako?

Ni habari njema kwa wengi, hususan wafanyabiashara na watumiaji wa bidhaa zinazotoka nje ya nchi. Ni nafuu pia kwa Serikali kuhudumia madeni yake na kulipa watoa huduma ambao mikataba yao imefungwa kwa sarafu ya kigeni.

Habari hiyo njema inatokana na kuimarika kwa Shilingi dhidi ya sarafu za kigeni, kwani sasa viwango vya kubadilishia fedha vimeimarika na kuwa nafuu zaidi kwa Tanzania, tofauti na kipindi cha miezi mitatu iliyopita.

Maana yake ni kuwa gharama za uagizaji wa bidhaa sasa zitapungua ikilinganishwa na wakati ambapo thamani ya Shilingi ilikuwa chini, lakini pia nchi itaweza kuvuna fedha nyingi za kigeni, kwani ili kununua bidhaa za Tanzania itamlazimu mnunuzi kuwa na sarafu zaidi ya kigeni.

Mathalan, viwango vya kubadilisha Dola ya Marekani sasa vimefikia kiwango cha juu dhidi ya Shilingi katika kipindi cha miezi 10 na Serikali inabainisha kuwa hali hii inaweza kuendelea hadi Februari 2025.

Kwa siku ya jana (Desemba 11, 2024) Benki Kuu ya Tanzania (BoT) iliripoti kuwa Shilingi ilikuwa inauzwa kwa wastani wa Sh2,430.5975 dhidi ya Dola ya Marekani. Hii ni sehemu ya mwenendo wa kuimarika ulioanza kuonekana Oktoba mwaka huu.

Oktoba 4, 2024, Dola iliuzwa kwa Sh2,721.68, na ikaimarika hadi Sh2,716.48 kufikia Oktoba 23. Hali hiyo iliendelea hadi kufikia Sh2,620.57 mwishoni mwa Novemba na kiwango cha sasa, cha Sh2,430.5975, kinafanana na kile kilichorekodiwa Februari 1, 2024.

Kwa mujibu wa BoT, sababu za kuimarika kwa Shilingi ni pamoja na ongezeko la mauzo ya nje, ukuaji wa utalii na kupungua kwa uagizaji wa bidhaa kutoka nje.

Aidha, hatua ya Marekani kuendelea kupunguza viwango vya riba chini ya utawala mpya wa Donald Trump, imechangia kupunguza shinikizo kwa sarafu za nchi zinazoendelea.

Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba amelieleza gazeti la The Citizen, kuwa hali ya kuimarika kwa Shilingi inatarajiwa kuendelea hadi Februari 2025. Alieleza kuwa matarajio hayo yanatokana ongezeko la uzalishaji wa mazao muhimu kama korosho inayouzwa sasa pamoja na mahindi na mpunga baadaye mwezi huu.

“Mpango wa kufadhili usafirishaji wa bidhaa nje ya nchi (Export Guarantee Scheme) uliozinduliwa Juni 2023, umeongeza thamani na wingi wa mauzo ya mazao nje ya nchi,” anasema Tutuba. Pia anabainisha kuwa miradi ya Stamico inatarajiwa kupewa dhamana ili kuchochea uzalishaji zaidi.

BoT inasimamia mipango miwili ya dhamana za mikopo kwa niaba ya Serikali: Export Credit Guarantee Scheme (ECGS) na Small and Medium Enterprises Credit Guarantee Scheme (SME-CGS). Mpango wa ECGS ulirekebishwa mwaka 2023 ili kusaidia miradi yenye lengo la kuuza nje, ambayo haina dhamana ya kutosha.

Tutuba alisisitiza kuwa kufufua mipango hii ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuongeza uzalishaji na mauzo ya nje. “Serikali inashirikiana na sekta za kilimo, mifugo, uvuvi, na viwanda kuboresha uzalishaji,” anasema.

Aliendelea kuwa Tanzania sasa inazalisha bidhaa kama vioo, vigae na nyaya za umeme, jambo ambalo limepunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje. Aidha, bei ya mazao kama kahawa na korosho imeongezeka kutokana na mipango kama Soko la Bidhaa Tanzania (TMX).

Sekta ya utalii nayo imeonyesha ukuaji, licha ya kuingia msimu wa utulivu. Tutuba aliongeza kuwa juhudi za kuhimiza matumizi ya Shilingi badala ya sarafu za kigeni zimepunguza mahitaji ya Dola za Marekani.

Kuhusu hali ya uchumi wa dunia, alisema kushuka kwa thamani ya Dola ya Marekani kumesababishwa na sababu za kimataifa, ikiwa ni pamoja na ongezeko la uzalishaji baada ya janga la Uviko-19.

Mchambuzi wa masuala ya kifedha, Oscar Mkude, alisema kuwa mauzo ya nje yameimarisha uchumi wa Tanzania: “Jitihada za Serikali za kuongeza mauzo ya nje na kupunguza uagizaji zimeimarisha Shilingi”.

Hata hivyo, alionya kuwa ni muhimu Serikali kusimamia sera zake za kifedha kwa umakini, ili kuepuka kudhoofisha thamani ya Shilingi.

Akizungumzia hali hiyo, Profesa Haji Semboja wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) amebainisha kuwa mara nyingi shilingi huimarika dhidi ya dola ya Marekani baada ya mwaka wa kifedha kutulia.

Anaeleza kuwa misimu ya mauzo ya mazao makubwa ya kilimo na kipindi cha kilele cha utalii ni mambo muhimu yaliyosaidia kuimarika kwa mapato ya fedha za kigeni ya Tanzania, hivyo kuimarisha shilingi.

“Changamoto kwa uchumi wetu, kama ilivyo kwa mataifa mengine ya Afrika, ni kwamba kile tunachozalisha hakihitajiki sana na majirani zetu,” anasema Profesa Semboja.

“Hata hivyo, mambo ya msimu kama mauzo ya mazao ya kilimo na utalii husaidia kuimarisha sarafu ya ndani.”

Mchambuzi wa Uchumi na Biashara, Dk Donath Olomi anasema kwa nchi ambayo inategemea sana kuagiza vitu kutoka nje, dola inapokuwa juu inaongeza gharama za uzalishaji, gharama za maisha, kufanya biashara hata mahitaji ya watu binafsi yanapanda bei.

Hivyo kushuka kwake kunaleta ahueni kwa watu wanaotaka kuendesha biashara na kufanya kitu kingine chochote hata ujenzi. “Hata hivyo, kwa upande mwingine inang’ata kwa sababu mtu anayeuza vitu nje kwa dola anakuwa kama anapoteza kwa sababu atapata hela kidogo na hii inaweza kushusha hamasa ya watu kuuza vitu vyao,” anasema Dk Olomi na kuongeza:

“Sisi wenyewe tulichangia kupanda kwa dola, Serikali iliweka masharti ikitaka baadhi ya vitu kulipiwa kwa dola na ilisababisha mahitaji ya dola ambayo si ya lazima, hali hii ilifanya watu wengi kuhodhi dola kwa kuona inaenda juu.

Kwa upande mwingine, Meneja Programu wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Kennedy Rwehumbiza anasema jambo hili lina athari chanya katika uchumi, kwani shilingi inapopata nguvu dhidi ya dola, maana yake mtu atahitaji fedha kidogo kununua dola kwa ajili ya kulipia huduma na bidhaa.

Hali hii itasaidia kushusha gharama za uzalishaji, kuongeza uwezo wa ufanyaji biashara na itasaidia kuongeza kiwango cha bidhaa kinachonunuliwa, ikilinganishwa na wakati ambao dola inakuwa iko juu.

“Kama unafanya biashara, unataka kununua bidhaa au malighafi, sasa utahitaji fedha kidogo za Tanzania kununua dola ili ulipie huduma. Kwa mfano manunuzi, kama mtu alikuwa ananunua kontena la malighafi kwa Sh20 milioni wakati dola iko juu, maana yake sasa utatumia Sh18 milioni, kiuchumi ni ukuaji,” anasema Rwehumbiza.

Hilo haliwanufaishi wafanyabiashara pekee, bali pia alitolea mfano wa Serikali katika ulipaji wa madeni yake ya nje, akisema sasa haitahitajika kutumia nguvu kukusanya fedha nyingi ili kupata fedha toshelevu na badala yake kiwango cha fedha za ndani kitakachotumika kitakuwa kidogo, lakini kinachotosha kutimiza mipango yao.

Katika upande wa mafuta, Mkurugenzi wa Chama cha wauzaji wa mafuta Tanzania (Taomac), Raphael Mgaya anasema matokeo ya hiyo yanamgusa zaidi mtumiaji wa mwisho ambaye ni mwananchi, kutokana na gharama ya mafuta kushuka.

Katika upande wao, itapunguza gharama za uendeshaji, kwani baadhi ya vituo vyao vinategemea mafuta kufanya shughuli zake za kila siku.

“Kwa upande wa magari ya kusafirishia bidhaa, watumishi, gharama zitakuwa chini kwa sababu mafuta yatashuka, lakini katika biashara moja kwa moja haitugusi kwa sababu sisi hatuathiriwi na kushuka wala kupanda kwa dola kama mdhibiti wetu anafanya kazi vizuri,” anasema Mgaya.

Related Posts